Habari

Utata wazidi kuzingira kifo cha seneta wa Machakos

December 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

SENETA wa Machakos, Boniface Kabaka aliaga dunia jana baada ya kulazwa Nairobi Hospital kwa wiki moja.

Kulingana na duru za familia zilizozungumza na Taifa Leo jana Ijumaa, kabla ya kuzirai wiki iliyopita katika hoteli moja na kupelekwa Nairobi Hospital, mwanasiasa huyo alikuwa akipata nafuu baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka hospitalini alimokuwa akitibiwa Covid-19.

“Alipokuwa akipata nafuu nyumbani, alianza kupata maumivu makali ya kichwa, jambo lililofanya madaktari wake kupendekeza uchunguzi wa MRI uliothibitisha kwamba alikuwa na uvimbe mdogo kichwani,” zilisema duru hizo.

Seneta Kabaka alilazwa Nairobi Hospital kwenye Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU) mnamo Ijumaa iliyopita baada ya kuugua katika chumba kimoja cha hoteli eneo la Kilimani, Nairobi, ambako anasemekana kujipeleka mwenyewe kwa gari lake kutoka nyumbani mwake.

Kulingana na msaidizi wake wa kibinafsi Jace Kyule ambaye ni binamu yake Seneta Kabaka, marehemu alikutana na rafiki yake wa miaka ya zamani waliyekuwa wakisoma pamoja kwa jina la Bi Esther Nthenya Muli katika hoteli moja ambapo walishiriki vyakula na vinywaji hotelini humo.

Mapema wiki hii, Bi Muli alifikishwa mahakamani ambapo polisi waliomba azuiliwe wakisubiri matokeo ya uchunguzi wa sampuli wa mlo waliokula ili kubaini kama kilikuwa na sumu.

Lakini baada ya matokeo ya maabara kuonyesha chakula hicho hakikuwa na sumu, Bi Muli aliachiliwa

Hapo jana, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alipuzilia mbali ripoti zinazosambazwa kuhusiana na kiini cha kifo cha Bw Kabaka akisema mwanasiasa huyo alifariki alipokuwa akifanyiwa upasuaji kwenye uvimbe uliokuwa kichwani mwake.

Viongozi wengine waliotuma rambirambi zao ni pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua aliyemsifu Bw Kabaka kama mtu mchangamfu aliyejitolea kuboresha maslahi ya watu wa Machakos.

Alitaja kifo cha seneta huyo kama pigo kuu kwa wakazi wa Kaunti ya Machakos kwa jumla.

“Kwa niaba yangu na watu wa Machakos, ninatuma rambirambi zangu kwa familia ya seneta mpendwa Boniface Kabaka ambaye ameaga dunia baada ya kushikwa na kiharusi kutokana na uvimbe wa mshipa wa damu ambao umekuwa ukimsumbua kwa muda,” alisema Dkt Mutua.