Michezo

Lucy Bronze atawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2020 kwa upande wa wanawake

December 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

BEKI Lucy Bronze wa Manchester City alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2020 kwa upande wa wanawake kwenye tuzo zilizotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Alhamisi kwa njia ya mtandaoni kutoka Zurich, Uswisi.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 ndiye mwanasoka wa kwanza raia wa Uingereza kuwahi kujinyanyulia taji hilo la Best Fifa Football Awards.

Bronze alimbwaga Pernille Harder wa Denmark na Wendie Renard kutoka Ufaransa.

Kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi, Sarina Wiegman, ambaye atamrithi Phil Neville na kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Uingereza kuanzia mwaka wa 2021, alitawazwa Kocha Bora wa Mwaka 2020 kwa upande wa wanawake.

Sarah Bouhaddi wa Olympique Lyon na timu ya taifa ya Ufaransa, alitawazwa Kipa Bora wa Mwaka.

Bronze aliyetawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka 2020 kwenye tuzo za BBC mnamo Machi 2020, aliwahi pia kuunga orodha ya wawaniaji wa taji la Mchezaji Bora wa Mwaka mnamo 2019. Mwaka huo, mshindi wa taji hilo alikuwa Megan Rapinoe wa Amerika aliyempiku mwenzake raia wa Amerika, Alex Morgan.

Bronze, 29, alinyanyua taji la Ligi Kuu, ubingwa wa League Cup na ubingwa wa UEFA katika msimu wa 2019-20 kabla ya kurejea Manchester City kunyanyua Kombe la FA mnamo Novemba mwaka huu.

Bronze na mwenzake Millie Bright katika timu ya taifa ya Uingereza waliunga orodha ya wachezaji 11 bora wa duniani mwaka huu wa 2020.

Wiegman, 51, alitawazwa Kocha Bora baada ya kuongoza Uholanzi kufuzu kwa fainali za Euro 2022 bila ya kupoteza mchuano wowote.