• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
UTAMADUNI: Vazi la kumtawaza Ruto lazua mvutano wa wazee

UTAMADUNI: Vazi la kumtawaza Ruto lazua mvutano wa wazee

FLORAH KOECH na WYCLIFF KIPSANG

VAZI la kitamaduni alilovikwa Naibu wa Rais William Ruto wakati wa kutawazwa kuwa mzee wa jamii ya Watugen hapo Jumamosi, limezua mvutano miongoni mwa wazee huku kukiwa na madai kuwa ‘liliibwa’.

Wazee waliomtawaza Naibu wa Rais katika hafla iliyofanyika Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo, Ijumaa walipuuzilia mbali madai kwamba vazi linalojulikana kama ‘sambut’ alilovikwa Bw Ruto lilichukuliwa kwa mzee mkongwe bila kumfahamisha.

Wazee hao walizungumza baada ya Mzee Kimitei Kiplagat, 93, mkazi wa kijiji cha Kapkoi kuambia vyombo vya habari kuwa vazi lililotumiwa katika hafla hiyo ni lake na lilichukuliwa bila idhini yake.

Lakini kundi la wazee walioongozwa na Elijah Kimanyim lilidai kuwa vazi hilo halikuazimwa kutoka kwa Mzee Kiplagat.

“Sisi ndio tulimtawaza Naibu wa Rais kuwa mmoja wa wazee wa jamii ya Watugen alipozuru eneo la Eldama Ravine wiki iliyopita. Tumeshangaa kusikia kwamba vazi lililotumiwa lilichukuliwa kwa Mzee Kiplagat. Hatumjui na wala hatukuazima vazi hilo kutoka kwake,” akasema Bw Kimanyim.

Alisema madai hayo si ya kweli na yanalenga kumpaka tope Bw Ruto kutokana na sababu za kisiasa.

“Tunapenda kueleza Wakenya kuwa vazi alilovikwa Bw Ruto wakati wa kutawazwa kuwa mzee wa jamii ya Watugen katika eneo la Eldama Ravine halikuchukuliwa kutoka kwa mtu yeyote. Hafla hiyo ilikuwa ‘takatifu’ na wale ambao hawajaridhika wanaweza kuandaa sherehe yao,” akasema Bw Kimanyim.

Bw Kiplagat alikuwa amedai kuwa rafikiye aliazima vazi hilo kwa ajili ya sherehe ya kitamaduni Desemba mwaka jana lakini hakulirejesha.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Bw Kiplagat alidai vazi lake lililotengenezwa kwa ngozi ya tumbili mweusi ndilo lilitumiwa kumvika Bw Ruto.

Lakini Mzee Kenneth Sang, alisema Bw Ruto tayari amebarikiwa na wazee hao na sasa yuko tayari kuongoza Wakenya.

Mzee Sang’ aliambia Taifa Leo kuwa yeye ndiye aliazima vazi hilo huku akikanusha madai kwamba lilimilikiwa na Mzee Kiplagat.

“Mimi ndiye niliazima vazi hilo lakini nataka kuelezea Wakenya kwamba sikulichukua kutoka kwa Bw Kiplagat.

Vazi hilo lilikuwa spesheli na kulingana na utamaduni wa jamii ya Wakalenjin haturuhusiwi kufichua mengi kuhusiana na hafla kama hiyo na anayevikwa huenda nalo baada ya kutawazwa,” akasema BwSang alipokuwa akihutubia wanahabari mjini Eldama Ravine.

Mwenyekiti wa kikundi cha kitamaduni cha Eldama Ravine, Jona Tallam alidai kuwa yeye ndiye aliazima vazi la Mzee Kiplagat mwaka uliopita na hajawahi kumpa nmtu mwingine.

  • Tags

You can share this post!

Maafisa wa CDF wajuta kumeza hongo

Maafisa 117 watumwa kwa ofisi za ubalozi ugenini

adminleo