COVID-19 yachelewesha kipute cha Ligi Kuu ya Wanawake KWPL
Na CHRIS ADUNGO
KUPULIZWA kwa kipenga cha kuashiria rasmi mwanzo wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini Kenya (KWPL) kumecheleweshwa na vipimo vya corona kwa siku moja zaidi.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ambao ni waandalizi wa kivumbi hicho ambacho sasa kitaanza Disemba 13 badala ya Disemba 12, 2020, vipimo vya corona vilikawia kuanza kwa siku tatu zaidi kinyume na jinsi ilivyotarajiwa.
Awali, vipimo hivyo vya lazima kwa kila mchezaji na maafisa wa benchi za kiufundi za klabu zote zinazoshiriki KWPL, vilitarajiwa kufanywa kati ya Disemba 7-9, 2020. Badala yake, vipimo hivyo vilianza Alhamisi ya Disemba 10, 2020, na wadau wote wanatarajiwa kupokea matokeo ya vipimo hivyo kufikia Disemba 12, 2020.
Vikosi mbalimbali vya Zoni A na Zoni B vilishiriki vipimo vya corona katika viwanja vyao vya mazoezi. Mabingwa watetezi Vihiga Queens kutoka Zoni B walifanyiwa vipimo katika uwanja wa Kidundu, Kaunti ya Vihiga huku Makolanders wa Kundi A wakiwa katika uwanja wa Buruburu Sports Complex, Nairobi.
Kocha Alex Alumira wa Vihiga Queens amesema kwamba kikosi chake kiko tayari kushuka dimbani kuvaana na Wadadia ambao watakuwa wageni wao uwanjani Mumias Complex.
Makolanders ambao waliambulia nafasi ya 10 katika kampeni za msimu wa 2019-20, wameratibiwa kuchuana na Kibera Girls Soccer Academy katika mechi ya kwanza ya msimu uwanjani Camp Toyoyo.
Msimu mpya wa 2020-21 utahusisha vikosi vya Ligi Kuu ya KWPL na Ligi ya Daraja la Kwanza pekee huku kila mojawapo ikijivunia vikosi 12 katika kila mojawapo ya zoni.