Tusker mbioni kunasa vipaji sokoni kuimarisha kikosi
Na CECIL ODONGO
MABINGWA mara 11 wa ligi kuu nchini KPL, Tusker FC wamejitosa sokoni mapema na kutwaa huduma za mshambulizi wa Bidco United David Juma.
Habari za kutwaliwa kwa huduma za fowadi huyo zilitangazwa katika mtandao wa klabu na Afisa mkuu mtendaji wa Tusker Charles Obiny.
“Tuna furaha kwamba tumeweza kumsaini David Juma kutoka Bidco United FC. Tuna wingu la matumaini kwamba atatufaa pakubwa katika safu ya ushambulizi. Kocha wetu anatambua ucheaji wake na pia alifanya kazi naye akiwa mkufunzi wa klabu hiyo,” ikasema taarifa ya Bw Obiny katika mtandao wa klabu.
Juma mwenye umri wa miaka 25 anatarajiwa kucheza mechi yake ya kwanza kwa mabingwa hao wa zamani Jumatatu katika pambano dhidi ya Posta Rangers uwanjani Camp Toyoyo.
Hata hivyo kocha wa Tusker Robert Matano alisema kwamba kusajiliwa kwa mchezaji huyo ni mwanzo tu wa sajili nyingi zinazotarajiwa kufanywa na klabu hiyo msimu huu wa kuingia sokoni kununua na kuwauza wachezaji.
“Bado tunatarajia kufanya usajili ili kuimarisha idara za timu zinazoonekana legevu. Tutamaliza usajili wetu juma hili na tunashukuru uongozi wa klabu kwa kutusapoti,” akasema Matano.
Tusker FC tayari wamewaachilia wachezaji wake wanne akiwemo kipa wao David Okello.
Waundamvinyo hao wanaonekana kulemewa mno msimu huu na walimtema aliyekuwa kocha wao Sam Ssimbwa kutokana na misururu ya matokeo mabaya ndipo Matano akakabidhiwa usukani.
Katika msimamo wa jedwali la ligi, Tusker FC wanakalia nafasi ya 11 baada ya kupata alama 23 katika mechi 19 walizowajibikia kwenye mkondo wa kwanza wa ligi.