Makala

OMAUYA: Diplomasia: Rais wa Somalia asichagulie Kenya marafiki

December 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MAUYA OMAUYA

KWENYE mahusiano kati ya mataifa hasa katika karne ya ishirini na moja, hakuna uwezekano wa kuchagua jirani wako.

Ndio maana mataifa huzingatia misingi thabiti ya diplomasia ili kujiepusha na karaha ya uhasama. Hata hivyo Somalia imezidisha uchokozi dhidi ya Kenya.

Historia ya mataifa ya Afrika haikuyapa fursa ya kuamua mipaka yao. Wakoloni walikongamana jijini Berlin mnamo mwaka wa 1884 chini ya chansela Oto Von Bismarck na ramani kuamuliwa. Ndio maana makabila mengi yalibwagwa kiholela bila mnato wa utaifa na kuchangia mizozo ya kikabila barani Afrika.

Makabila kadha ya Afrika yametawanyika na kutapakaa kote mipakani. Maasai, Oromo, Wasomali, Wateso, Waluo, wote wana ndugu zao katika taifa jirani. Hili wakati mwingi linaathiri mvuto wa uzalendo.

Hii ni tofauti mno na nchi za bara Uropa ambako mipaka ya nchi ilichukua misingi ya makabila yao baada ya vita vya miaka mingi, Ufaransa, Italia, Uingereza, Ujerumani, Latvia, Urusi… Hata vita vya majuzi katika maeneo ya Balkan vimesababisha mipaka thabiti katika misingi ya koo zao. Mataifa kama Kosovo, Czech, Slovakia, Albania yamezalishwa kutoka kwa vita vikali, hasa vya kikoo. Kumbuka taifa la Yugoslavia liliyeyuka kabisa.

Hatuwezi kuunda mipaka upya na taifa la Somalia kupitia mtutu wa bunduki. Vivyo hivyo haiwezekani kubadili mipaka na Tanzania au Uganda licha ya raia kuwa wa ukoo mmoja. Mipaka ya kudumu inahitaji vita vikali kama vile Sudan Kusini na Sudan, au Eritrea na Ethiopia. Vita vya aina hiyo vitakuwa maangamizi kwa Afrika. Lazima tuamue kusalia na mipaka ya wakoloni na tutafute mbinu tofauti ya kujenga utaifa wetu.

Wakati mmoja, hata dikteta Idi Amin aliwazia kupanua mpaka wa Kenya na Uganda hadi kufikia Naivasha. Somalia ilidai Kaskazini mashariki mwa Kenya.

Usumbufu wa Somalia wa sasa haufai hasa ukizingatia kwamba Mogadishu inategemea sana Nairobi kwa siasa zake na uthabiti wa vikosi vyake vya usalama hasa kupitia AMISOM.

Vitisho vya mara kwa mara, kufunga mpaka, kukatiza safari za ndege na kutimua mabalozi ni ishara kwamba Rais Abdullahi Farmaajo wa Somalia hajakoma vituko. Tayari mzozo wa mpaka wa maji ya Bahari Hindi umefikia mahakama ya kimataifa.

Somalia inalaumu Kenya kwa kuingilia masuala yake ya ndani. Ukweli ni kwamba Farmaajo hapendi uhusiano wa karibu kati ya Kenya na majimbo ya Jubaland na Somaliland.

Somaliland ni taifa thabiti ambalo limenawiri na kujitawala kwa utulivu na amani huku jirani Somalia ikizama kwa misukosuko. Mogadishu inapinga juhudi za Somaliland kutangaza uhuru wake. Kenya pia inaunga mkono wapiganaji wa Jubaland chini ya mbabe Sheikh Madobe ambaye pia anatawala eneo hilo kama Jimbo lililojitenga.

Kwa kushirikiana na Madobe, Kenya imefaulu kudhibiti mashambulizi ya kundi la Al Shabaab mipakani. Mogadishu ingali inapambana na Shabaab na ushirikiano wa Madobe utaendelea kuhitajika.

Yafaa Rais Uhuru atoe mwongozo wa kidiplomasia kuhusu Somalia bila kuathiri uhusiano na Jubaland au Somaliland. Farmaajo akome kuchagulia Kenya marafiki zake.

Katika msimamo huu, Kenya inatakiwa ichukue msimamo mkali ili Somalia ikome usumbufu. Mataifa haya yanategemeana kwa masuala kadhaa na ni kosa kubwa kwa wanasiasa wa Mogadishu kuvuruga maisha ya raia wa eneo hili.