• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
WASONGA: Haikufaa Rais kupuuza madaktari na kupigia debe BBI

WASONGA: Haikufaa Rais kupuuza madaktari na kupigia debe BBI

Na CHARLES WASONGA

NI jambo la kuvunja moyo kwamba Rais Uhuru Kenyatta aliamua, kimakusudi, kutumia maadhimisho ya 57 Siku Kuu ya Jamhuri Dei kama jukwaa la kupigia debe mageuzi ya Katiba yanapendekezwa kupitia mpango wa maridhiano (BBI).

Hotuba yake katika uwanja wa Nyayo, Nairobi iliyoakisi kampeni ya kuwahimiza Wakenya kupiga kura ya “NDIO” katika kura ya maamuzi ya kuhusu mageuzi hayo huku akichelea kuzungumzia masuala mengine yenye umuhimu kwa taifa hili.

Kwa mfano, Wakenya wengi walitarajia kiongozi wa taifa kuweka bayana mikakati ambayo serikali yake imeweka kukabiliana changamoto zinazoisibu sekta ya afya nchini.

Sawa na raia wengine nilitarajia kuwa Rais Kenyatta angetoa maagizo mapya yatakayosaidia kukomesha mgomo wa wauguzi na wahudumu wengine wa afya unaoendelea pamoja na mgomo wa madaktari ambao umeratibiwa kuanza Desemba 21.

Lakini Rais hakutoa mwelekeo wowote kuhusu suala hilo ambalo ni lenye umuhimu mkubwa mno wakati kama huu wa janga la Covid-19. Tulitarajia Rais Kenyatta angetangaza jinsi serikali yake kwa ushirikiano na zile za kaunti zigetimiza matakwa ya wahudumu hao wa afya ili warejee kazini na kuwaondolea wagonjwa mateso.

Hii ni kwa sababu nguzo moja katika Agenda Nne Kuu ya maendeleo ya serikali yake ni Afya kwa Wote. Azma hii haiwezi kufikiwa ikiwa sekta ya afya itaendelea kuzongwa na migomo ya kila mara wahudumu wa afya wakilalamikia nyongeza za mishahara, marupurupu, vifaa vya matibabu miongoni mwa mahitaji mengine ya kimsingi.

Pili, nilitarajia hotuba ya Rais Kenyatta ingeangazia mada hii ya afya kwa sababu taifa hili lilipopata uhuru mwaka 1963, mojawapo ya maadui ambayo waanzilishi wake waliazimia kupambana nayo ni magonjwa. Mengine ni ujinga na ufukara ambayo makali yake huathiri wanadamu zaidi endapo wataendelea kuzongwa na magonjwa.

Kinaya ni kwamba, miaka 57 baada ya Kenya kupata uhuru wa kujitawala, changamoto kubwa inayoathiri wananchi imesalia kuwa magonjwa. Idadi kubwa ya watu wamekuwa wakifariki kutokana na magonjwa yanayoweza kudhibitiwa kama vile Malaria, ishara kwamba asasi zetu za kiafya zingalifu dhaifu.

Mlipuko wa janga la Covid-19 mnamo Machi 13 mwaka huu ulifichua ukweli kuhusu hali hii. Imebainika kuwa hospitali nyingi haswa zile za umma hazina dawa na vifaa hitajika vya tiba.

Isitoshe, kuna idadi ndogo ya wahudumu wa afya katika hospitali hizo ikilinganishwa na idadi ya watu wanaohitaji huduma.

Kwa hakika ni aibu kwamba Rais Kenyatta anaweza kuhutubia taifa wakati wa Sikuu Kuu muhimu kama Jamhuri Dei pasina kuangazia masuala kama hayo ambayo yenye umuhimu mkubwa kwa taifa hata kuliko mageuzi ya katiba.

[email protected]

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Baada ya dhiki ya miaka 13, ‘uboho mpya’...

KAMAU: Binadamu ni mwepesi wa kusahau akifanikiwa