ODONGO: Msambweni yaonyesha mambo si shwari katika ODM
Na CECIL ODONGO
KUSHINDWA kwa ODM katika uchaguzi mdogo wa Msambweni ni ishara kuwa chama hicho kinaendelea kupoteza umaarufu katika ngome zake muhimu Pwani ikiwa kati yao.
Tukio hilo linajiri baada ya David Ochieng kumbwaga mwaniaji wa ODM Chris Karan mnamo Aprili mwaka jana kwenye kiny’ang’anyiro cha eneobunge la Ugenya.
Kabla ya uchaguzi wa Jumanne Msambweni, viongozi wa ODM walikuwa wamejipiga kifua kwamba chama hicho kingehifadhi kiti hicho.
Kinyume na matarajio ya wengi mwaniaji huru Feisal Bader alipata kura 15,251 dhidi ya 10,444 za mwaniaji wa ODM Omar Boga.
ODM imekuwa ikichukuliwa kuwa isiyo na demokrasia na yenye udikteta wa kulazimishia raia viongozi.
Ili kurejelea umaarufu wake jinsi ilivyokuwa mwaka wa 2007, kiongozi wa ODM Raila Odinga anafaa ahakikishe kuwa kuna demokrasia ndipo wawaniaji wasikimbilie vyama vingine au kuwania kama wagombea wa kujitegemea.
Haina umuhimu wowote kwa Bw Odinga kudai kuwa Bw Bader alikuwa na nia ya kuwania kiti cha eneo bunge hilo kupitia ODM ilhali Bw Boga ashabwagwa na kiti kimetwaliwa na mwaniaji huru.
Bw Odinga anafaa kujiuliza ni kwa nini Bw Bader hakutaka kushiriki mchujo wa ODM ambao ulimshirikisha tu Bw Boga na Nicholas Zani.
Je, ubaguzi na mapendeleo ambayo yamekuwa yakifanyika kwenye mchujo wa chama hicho ndiyo yanawahofisha wawaniaji dhidi ya kushiriki uteuzi?
Pili, ODM inafaa ikomeshe kiburi cha baadhi ya viongozi wake kujiona wafalme kuliko hata raia wanaopiga kura, eti kwa sababu wapo karibu sana na Bw Odinga.
Katika uchaguzi mdogo wa Msambweni, Gavana wa Mombasa Hassan Joho, Katibu Mkuu Edwin Sifuna na viongozi wa ODM waliomba kura kwa kiburi huku wakimkejeli Gavana Salim Mvurya ambaye ana ufuasi mkubwa eneo hilo na Naibu Rais Dkt William Ruto.
Japo siasa ni mchezo mchafu, hekima na unyenyekevu mara nyingine huwashawishi raia kukumbatia mwaniaji wako.
Ili ODM ijifufue, lazima bodi ya chama hicho chini Dkt Catherine Mumma ijitayarishe kuwatendea wanaotafuta tiketi ya ODM haki mnamo 2022.
Wafuasi wa ODM wanahofia kwamba kuna njama ya kuwapendelea washirika wa Bw Odinga wanaowania vyeo mbalimbali ilhali hata waliofanikiwa kuchaguliwa kutokana na sababu hiyo 2017 hawajafanya maendeleo ya maana.
Bw Odinga anafaa aepuke kuwaidhinisha wanaopokezwa tiketi ya chama jinsi alivyofanya katika kaunti ya Kisumu mapema mwaka huu kwa kumhakikishia Profesa Anyang’ Nyong’o tiketi ya chama 2022.