Makala

NGILA: Tusikubali mitandao ya kijamii kuiba data zetu

December 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na FAUSTINE NGILA

HATUA ya serikali ya Amerika kuziamrisha kampuni tisa za mitandao ya kijamii kueleza kwa kina jinsi zinavyokusanya data ya watumizi kwa manufaa ya kuboresha matangazo ya mitandaoni ni mwamko mpya kwa juhudi za kukomesha matumizi mabaya ya data duniani.

Kampuni hizo – Amazon, Facebook, TikTok, Discord, Reddit, Snap, Twitter, WhatsApp na YouTube zimepewa siku 45 kuwasilisha maelezo kamili kuhusu teknolojia zinazotumia kuwatumia mabilioni ya watu duniani matangazo kulingana na hulka zao.

Kwa mujibu wa Tume ya Kudhibiti Biashara nchini humo, kampuni hizi zinafaa kufichua vigezo ambavyo zinatumia kutambua mienendo ya watumizi wake, na zinavyojua ni matangazo yapi ya kuwatumia watu hao.

Pia, zimetakiwa kutoa data kuhusu watu wanaofikiwa na matangazo hayo na jinsi yanawaathiri watoto na matineja.

Tangu mwaka wa 2005 ambapo kampuni hizi ziliasisiwa, zimekuwa zikitumia ujanja wa kidijitali kufuatilia maisha ya kila mtumizi wa huduma zake, na kutumia data hiyo bila idhini ya watumizi kuuza matangazo ya matrilioni ya pesa.

Kwa kutumia teknolojia za kisasa, zimeweza kutambua mahali tunapoishi, tunachofanya, tunachokula, tunaposafiri, tunaozungumza nao na pia biashara zetu huku zikiandika masharti mengi hasi kwa watumizi wanapofungua akaunti za kwanza na kuwashurutisha kuyakubali.

Kupitia mbinu hiyo, zimefanikiwa kukusanya mienendo yako na kuhifadhi data hiyo kwa seva zake ili kukutumia matangazo bila idhini yako, kuhusu mambo unayofanya mitandaoni.

Matangazo

Kampuni hizo, ambazo zinajivunia mamilioni ya watumizi hapa Kenya, zina uwezo wa kubashiri wananchi wa umri na jinsia mbalimbali watakachofanya katika miezi au miaka ijayo na kuzisaidia kampuni kuwatumia matangazo ya bidhaa zake baada ya kulipa ada.

Kwa ufupi, tumekuwa watumwa wa mitandao hii isiyojali hali zetu za umiliki wa taarifa kutuhusu. Tumezipa uhuru wa kutumia data yetu kufanyia biashara bila kutuhusisha.

Hata baada ya Kenya kuunda Sheria ya Ulinzi wa Data mwaka uliopita, suala zima la matumizi ya data kuhusu wananchi na kampuni za kimataifa liliachwa nje, huku kampuni za humu nchini zinazofanya hivyo zikiwekewa adhabu ya kitoto.

Sh5 milioni si adhabu tosha kwa kampuni ambayo imeiba data ya Wakenya milioni 30 na kuiuza bila kujali na kuvuna mabilioni ya hela.

Ikilinganishwa na Sheria ya Data ya Bara Ulaya, sheria na kanuni zetu za matumizi ya data ni hafifu. Hii inamaanisha kuwa iwapo Amerika itapiga marufuku baadhi ya kampuni hizi kutumia data wa Waamerika, kampuni hizo sasa zitajitosa kwenye bara la Afrika ambapo mataifa mengi bado hayana sheria za kulinda data ya wananchi wake.

Kwa kuwa Kenya sasa inajivunia kuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza Afrika kuwa na Afisi ya Kamishna wa Data, tunafaa kuimarisha kanuni zetu na kushurutisha kampuni zote za kigeni, hasa zinazotegemea uchanganuzi wa data ya Wakenya kurina mabilioni, kuzifuata la sivyo zilipe faini ya mabilioni.

Tukifanya hivyo, tutakuwa tumewekea Afrika msingi na mkondo wa kufuata katika juhudi za kuzima kampuni za kigeni kumumunya hela kutokana na taarifa zetu kinyume cha sheria.