CHOCHEO: Krismasi bila sherehe, itakuwaje?
Na BENSON MATHEKA
KILA Desemba Shiru huwa anafurahia kukutana na jamaa zake ushago kwa sherehe za Krismasi kwa siku tatu kabla ya kurejea mjini kuungana na mpenzi wake Nderitu kuukaribisha mwaka mpya.
Lakini mwaka huu anahisi kuwa hataweza kusafiri mashambani Mathira, Kaunti ya Nyeri kwa sababu ya janga la corona.
“Tumekubaliana kama familia kwamba hatutakuwa na sherehe ya familia mwaka huu. Hatutaki kuhatarisha maisha yao msimu huu wa janga la corona hasa wale walio na umri mkubwa,” asema Shiru.
Hata kama hatua hii itampa fursa ya kuwa na mpenzi wake kwa muda mrefu wakati wa sherehe za Krismasi, itabidi wawe waangalifu sana. “Mimi na Nderitu tumeamua kutotembelea sehemu za burudani zilizo na watu wengi ili tuepuke kujiweka kwenye hatari ya kuambukizwa virusi hivi. Tungesafiri hadi Watamu lakini tumeamua kujivinjari Nairobi kwa usalama wa afya zetu,” asema.
Wataalamu wa afya na mahusiano wanasema kuwa sherehe za Krismasi mwaka huu zitakuwa tofauti kwa watu wanaoelewa hatari iliyomo. “Tunajua watu wamezoea kuthibitisha upendo kwa familia na mapenzi kwa wachumba wao wakati wa Krismasi. Familia huwa zinaandaa sherehe kubwa za kushukuru ambapo watu husafiri kutoka maeneo mbalimbali kuungana na jamaa zao. Tunashauri kwamba wafute sherehe na safari mwaka huu kuepusha hatari ya kusambaza virusi vya corona,” asema Meshack Omondi wa shirika la Love Care, Nairobi.
Meshack anasema kuwa tafiti zimeonyesha hata sherehe ndogo za kifamilia zinaweza kuchangia ongezeko la maambukizi ya corona jinsi ilivyofanyika Canada mwezi Oktoba familia zilipoandaa hafla za kutoa shukrani.
Kulingana na utafiti wa shirika la Ipsos Canada, nchi hiyo ilikuwa na watu 185,000 waliokuwa wameambukizwa corona kufikia Oktoba 12. Baada ya sherehe hizo, idadi hiyo iliongezeka maradufu. Hii ilitokana na watu kuandaa sherehe ndogo za kifamilia licha ya kuonywa kuziepuka. “Watu walionywa lakini familia chache zilipuuza na kukutana na wapendwa wao. Tunaona matokeo kutokana na maambukizi kuongezeka,” Ipsos ilisema kwenye ripoti yake.
Kulingana na Meshack, watu wanapaswa kuweka breki safari za mashambani na kuhudhuria burudani katika maeneo yaliyo na msongamano wa watu msimu huu wa sherehe. “Huu ndio wakati wa wapenzi kubuni mbinu mbadala za kudhihirisha mapenzi. Anayekupenda hatakushurutisha umpeleke katika kumbi za burudani au usafiri kwa matatu kwenda kumtembelea. Ikiwa anakulazimisha, basi hakupendi. Anayekupenda kwa dhati atakuambia kaa nyumbani kwa usalama wa afya yako,” asema Meshack.
Wataalamu wanasema hata hafla za chini ya watu kumi zimehusishwa na ongezeko la maambukizi katika nchi tofauti ulimwenguni. “Njia salama pekee ya watu kukutana msimu wa sherehe mwaka huu ni kupitia video mtandaoni. Mikutano hii ndiyo suluhu kwa wakati huu kote ulimwenguni,” Dkt Iahn Gonsenhauser, mkuu wa usalama wa wagonjwa katika Wexner Medical Center, chuo kikuu cha Ohio, Amerika aliambia jarida la Huffpost.
Anasema ili watu waweze kukinga wapendwa wao wasiambukizwe corona, wanafaa kuepuka kusafiri kukutana nao msimu wa sherehe mwaka huu. “Itabidi watu wavumilie mwaka huu ili kuweka jamii ikiwa salama. Kuna matumaini kwamba mambo yatakuwa sawa Desemba 2021 wakitii kanuni za kukabili janga hili na chanjo zikipatikana,” asema Dkt Iahn.
Hivi ndivyo anavyoamini Jerusha, mwanadada mwenye umri wa miaka 26 anayesema ingawa anampenda mchumba wake kwa dhati, hataweza kusafiri Afrika Kusini kuwa naye msimu huu. “Tulikubaliana kwamba kwa usalama wetu, tutawasiliana kwenye mtandao. Tungetaka kukumbatiana na kulishana mapenzi ‘mundu kumundu’ lakini afya yetu ni muhimu zaidi,” asema Jerusha.
Wataalamu wa afya wanasema ingawa maambukizi yamesambaa kote nchini, watu wanaweza kujikinga kwa kuepuka kusafiri msimu huu wa sherehe na kuepuka maeneo ya burudani yenye watu wengi.