• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:10 PM
DAISY: Vijana wajiepushe na shinikizo zisizofaa mitandaoni

DAISY: Vijana wajiepushe na shinikizo zisizofaa mitandaoni

Na LUCY DAISY

KIWANGO cha juu cha ukosefu wa kazi nchini, misukosuko ya kiuchumi na maisha kwa jumla, anasa za ujana, na shinikizo za marika zimefanya vijana wa siku hizi kukumbwa na matatizo ya kiakili na kutumbukia katika msongo wa mawazo.

Wengi wao wana dhiki na huzuni kila siku ndiposa wanatumbukia katika dawa za kulevya na uraibu mwingine hatari ili kujiliwaza, na hali ikiwasonga zaidi wengine wanajitia vitanzi.

Kwa kweli maisha ya siku hizi ni magumu hasa kwa vijana ambao wengi wao hawana ajira, na walioajiriwa wanapata mishahara duni licha ya familia zao kuwategemea kwa kila kitu.

Ingawa vijana wanakumbwa na matatizo hayo, kwa maoni yangu kichocheo kikuu cha wao kutumbukia katika msongo wa mawazo ni presha za mtandaoni.

Siku hizi kila kijana yupo kwenye mitandao ya kijamii kuona jinsi wengine wanaendelea kimaisha.

Humo mitandaoni vijana wenzao wanaposti picha za kuashiria maisha kwao ni mteremko, na kuwafanya wao kuhuzunika wakiona kana kwamba ni wao tu hawajaendelea katika maisha.

Ukweli ni kuwa, hata hao wanaoposti picha nzuri nzuri, wengine wakionekana kusafiri na kujivinjari vilivyo, bado wana dhiki zao.

Wanajaribu kutumia mitandao ili kujipa moyo na kuficha matatizo chungu nzima yanayowakumba.

Mtandaoni ni mahali pazuri pa kujuliana hali, kujifahamisha kuhusu yanayojiri ulimwengu, kujifunga mawili matatu ya kujielimisha, kujinufaisha kupitia ajira za kidijitali, na kujiburudisha kwa raha zako.

Ni mahali ambapo wengi wamepatana na marafiki wa dhati na hata wengine kupata wachumba mle ndani.

Hata hivyo, vijana hawana budi kuepukana na presha wanazosukumiwa humo mitandaoni.

Wasilinganishe maisha ya kwao na ya wenzao wanavyojitangaza kwenye kurasa mbalimbali za kijamii.

Ukweli ni kwamba picha wanazoposti ni za kujigamba na kudanganya tu; uhakika ni kuwa wao pia wanang’ang’ana na maisha.

Hivyo vijana watazame tu picha za wenzao nzuri na posti za furaha, lakini wasikubali ziwape presha.

Isitoshe, wengi wanaposti vitu visivyo vyao halisi: gari, nyumba na mashamba, na hata nguo za kuazima ili tu waonekane kuwa wamefika mbali. Hawa wasikupe presha.

Hata iwapo kuna wale ambao kwa kweli maisha yao yanaendelea vyema, vijana wakumbuke kila mja ana siku yake.

Wasife moyo wala kuumia eti wao hawajafanikiwa kama wenzao; bali wajikakamue zaidi angalau pia wao wafanikiwe.

Wazazi na jamii kwa jumla haina budi kuwakumbusha vijana na watoto kwamba maisha sio yale wayaonayo mitandaoni.

Kwamba kila mja ana riziki yake na siku yake; wasipate presha. Cha muhimu ni wao kufanya bidii kuafikia malengo yao maishani.

Iwapo mitandao inawadhuru badala ya kuwasaidia, ni bora waachane nayo na waishi maisha yao polepole bila presha zisizofaa.

Viongozi wa kidini pia wanahitajika sana kuwapa vijana ushauri nasaha. Kuwakumbusha kuwa ni vyema watumie mitandao kwa njia ya hekima, inayofaa na kujinufaisha kihalali.

Pia wawaombee vijana wetu nyakati hizi ngumu wamerejelea Muumba wao ili wasipotee, wakajisahau na kukata tamaa.

You can share this post!

KAMAU: Kifo cha Dkt Mogusu kichochee Wakenya kushinikiza...

Umuhimu wa tunda la Pitaya yaani Dragon fruit