Gor Mahia na Ulinzi Stars kuwania taji la Jamhuri Day Cup
Na CHRIS ADUNGO
GOR Mahia wanatazamiwa kufufua uhasama wao dhidi ya wanajeshi wa Ulinzi Stars watakaposhuka dimbani mnamo Disemba 12 kwa mechi ya Ligi Kuu ya FKFPL ambayo pia itatumiwa kupata mshindi wa taji la Jamhuri Day Cup.
Vikosi hivyo havijawahi kushiriki mchuano wowote wa ligi msimu huu wa 2020-21 kutokana na mvutano uliozuliwa na dili ya kibiashara iliyotiliwa saini na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na shirika la StarTimes ambalo litakuwa likipeperusha matangazo ya baadhi ya mechi za kivumbi hicho moja kwa moja.
Sawa na Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi na washindi mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya, wanajeshi wa Ulinzi Stars ambao wametwaa ufalme mara nne, watapania kutia kapuni alama tatu muhimu na kunyanyua taji la kwanza muhula huu.
Mechi hiyo ambayo ilikuwa imeratibiwa hapo awali kuchezewa uwanjani Utalii Grounds sasa utapigiwa katika uga wa Nyayo, Nairobi.
Gor Mahia watatumia mchuano huo kama sehemu muhimu ya kujindaa kwa mechi ya mkondo wa kwanza katika raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria mnamo Disemba 22, 2020 jijini Algiers.
Hii ni baada ya FKF kukataa kuidhinisha mpango wa Gor Mahia kushiriki mechi ya kirafiki kati yao na Al-Hilal ya Sudan mnamo Disemba 16, 2020.
Mwenyekiti wa Gor Mahia, Ambrose Rachier amesisitiza kwamba Katibu Mkuu Sam Ocholla ambaye kwa sasa amesimamishwa kazi kwa muda, hakuidhinishwa na usimamizi wa kikosi kurasimisha mkataba kati ya FKF na StarTimes.
Kwa upande mwingine, Ulinzi walipewa na FKF siku tano zaidi kutia saini mkataba huo wa upeperushwaji wa matangazo ya mechi za ligi msimu huu au la watemwe kwenye orodha ya washiriki 18 wa kivumbi cha FKFPL muhula huu.