• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 AM
UBWANYENYE: Mbinu wanazotumia mabilionea kujizolea utajiri

UBWANYENYE: Mbinu wanazotumia mabilionea kujizolea utajiri

Na FAUSTINE NGILA

UTAJIRI wa dunia unazidi kukua huku ubabe wa ubwanyenye ukishamiri katika uwekezaji kwa sekta mbalimbali za uchumi mwaka huu, kila mmoja akinoa mbinu zake za kurina hela. 

Katika orodha ya shirika la utafiti la Forbes ya walimwengu waliojizolea pesa kama njugu, tunapata mabilionea wa dola za kimarekani wapatao 2,208 kutoka mataifa 72, pakiwemo mabilionea wapya kutoka Zimbabwe na Hungary.

Anayeongoza kwa orodha hiyo iliyotayarishwa Machi mwaka huu ni mmiliki wa kampuni ya mauzo ya mtandaoni Amazon, Bw Jeff Bezos (pichani), hii ikiwa mara yake ya kwanza kuwapiku wenzake.

Bezos ameweka rekodi mpya kwa kuwa mtu wa kwanza duniani kuwa na utajiri uliozidi USD100 bilioni na kumwacha Bill Gates kwa umbali na USD39 bilioni.

Kwa jumla, wakwasi hawa wanaoetetemesha Dunia kifedha, wanamiliki jumla ya USD9.1 trilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 kutoka mwaka 2017.

Kwa wastani, kila bilionea anamiliki USD4.1 bilioni huku Amerika ikiongoza kwa idadi kubwa ya mabilionea miongoni mwa mataifa. Taifa hilo lina mabilionea 585, ikifuatwa na Uchina kwa 373.

Katika orodha hiyo, kuna mabilionea wapya 259 huku sekta ya sarafu za kidijitali, ambayo mwaka huu imejipigia debe mno,  ikipata mwakilishi kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, mabilionea 121 walitemwa kwa orodha ya mwaka huu baada ya mapato yao kudidimia na kushuka kwa ligi ya mamilionea wa dola za kimarekani. Wakija Kenya watakuwa mabilionea.

Katika orodha ya kumi bora kwa kutaja jina, utajiri wa 2018, miaka, kampuni/sekta na taifa wanakotoka, tunawapata:

 1. Jeff Bezos ($112b, 54, Amazon, Amerika), 

2. Bill Gates ($90b, 62, Microsoft, Amerika),

3. Warren Buffett ($84b, 87, Berkshire Hathaway, Amerika),

4. Bernard Arnault ($72b, 69, LVMH, Ufaransa), 

5. Mark Zuckerberg ($71b, 34, Facebook, Amerika) ,

6. Amancio Ortega ($70b, 82, Zara, Uhispania), 

7. Carlos Slim Helu($67.1b, 78, Mawasiliano, Mexico), 

8. Charles Koch ($60b, 82, Koch Industries, Amerika),

9. David Koch ($60b, 78, Koch Industries, Amerika) na 

10. Larry Ellison ($58.5b, 73, Kifauroro, Amerika).

Hapa barani Afrika kuna mabilionea wa Dola za Kimarekani wapatao 21 (wanawake wawili), lakini hakuna yeyote anayetoka Kenya kwa kuwa vigezo vya Forbes vya kuorodhesha havikubali utajiri unaomilikiwa na familia kama zile za Kenyatta, Moi na Chandaria.

Utajiri wa mabilionea wa Afrika pia ulipanuka kutoka USD70 bilioni hadi USD75.4 bilioni huku Aliko Dangote ($12b) wa Nigeria akiongoza kwa mwaka wa saba mfululizo.

Kati ya mabilionea wote 2,208, wanawake ni 256. Idadi hii iliongezeka na kufikia kiwango cha juu zaidi katika historia ya uorodheshaji huo.

Hata hivyo, hii ni asilimia 12 tu ya mabilionea wote kwa jumla. Fauka ya hili, wanawake wengi walipata utajiri wao kwa kuurithi. Ni wanawake 72 pekee waliong’ang’ana jino kwa ukucha kivyao na kujipata kwa orodha hiyo.

Wawili wao wameorodhesha katika 20 bora duniani. Hakuna aliyepambana kuingia 10 bora. Kwa sasa, Alice Walton wa Amerika, aliye nambari 16, ndiye mwanamke mkwasi zaidi duniani akiwa na mali ya thamani ya USD46 bilioni kutokana na faida ya kampuni ya Walmart.

Mbinu za ukwasi

Kuna mbinu kadha ambazo wadosi hawa walitumia kufika walipo sasa. Baadhi yao waliunda mashine za kipekee na kuziuza, wengine waliuza gauni za harusi kimataifa, baadhi wauza vyakula navinywaji huku wengine nao wakivumbua apu mpya za simu.

Ingawa kuna njia nyingi za kutajirika kiasi hiki, kuna mbinu chache ambazo zitampa mwekezaji uwezekano wa juu kuinuka kiuchumi na kufikia kiwango cha bilionea.

Mbinu ya kwanza ni kuwekeza katika ununuzi na uuzaji wa hisa na mali. Katika sekta hii ya fedha, kuliibuka mabilionea 310. Ni katika sekta hii ambapo utapata wawekezaji wa sarafu za dijitali kama Bitcoin.

Fasheni

Fasheni na bidhaa za rejareja ndiyo njia ya pili. Mabilionea 235 walijenga himaya zao za kidedha katika ulingo huu. Sita kati ya 20 bora walitoka kategoria hii.

Asilimia 10 ya mabwanyenye hao nao waliunda hela zao kutokana na ujenzi, ununuzi na uuzaji wa nyumba za makazi na biashara. Mabilionea 220 walifuata mkondo huu huku Uchina ikiongoza.

Sekta ya utengenezaji bidhaa inafuata. Wawekezaji 207 waliamini wakizidi kuboresha bidhaa zao kuwiana na matakwa ya wateja wao, wangeimarisha utajiri wao.

Teknolojia

Wapenzi wa teknolojia nao ni wa tano kwa uwezekano wa kuingia kwa orodha hii. Asimilia 9 ya mabwanyenye wote 2,208 waliimarisha ustadi wao wa dijitali, huku wanane wakiingia ndani ya 20 bora ulimwenguni.

Hapa ndipo utampata John Collison, aliyejizatiti na kuibuka bilionea wa umri wa chini zaidi, 27, kutinga orodha hiyo. Alivumbua mfumo wa malipo ya dijitali, Stripe unaotumika na idara za fedha kote duniani kuwalipa wafanyakazi.

Ingawa mbinu za kutajirika zinazidi kupanuka, asilimia 33 ya watu kwenye orodha ya Forbes walirithi ukwasi walio nao kutoka kwa watu wa familia.

Kwa wengine wote, kuna jambo moja ambalo walijua ingewafikisha mbali – kufanya jambo ulipendalo kuunda pesa. Iwapo unaanzisha biashara, mwanzo fikiria ndani ya moyo wako jambo unalolipenda zaidi.

Mapenzi ya unachofanya yatakunoa kuwazia jambao ambalo litakulipa kitia kizuri cha hela. Wote wanaamini kuwa kuajiriwa ni kuwa mateka wa kampuni huku ukizika uwezo wako mwenyewe wa kuanzisha kampuni na kuwaajiri mamia au hata maelfu ya watu.

You can share this post!

PROLACTINOMA: Ugonjwa wa kutoa maziwa kwa matiti...

Harmonize jikoni kuandaa kolabo ya kutisha akiwa na...

adminleo