Kenya yapanda vikapuni kwa nafasi saba zaidi hadi nambari 115 kwenye orodha ya dunia
Na CHRIS ADUNGO
USHINDI wa 79-62 uliosajiliwa na wanavikapu wa Kenya Morans mnamo Novemba 27, 2020, dhidi ya Msumbiji katika mojawapo ya mechi za Kundi B kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AfroBasket) jijini Kigali, Rwanda umechangia kupanda kwa Kenya kwenye orodha ya Shirikisho la Vikapu Duniani.
Kenya kwa sasa imeorodheshwa ya 115 baada ya kupanda kwa nafasi saba kwenye orodha hiyo ya FIBA licha ya kupokezwa vichapo vya 92-54 na 83-66 kutoka kwa Senegal na Angola mtawalia katika mechi mbili za ufunguzi wa Kundi B kwenye mchujo wa AfroBasket mnamo Novemba, 2020 nchini Rwanda.
Sudan Kusini ambao ni majirani wa Kenya walipanda kwa nafasi tisa hadi nambari 98 kwa sasa baada ya kupepeta Rwanda na Mali jijini Kigali chini ya kocha Luol Deng aliyewahi kutamba katika enzi zake akichezea vikosi vya NBA.
Morans walitua Rwanda kwa minajili ya mechi hizo za mkondo wa kwanza katika juhudi za kufuzu kwa fainali za AfroBasket wakikamata nafasi ya chini zaidi kwenye Kundi B. Waakati huo, walikuwa wakishikilia nambari 122 duniani huku Angola, Senegal na Msumbiji wakiwa katika nafasi za 32, 35 na 93 mtawalia.
Kwa mujibu wa orodha ya viwango bora vya hivi punde vya FIBA, Amerika bado kileleni huku Uhispania ikishikilia nafasi ya pili duniani. Urusi ndicho kikosi cha pekee kipya kilichoingia ndani ya mduara wa 10-bora baada ya kupanda kwa nafasi mbili zaidi hadi nambari tisa. Wamechukua nafasi ya Jamhuri ya Czech ambao kwa sasa wameteremka hadi nafasi ya 11 duniani baada ya kupigwa na Denmark na Ubelgiji kwenye mchujo wa kufuzu kwa fainali za FIBA EuroBasket mnamo 2022.
Kupanda kwa Urusi kulichangiwa na ushindi wa 84-56 waliosajili dhidi ya Estonia kabla ya chombo chao kuzamishwa na Italia 70-66.
Italia waliocheza mechi moja pekee mnamo Novemba 2020, walisalia katika nafasi ya 12 duniani licha ya pointi zao kushuka hadi 582.5.
Mabingwa watetezi wa EuroBasket, Slovenia, walipanda kwa nafasi mbili zaidi hadi nambari 16 baada ya ushindi waliosajili dhidi ya Ukraine na Austria mnamo Novemba kuimarisha zaidi nafasi yao ya kufuzu kwa fainali zijazo. Slovenia walichupa kutoka nafasi ya tatu hadi ya kwanza kwenye Kundi F katika mechi hizo za kufuzu.
Ushindi dhidi ya nambari mbili Uhispania na Poland wanaoshikilia nafasi ya 13 duniani ulisaidia Israel kupanda kwa nafasi mbili zaidi kutoka 41 hadi 39 kwenye orodha ya vikosi bora duniani.
Syria na Saudi Arabia ndio walioimarika zaidi kwenye orodha hiyo miongoni mwa vikosi vya bara Asia. Syria walipanda kwa nafasi tano hadi 90 huku Saudi Arabia nao wakipanda kwa nafasi tano zaidi hadi nambari 91 duniani. Vikosi hivyo viliambulia sare vilipokutana mara ya mwisho mnamo Novemba, 2020.
Barani Ulaya, Albania walipanda kwa nafasi saba na kuingia ndani ya mduara wa 100-bora baada ya kushinda Ureno na Belarus kwenye mechi mbili za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za mnamo 2023 na Euro 2021.
Kikosi kilichoshuka chini zaidi kwenye orodha mpya ya FIBA ni Madagascar kilichoteremka kwa nafasi 30 hadi nambari 124 baada ya kupoteza mechi zote tatu za kufuzu kwa fainali za AfroBasket nchini Rwanda mnamo Novemba 2020. Kikosi hicho kilipigwa na Tunisia kwa pointi 37 kabla ya Central African Republic na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kukipiga kwa pointi 26 na 18 mtawalia.