Sam Allardyce aanza kazi ya ukocha kambini mwa West Brom kwa kichapo cha 3-0 kutoka kwa Aston Villa
Na MASHIRIKA
KOCHA Sam Allardyce alianza kibarua cha kudhibiti mikoba ya West Bromwich Albion kwa masaibu ya kikosi chake kupokezwa kichapo kikali cha 3-0 kutoka kwa Aston Villa mnamo Disemba 20, 2020.
West Brom almaarufu The Baggies walikamilisha mchuano huo na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya nahodha Jake Livermore kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea visivyo Jack Grealish katika dakika ya 36.
Refa Martin Atkinson alilazimika kurejelea mtambo wa teknolojia ya VAR kabla ya kumfurusha Livermore uwanjani.
Anwar El Ghazi aliwafungulia Villa ukurasa wa mabao katika dakika ya tano kwenye debi hiyo ya West Midlands.
Grealish alichangia bao la pili la Villa lililojazwa wavuni na Bertrand Traore katika dakika ya 84 kabla ya El Ghazi ambaye ni raia wa Misri kufunga penalti mwishoni mwa kipindi cha pili.
Wachezaji na maafisa wa benchi ya kiufundi wa West Brom walilalamikia hatua ya refa Atkinson kupuuza rai yao ya kupokezwa penalti mwishoni mwa kipindi cha kwanza licha ya Kortney Hause kumchezea visivyo kiungo Grady Diangana ndani ya kijisanduku.
Chini ya Allardyce, West Brom kwa sasa wanashikilia nafasi ya 19 jedwalini kwa alama saba, tano zaidi kuliko Sheffield United wanaovuta mkia.
Ilikuwa mechi ya kwanza kwa Allardyce, 66, kusimamia katika EPL tangu Mei 2018 alipoagana rasmi na Everton. Mkufunzi huyo aliteuliwa na West Brom kuwa kocha wao kwa mkataba wa miezi 18 ijayo mnamo Disemba 16 baada ya kutimuliwa kwa Slaven Bilic aliyefurushwa kwa sababu ya matokeo duni.
Kocha huyo amewahi pia kunoa vikosi vya Bolton Wanderers, Newcastle, Blackburn, West Ham na Sunderland.