MWANAMUME KAMILI: Ole wenu mliozika akili ulevini, mtajua Desemba tanuri la moto
Na DKT CHARLES OBENE
DESEMBA ni moto kuliko tanuri la moto.
Pindi tu mshale wa saa ulipogonga tarehe moja Desemba, zile minong’ono na wasiwasi za wanaume kwa wanawake zilianza tena kuvuma kwa kasi.
Wenye kulia na kulilia hali ngumu ya maisha wamekwisha anza kulaumu mwezi wa Desemba kwa kuwa umefika haraka tena bila taarifa.
Huu umekuwa ndio mtindo wa kawaida, wanaume kwa wanawake kujawa mhemko na wengine kuzidisha mikwala kana kwamba wamejawa milihoi. Nani aliwarithisha hii mirimo ya Desemba ilhali kila kukicha mmeishi maisha ya patapotea, raha kuponda, minofu na mifupa kuguguna na vinywaji kuteremesha kooni?
Kwa ghafla, zile mbwembwe za majike na madume zimekatika, wanenguaji na walaji surua wamesitishwa na jekejeke angalau kusikiliza mwangwi ukivuma na kuwakumbusha kwamba mwisho wa mwaka unabisha tena kwa nguvu! Hamna budi kusimama, japo dede, na kuzikabili hizo jelezi zenu. Ndio kwanza mkoko unaalika maua! Januari mwanzoni hadi Novemba mmeishi kama watu wenye vyao. Kula mmekula shibe yenu.
Kunywa mmekunywa na ardhi ikanywa vilevile. Waliopata uraibu kuchana majani hawakusaza kitu. Hata meno na fizi zimekwisha pata umbijani!
Kunani enyi wenye dunia mliodunisha akina sisi walalahoi pesa kuzimwaga mezani na nyingine kuwazawadi mashangingi waliofika vilabuni kuwatumbuiza wakiwa wamevalia mfano wa kumbikumbi! Nakumbuka enzi za udogoni bibi akinisuta kwa kutembea kama kumbikumbi. Kweli, sikuvalia chochote chini.
Hivyo ndivyo wanavyofanya hawa watumbuizaji tunaowalipa pesa kuwatazama vilabuni. Kando na kuponda raha, janga la virusi vya Corona limetuduwaza, wengi wetu tukasalia hatuna kazi hatuna bazi. Tunaishi kubahatisha na kula mwikoni mfano wa mende.
Ninaelewa tosha asili fasili ya butwaa kutuvaa ghafla. Ndio sasa inatupambazukia kwamba mwakani tunahitajika kuwarudisha watoto shule. Hilo la kuwarudisha shule ndio nafuu. Wanaotarajiwa kwenda shuleni ndio kwanza mahambe waliopotoka afadhali nguruwe mcheza topeni. Tumewaachia wajakazi kuwalea na kuwafunza nyumbani; sisi wenyewe tukitafuta maisha! Wamecheza wakachana hadi sare za shule. Wamelala wakalaza damu na bongo zao. Ole nyinyi walimu wanaotarajiwa kuzikwamua hizi bongo zilizolala kwa mwaka mmoja. Afadhali kufufua maiti.
Desemba inatuzolea dhiki maradufu. Ndio kwanza tunakumbuka zile desturi za watu kwenda kujivinjari likizoni, jamii na jamaa kutangamana kula na kunywa pamoja, wanawake kwa watoto kuzawadiwa majozi ya viatu na nguo patanifu! Wajua tena ukarimu wa wanaume wa leo kuwavisha wengine wenyewe wakavalia vimori kana kwamba wanazoa majitaka! La ajabu ni kwamba wanaume wamereresheka mashangingi kuwarembesha ilhali hawajapanga lolote wala kuekeza popote kwa manufaa ya watoto na wake zao. Msione hofu tanuri la moto wa Desemba kuwaoka mfano wa keki.
Mnaweza kataa katakata kutumia zenu akili kwa wakati ufaao lakini mwezi wa Desemba umekwisha bisha hodi hamna chenu nyinyi wenye vichwa vya mawe na bongo za uji. Mtajuta kufuja pesa kwenye anasa na ulimbukeni wa mwanamume wa leo.
Kwa kuwa mambo ya sasa yanakwenda kwa kasi ya umeme, mwanamume mwenye mawazo chanya na akili timamu hana budi kujituma ipasavyo tena kwa wakati unaofaa ili kufanikisha maisha yake na maisha ya familia wanaomtegemea. Badala ya kuwazia anasa kila kukicha, mwanamume kamili anapasa kuwazia mambo ya tija tena mazito yanayofaidi jamaa na jamii.
Kuche kusiche, akili na mawazo ya mwanamume kamili yanastahili kulenga jinsi watoto watakavyosoma, watakavyolelewa, na vipi kuwapa motisha kukabiliana na majanga yanayozonga jamii. Na ikiwa hana mtoto haidhuru! Huu ndio wakati wa mwanamume kufika sokoni kuuza sera na kujaribu bahati angalau kuanza safari ya kuwa mwanamume kamili. Huu sio muda wa mwanamume kuzika akili ulevini na kuwatelekeza watoto na wanawake nyumbani. La sivyo mtakuja tambua ukweli kwamba Desemba ni moto tena unaoteketeza kuliko tanuri la moto.