JAMVI: Uungwaji mkono na Rais wamweka Boga pazuri
Na MOHAMED AHMED
KARATA za kisiasa zinazochezwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Msambweni zimeonekana kuwazidi maji wapinzani wa chama cha ODM.
Wakati kampeni za kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Msambweni zinakamilika leo (Jumapili), Bw Joho ambaye amekuwa akiongoza siasa za mgombea wa ODM Omar Boga amehakikisha kuwa anawazima wapinzani wao kwa mpango kabambe.
Mnamo Alhamisi, Bw Joho alihakikisha kuwa amemkutanisha Bw Boga na Rais Uhuru Kenyatta jambo lililoonekana kuwathibitishia na kuwazima midomo wale waliokuwa wanapinga kuwa Boga ni mgombea wa “handisheki”.
Baada ya Bw Boga kukutana na Rais Kenyatta, picha zilisambazwa mitandaoni na wafuasi wa Boga wakiwazomea wapinzani wao ambao walikuwa wanapinga kuwa mgombea huyo anaungwa mkono na serikali ya Rais.
Bw Joho alimkutanisha Rais Kenyatta na Bw Boga wakati wa uzinduzi wa daraja la kuelea la Likoni eneo la Liwatoni ambapo watatu hao walikuwa na mazungumzo mafupi kabla ya kuja mbele ya wanahabari.
“Mimi niko hapa na mgombea wangu wa kule Msambweni ambaye ni Bw Boga. Nimetembea kule na nikaona kuwa serikali yako inaweza kutusaidia kuangalia baadhi ya shida za watu wa huko na nakuomba Rais utusaidie kwa hilo kupitia huyu Boga,” akasema Bw Joho wakati alipomuita rasmi Bw Boga mbele ya Rais.
Baada ya mazungumzo yake kuhusiana na miradi ya maendeleo eneo la Pwani, Rais Kenyatta akamuamuru waziri wa uchukuzi James Macharia ambaye alikuwa ameandamana naye na kumueleza aangalie maswala hayo ya watu wa Msambweni.
“Utaangalia hayo mambo ya barabara na daraja ambalo tumeambiwa hapa na hayo mambo ya soko pia,” akasema Rais Kenyatta kabla ya kumaliza mazungumzo yake kwa wananchi waliokuwa wamejitokeza kumlaki.
Kukutana kwa Bw Boga na Rais Kenyatta kulikuja saa chache tu baada ya mgombea huyo wa ODM kuandamana na kinara wa chama Raila Odinga ambaye Jamvi limetambua kuwa alichangia kusukuma ajenda hiyo ya mgombea wake kukutana na Rais Kenyatta.
Sasa, wachanganuzi wa masuala ya siasa wameeleza kuwa kukutana kwa Bw Boga na viongozi hao wawili kutampa jeki mgombea huyo kwa kukuthibitishwa kuwa “mgombea wa serikali”.
Kauli hiyo ya kuwa Boga ni mgombe wa serikali imekuwa ikiendeshwa na Bw Joho na kupingwa vikali na Gavana wa Kwale Salim Mvurya ambaye amekuwa akiendesha kampeni za hasimu wa karibu wa Boga, mgombea huru Feisal Bader.
Bw Bader anaungwa mkono na Naibu Rais William Ruto pamoja na baadhi ya wabunge wa Kwale na Mombasa.
Katika mkutano na wazee wakati alipokuwa anamfanyia kampeni Bw Boga, Bw Odinga alisema kuwa ushindi wa mgombea huyo ni mwanzo wa ushindi wa ripoti ya jopokazi la maridhiano (BBI).
“Uchaguzi huu ndio utathibitisha mwelekeo wa BBI ndio maana tunataka tushinde kwa asilimia Zaidi ya 80 ama hata 90. Sisi tuko na umoja sasa na Rais na tunaendesha hii ajenda pamoja,” akasema Bw Odinga akiwa Diani.
Licha ya viongozi hao wa ODM kundesha ajenda hiyo kuwa Bw Boga ni mgombea wa serikali, Bw Mvurya amekuwa akipinga madai hayo na kuwaeleza wananchi kuwa hakuna mgombea wa serikali.
Katika kampeni ambazo amekuwa akiendesha, Bw Mvurya amekuwa akisema kuwa yeye ndio Gavana wa chama cha Jubilee na Rais Kenyatta ndio kinara na hivyo basi hakuna mtu yoyote ambaye amechaguliwa kuwa mgombea wa serikali.
“Musisikize hizi porojo kuwa kuna mgombea wa serikali. Mwanzo mimi nataka kuwaambia kuwa siasa za chama zilipitwa na wakati. Musichague chama kwa sababu sio chama ambacho kinaleta maendeleo bali ni mtu binafsi,” anasema Bw Mvurya.
Ikiwa malumbano hayo leo yanafikia mwisho, itasubiriwa wapiga kura kuamua yule ambaye wanaemtaka katika nafasi hiyo ya ubunge wa Msambweni.
Kura za uamuzi huo zitapigwa mnamo Jumanne na mshindi kutambulika siku ifuatayo iwapo mipango ya uchaguzi huyo yataenda kama yalivyopangwa.
Wapiga kura pia watakuwa na fursa ya kuwachagua wagombea wengine ambao wapo kwenye kinyangányiro hicho mbali na Bw Boga na Bw Bader ambao ndio wameibuka kuwa wagombea wakuu kwenye uchaguzi huo mdogo.
Wagombea hao wengeni ni Charles Bilali na Mansury Kumaka (wagombea wa kujitegemea), Shee Abdulrahman (Wiper), Khamis Mwakaonje (United Green Movement), Ali Hassan Mwakulonda wa chama cha Peoples Economic Democracy (PED) na Mwarere Wamwachai.