Michezo

Anthony Joshua amdengua Kubrat Pulev kwa Knock-Out (KO)

December 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MWINGEREZA Anthony Joshua, 31, alifaulu kutetea mataji yake ya WBA, WBO, IBF na IBO baada ya kumshinda Kubrat Pulev wa Bulgaria kwa njia ya Knockout (KO) kwenye raundi ya tisa katika pambano la uzani wa juu mbele ya mashabiki 1,000.

Mchapano huo ulifanyika katika ukumbi wa SSE Arena, uwanjani Wembley, jijini London, Uingereza mnamo Disemba 12, 2020.

Baada ya kushinda pambano la 25 kati ya 26 aliyoshiriki awali, akiwa amepigwa moja tu – sasa Joshua anaweza kupanda ulingoni kupigana na Mwingereza mwenzake, bingwa wa WBC, Tyson Fury katika pambano la kuunganisha mataji.

Joshua alikuwa anapigana kwa mara ya kwanza tangu arejeshe mataji yake hayo nchini Saudi Arabia mnamo Disemba 2019 kwa kumshinda Andy Ruiz Jr wa Mexico na kulipiza kisasi cha Juni 2019.

Kwa upande wake, pigano la Disemba 12 lilikuwa la pili kwa Pulev, 39, kupoteza kati ya 29 yaliyopita baada ya kuzidiwa maarifa na Wladimir Klitschko kwa mara ya kwanza mnamo 2014.

Ushindi wa Joshua aliyefaulu kuhifadhi taji lake la bingwa wa uzani wa juu zaidi dunia kwa mara ya tatu, ulisherehekewa pakubwa na mamilioni ya watu hasa Magharibi wa mji wa Sagamu, Nigeria inakotokea familia ya mwanamasumbwi huyo.

Familia ya Joshua inajulikana sana Sagamu ambako mababu wake walizaliwa. Babu yake mkuu, Daniel Adebambo Joshua, tajiri aliyemiliki ardhi na mfanyabiashara mashuhuri, anasadikiwa kubatizwa jina lake la mwisho baada ya kijiunga na dini ya Kikristo.

Daniel alimpeleka mwanawe wa kiume Isaac Olaseni Joshua kwa msomo ya juu nchini Uingereza ambako hatimaye alioana na mwanamke kutoka Ireland na kurudi naye nyumbani Nigeria na kuzaa na kulea watoto saba pamoja.

Mmoja wa watoto hao, Robert aliishia kumuoa Yeta Odusanya, pia kutoka Sagamu, ambayea pia ni baba yake Anthony na dada yake Janet.

Jina lake la katikati, Olaseni, alipewa kwa heshima ya babu yake. Shughuli zake za michezo hivi karibuni zimehakikisha jina la familia linakuwa maarufu si tu katika mji huo, bali pia ndani na nje ya nchi.

Joshua anajivunia sana chimbuko lake la Nigeria ikizingatiwa kwamba ana mchoro na chale ya kudumu inayoonyesha ramani ya bara la Afrika. Chale nyingine pia ina bendera ya Nigeria kwenye bega lake la kulia.

Muziki uliochezwa wakati akiingia ulingoni katika mapigano yake mawili ya awali dhidi ya Andy Ruiz Jr ulikuwa wa wasanii nyota kutoka Nigeria – Burna Boy na Femi Kuti, mwana wa kiume wa nguli wa muziki wa Kiafrika, Fela Kuti.

Mapenzi yake kwa muziki wa Nigeria yanaonekana katika mitandao yake ya kijamiii ambako huwa akipakia video yake akiimba nyimbo kutoka nchi hiyo ya Afrika Magharibi .

Joshua anamiliki pia klabu yake ya mashabiki mjini Sagamu ambayo aliianzisha mnamo 2017 kabla ya pigano lililoimarisha taaluma yake dhidi ya Wladimir Klitschko.

“Joshua ameiweka Sagamu kwenye ramani kubwa ya dunia,” Azeez Adekunle Okunoren almaarufu ‘Bwana Naira’ ambaye ni mwanzilishi wa klabu ya mashabiki ya Anthony Joshua, aliwahi kunukuliwa na BBC.