Raila ajiandaa kustaafu siasa
Na CECIL ODONGO
KIONGOZI wa ODM, Raila Odinga Jumanne alifichua mpango wake wa kustaafu siasa akisema jukumu alilobakisha sasa ni kuunganisha Wakenya.
“Iwapo nitafanikiwa kuunganisha nchi hii kwa muda wa miaka michache ijayo ambapo kila Mkenya atajihisi nyumbani, na kabila lake litakuwa baraka wala si laana, sitakuwa na budi ila kustaafu,” akasema Bw Odinga alipomtembelea mfanyabiashara Chris Kirubi nyumbani kwake Nairobi.
Hii ni mara ya kwanza kwa kigogo huyo wa siasa za Kenya kutangaza mpango wake wa kustaafu siasa na ishara kuwa hatakuwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais 2022.
Tangu alipoafikia maelewano na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi, Bw Odinga ameonekana kujiepusha na masuala ya kisiasa. Badala yake amekuwa akijadili kuhusu kuunganishwa kwa taifa, kinyume na awali ambapo alikuwa mwiba kwa Serikali kwa kuikosoa katika kila hatua.
Kutulia kwake pia kumeonekana kuzima upinzani nchini huku waliokuwa nao katika NASA, Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka na Moses Wetang’ula wakionekana kushindwa kujaza nafasi yake.
Dkt Kirubi alichangamkia tangazo la Bw Odinga kupanga kustaafu na akampongeza kwa kuungana na Rais ili kufanikisha mpango huo. “Ni tangazo kubwa linalotolewa hapa kwangu.
Rais Kenyatta ana nguzo nne za maendeleo na mchango wako utakuwa muhimu katika utekelezaji wa nguzo hizo. Jambo zuri ni kuwaleta Wakenya wote pamoja,” Dkt Kirubi akamweleza Bw Odinga.
Alisisitiza kwamba wawekezaji watavutiwa nchini iwapo watahakikishiwa kwamba kila baada ya uchaguzi Wakenya wanakumbatia amani.
Bwanyenye huyo aliwaomba viongozi hao wawili wape kipaumbele utoaji huduma na wapuuze viongozi wanaolenga siasa za 2022. “Tuzungumzie rekodi nzuri ya uongozi badala ya siasa ya 2022.
Wewe ni mzalendo na nakuomba uendeleze na ubuni nchi ambayo kizazi kijacho kitakukumbuka na kiseme kwa kweli tulikuwa na kiongozi shupavu,” akaongeza Dkt Kirubi.
Bw Odinga alikuwa ameandamana na wakili Paul Mwangi, ambaye ni moja wa wenyekiti wa kamati ya pamoja iliyobuniwa na Rais na Bw Odinga kwa lengo la kuwaunganisha Wakenya.
Miongoni mwa mambo wanaolenga kutekeleza katika muafaka wao ni pamoja na kuunda sera za maadili ya kitaifa, kuleta usawa, kumaliza uchaguzi unaogawanya Wakenya pamoja na kukomeshwa ufisadi.
Bw Odinga ambaye alikuwa mkosoaji mkuu wa serikali ameonyesha dalili za kustaafu ulingo wa kisiasa kwa kuyakumbatia majukumu mapya ya kuwa balozi maalum wa amani barani Afrika.
Wiki iliyopita, Bw Odinga alitua nchini Sudan Kusini kama balozi wa amani aliyewakilisha serikali ya Kenya na Muungano wa Afrika ambapo aliandaa mkutano na Rais Salva Kirr katika juhudi za kuleta amani na kumpatanisha na aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar.
Bw Odinga pia anatarajiwa kukutana na Bw Machar nchini Afrika Kusini alikoenda uhamishoni.
Kando na hayo kiongozi huyo wa chama cha ODM ambaye zamani alikuwa mwiba katika kukemea sakata za ufisadi ametuliza makali yake ya kushutuma serikali kuhusiana na sakata zinazoendelea kuripotiwa serikalini.