ONYANGO: Fedha za refarenda zitumiwe kuagiza chanjo ya corona
Na LEONARD ONYANGO
HUKU mataifa yaliyostawi kiuchumi duniani yaking’ang’ania chanjo ya virusi vya corona, humu nchini tunajadili namna tutakavyopata fedha za kuandaa kura ya maamuzi – kurekebisha Katiba – kuwezesha wanasiasa wanaokataliwa na wananchi katika uchaguzi mkuu wapate nyadhifa serikalini.
Tayari chanjo ya virusi vya corona imeanza kutolewa kwa maelfu ya watu nchini Amerika na Uingereza lakini bado haijulikani itafika lini humu nchini.
Kwa mujibu wa wizara ya Afya, Kenya imeagiza dozi milioni 24 za chanjo ya virusi vya corona ambayo inatarajiwa kupewa asilimia 20 ya Wakenya. Hiyo inamaanisha kuwa takribani Wakenya milioni 9.4 kati ya milioni 48, watapewa chanjo hiyo. Hatima ya asilimia 80 ya Wakenya waliosalia haijulikani kwani serikali haina fedha za kununua chanjo ambayo ni ghali.
Kenya imeagiza chanjo hiyo chini ya mpango wa shirika la Gavi ambapo mataifa maskini yatapewa chanjo nafuu itakayotolewa kwa asilimia 20 ya watu.
Katika mpango huo wa chanjo nafuu, nchi maskini, ikiwemo Kenya, italipia takribani Sh320 kwa kila dozi. Kenya imetumia Sh10 bilioni kuagiza chanjo hiyo.
Shirika la Gavi limeshirikiana na Benki ya Dunia, Wakfu wa Bill & Melinda Gates pamoja na wahisani wengineo kuhakikisha kuwa nchi maskini zinapata chanjo nafuu ili kulinda watu walio hatarini kama vile wahudumu wa afya, wazee na wanaougua maradhi hatari kama vile kisukari.
Wataalamu wamedokeza kuwa chanjo hiyo iliyoagizwa chini ya Gavi huenda ikawasili nchini Kenya pamoja na mataifa mengine ya Afrika, kati ya Januari na Februari 2021.
Maambukizi
Kenya inashikilia nafasi ya saba kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu ambao wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona barani Afrika.
Maelfu ya Wakenya wamepoteza kazi kutokana na janga la virusi vya corona. Uchumi umedorora. Bado kuna hofu kuhusu usalama wa wanafunzi na walimu shule zitakapofunguliwa Januari 4, 2021.
Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), karibu Sh15 bilioni zitahitajika kuiwezesha kukagua saini zinazounga mkono Mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) na kuandaa kura ya maamuzi ili kurekebisha Katiba. Mabilioni ya fedha pia yatatumiwa na wanasiasa wakati wa kampeni za kupigia debe mswada huo baada ya kuidhinishwa na mabunge ya kaunti.
Wanasiasa wanajali masilahi yao ya kibinafsi tu. Kuna uwezekano kwamba chanjo ya corona ikiwasili humu nchini wanasiasa pamoja na familia zao watakuwa wa kwanza kupewa na kuwaacha maskini kuendelea kuteseka.
Fedha hizo zaidi ya Sh15 bilioni zinazolenga kutumiwa kuendesha referenda zitumiwe kutafuta chanjo ya virusi vya corona.