Habari

Wafanyakazi wa kaunti kula Krismasi kavu

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

MWANGI MUIRURI, DAVID MUCHUI na GEORGE MUNENE

HUENDA wafanyakazi wa kaunti nchini wakasherehekea Sikukuu ya Krisimasi mikono mitupu, baada ya kutolipwa mishahara yao kwa muda wa miezi miwili.

Novemba, Baraza la Magavana (CoG) lililalamika kwamba Wizara ya Fedha haijatoa Sh78 bilioni ambazo serikali za kaunti zinafaa kupokea tangu mwezi Septemba.

Lilisema hali hiyo imefanya shughuli nyingi muhimu kukwama.

Katika Kaunti ya Murang’a, wafanyakazi wa serikali hiyo waliambiwa Jumatano kuwa kaunti haina fedha za kuwalipa mishahara ya miezi ya Novemba na Desemba.

Kwenye notisi iliyotoa kwa wafanyakazi hao, serikali ilitaja hali hiyo kuchangiwa na janga la virusi vya corona na serikali ya kitaifa kutozitumia kaunti pesa.

Hata hivyo, notisi ilisema serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha imewalipa wafanyakazi mishahara yao ya mwezi Novemba kabla ya Krisimasi.

“Hii ni hali ya kusikitisha sana kwetu. Limekuwa jambo gumu kupokea mishahara yetu kwa muda ufaao. Wakati mwingine tumecheleweshewa mishahara kwa hadi miezi minne. Hili ni sikitiko kuu ikizingatiwa baadhi yetu tunategemewa na familia zetu kukidhi mahitaji yao,” akasema kibarua mmoja.

Katika Kaunti ya Meru, Naibu Gavana Titus Ntuchiu, ambaye pia ndiye Waziri wa Fedha, alisema wameanza kushauriana na benki kuwapa mkopo ili kuwalipa wafanyakazi hao kabla ya Krisimasi.

Bw Ntuchiu alisema wanaidai serikali ya kitaifa karibu Sh2 bilioni kwa miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba.

Alisema benki huwa zinawatoza riba ya juu kila mara wanapochukua mikopo kutoka kwazo.

“Huwa tunatozwa riba ya kati ya asilimia mbili na asilimia 2.5. Katika utaratibu kama huo, huenda tukatozwa riba ya hadi Sh10 milioni kwa mkopo wa Sh400 milioni. Hiyo ndiyo sababu ambapo huwa tunaepuka kuchukua mikopo ya benki,” akasema.

Bw Ntuchiu alisema benki nyingi zinatahadhari sana kuipa mkopo kaunti hiyo.

Hata hivyo, alisema wanaendelea na mazungumzo kuhakikisha wafanyakazi wamelipwa kabla ya Krisimasi.

Alisema ucheleweshaji huo umechangia mikopo mingi muhimu kukwama, hali ambayo pia imefanya wanakandarasi wengi kudinda kuchukua miradi inayotangazwa na kaunti.

“Nimekuwa nikiandika barua nyingi kwa benki kuziomba kutouza mali ya wanakandarasi kwani tumewacheleweshea fedha zao. Hatuwezi kutekeleza mradi wowote kwa sasa ikiwa hatutapokea fedha za miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba,” akasema.

Wakati huo huo, wafanyakazi katika kaunti za Embu na Kirinyaga pia wamelalamika kuwa huenda wakasherehekea sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya bila chochote mifukoni mwao.

“Hatuna fedha. Hivyo, itakuwa vigumu kwetu kusherehekea Sikukuu ya Krisimasi. Je, ni vipi serikali inatarajia tusherehekee sikukuu hizo bila pesa?” akashangaa mfanyakazi mmoja katika Kaunti ya Kirinyaga.