• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 1:14 PM
PAMBO: Yaliyopita yasiwe ndwele kwako

PAMBO: Yaliyopita yasiwe ndwele kwako

Na Benson Matheka

WATU wakiachwa na wachumba wao au wakipata talaka huanza maisha mapya ya mapenzi. Wataalamu wanasema watu hao huwa na kipindi kigumu sana baada ya kuachwa na kabla ya kupata wachumba wapya.

Wanasema kuachwa na mpenzi au kupata talaka kunasononesha sana hata kwa wale ambao hupeana talaka wenyewe. “Haijalishi ni nani anayeacha mwenzake, anayeachwa au sababu ya kuachana.

Ukweli ni kwamba talaka na kuachwa na mchumba humuathiri mtu na maisha yake kwa jumla,” aeleza mwanasaikolojia Bela Gadhi kwenye makala yaliyochapishwa kwenye jarida la mtandaoni, Psychology Today.

Kulingana na mtaalamu huyu wanaojipata katika hali hii huogopa kujihusisha na mapenzi tena. “Japo inategemea sababu na mazingira ya kuachana, watu wengi huchelea kuanza maisha mapya ya mapenzi. Hata hivyo, kuna mbinu na hatua za kufuata ili kuhakikisha mtu amefurahia maisha,” aeleza.

Anasema watu wengi huwa wanaalika masononeko kwa kunyamaza na kujitenga na watu wengine bila kufahamu kwamba kuzungumzia masaibu yao ni tiba.

“Badala ya kunyamaza na kusononeka peke yako, mtafute mtu unayemwamini umfungulie moyo wako. Anaweza kuwa jamaa yako wa karibu, rafiki yako au pasta wako. Hakikisha kwamba unayemfungulia moyo wako ni mtu ambaye hatatumia masaibu yako kukuvunja moyo zaidi au kukutumia vibaya,” aeleza Bi Gadhi.

Kulingana na Julia Makena wa shirika la Big Hearts jijini Nairobi, mtu anafaa kutafuta msaada kutoka kwa washauri nasaha waliohitimu.

Anasema kwa kuogopa upweke, watu wengi huwa wanaangukia mitego ya walaghai wa mapenzi kwa kusaka wapenzi wapya kwa pupa.

“Mtu anafaa kuchukua muda kabla ya kuanza uhusiano mpya wa mapenzi. Kuchukua muda kutakusaidia kuelewa kilichovuruga uhusiano wako wa kwanza. Muda huo unakufanya utulie na kufanya maamuzi yanayofaa,” aeleza.

Kulingana na Bi Gadhi, ni makosa kujitosa katika uhusiano mpya wa mapenzi kwa sababu ya hasira ya kutemwa na wachumba wao. “Kwa kawaida hasira ni hasara na itakuongezea mateso zaidi moyoni.

Kuna wanaojibwaga katika uhusiano mpya wakidai wanataka kulipiza kisasi kwa kuachwa na wachumba wao. Kuingia katika uhusiano wa mapenzi kwa sababu ya hasira au kulipiza kisasi ni hatari mno,” aeleza.

Wataalamu wanasema watu wengi hufanya makosa kwa kuanza uhusiano mpya ili kujituliza badala ya kufanya lililo sahihi kuponya roho zao baada ya kupigwa teke na wachumba wao.

“Acha yaliyopita yasiwe ndwele kwako. Tulia ili usijipate mikononi mwa watu wabaya tena kwa sababu ya kufanya uamuzi usiofaa. Kilicho muhimu sio kuondoa upweke, ni kupata mtu ambaye atakupa maisha ya raha. Lakini kumbuka maisha ya raha huanza na mtu binafsi,” aeleza Bi Gadhi.

“Huwa ninakumbusha watu kuwa kuanza uhusiano wa mapenzi baada ya talaka sio rahisi na mtu huwa anahitaji watu kumtia motisha na kumchochea kurejelea maisha ya mapenzi. Hata hivyo, huwa inategemea watu ambao mtu huamua kuwa karibu nao,” anaeleza.

Kulingana na Bi Makena, mtu akiachwa hafai kufananisha watu wengine na mpenzi wake wa zamani. “Tarajia kwamba mpenzi wako mpya atakuwa tofauti na aliyekutema.

Usifananishe vipusa wote na mkeo wa zamani au wanaume wote na mumeo aliyekutaliki. Muhimu ni kuvutiwa na tabia ya mtu. Hiki ndicho kigezo muhimu kwa uhusiano wa mapenzi wa muda mrefu,” aeleza Bi Makena.

Watalaamu wanashauri watu wanaosaka wapenzi wapya baada ya kupata talaka kutopeana mili yao kwa uroda kwa wapenzi wapya haraka. Kulingana na Bi Gadhi, kufanya hivi kunaweza kufifisha uhusiano na kuongezea mtu masononeko.

Hata hivyo, anasema hii haifai kuwa sababu ya kujinyima raha ya uroda akipata mtu mwaminifu, mradi awe mwangalifu akilishana asali.

You can share this post!

Kakangu huenda kwa mganga akitaka kuniangamiza, polo aambia...

FUNGUKA: Sihitaji urembo kunyaka wahadhiri chuoni na...

adminleo