ADUNGO: Liverpool ndio madume EPL msimu huu, Guardiola, Mou, Emery wajipange
Na CHRIS ADUNGO
INGAWA Manchester City na Arsenal wanapigiwa upatu wa kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika kampeni za msimu ujao wa 2018-19, nahisi kwamba kikosi cha pekee chenye uwezo wa kuvuruga matumaini ya miamba hao ni Liverpool.
Baada ya kutinga fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu uliopita na kuwalaza Man-City 2-1 na Man United 4-1 katika michuano ya kirafiki iliyowakutanisha nchini Amerika majuzi, Liverpool ni mpinzani ambaye kwa sasa amedhihirisha kuwa ana uwezo mkubwa usiostahili kupuuzwa.
Kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kwa sasa ni timu tofauti kabisa. Chini ya mkufunzi huyu wa zamani wa Borussia Dortmund, viwango vya wachezaji wengi wa Liverpool vimeimarika.
Hili limedhihirishwa kupitia kwa ukali wa nyota Sadio Mane, Alex Oxlade-Chamberlain, Roberto Firmino na Mohamed Salah ambaye aliibuka Mfungaji Bora wa EPL msimu uliopita na hivyo kutia kibindoni ‘kiatu cha dhahabu’.
Hadi kufikia mwisho wa msimu uliopita katika EPL, Liverpool na Manchester United ndizo timu za pekee ambazo ziliishinda Man-City ligini. Silaha kubwa ya Liverpool ni uwezo wao wa kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza kupitia kwa wachezaji wao wenye kasi sana na ambao hawahitaji nafasi nyingi ili kufunga mabao.
Huu ndio upekee wa kikosi cha Klopp. Kwa namna moja au nyingine, Liverpool ni timu ambayo ubora wake utadhihirika kila inapocheza na mpinzani aliye na mazoea ya kumiliki mpira kwa muda mrefu na ambaye anacheza soka ya kushambulia kama mabingwa washikilizi wa taji la EPL, Man-City.
Mnamo 2013, Klopp aliwachochea Dortmund kutinga fainali ya UEFA baada ya kuwabandua Real Madrid kwenye nusu-fainali. Ingawa kulikuwapo na klabu nyingi zenye vikosi bora zaidi kuliko Dortmund wakati huo, mfumo na upekee wa mbinu za ukufunzi wa Klopp uliwatambisha wapambe hao wa soka ya Ujerumani.
Man-City na Arsenal kwa sasa wana vikosi bora zaidi kuliko Liverpool. Hata hivyo, iwapo kuna timu iliyo na nafasi kubwa sana ya kusambaratisha kabisa ndoto za Man-City ya kocha Pep Guardiola na Arsenal ya mkufunzi Unai Emery katika jitihada za kuwania ubingwa wa EPL msimu ujao, basi ni Liverpool inayonolewa na Klopp!
Hadi kufikia sasa, hakuna kitu kizuri zaidi kuliko kuwa shabiki wa Liverpool. Hadi msimu mpya utakapoanza, Klopp atakuwa amefanikiwa kuwafanya wachezaji wake kuoanisha mitindo yao na kuelewa kabisa uwanjani.
Usajili ambao Klopp tayari ameufanya muhula huu ni ishara ya ukubwa wa kiu aliyonayo ya kutia kibindoni ufalme wa EPL na taji la UEFA. Japo matumizi yake ya fedha yameshtumiwa na mahasimu wake wakuu katika EPL, naona kwamba Klopp amepania kujenga kikosi thabiti kitakachohimili mawimbi yaushindani katika EPL na UEFA.
Baada ya kujinasia huduma za viungo Naby Keita na Fabinho, Klopp alimsajili fowadi Xherdan Shaqiri kabla ya kujitwalia maarifa ya kipa Alisson Becker ambaye ni mzawa wa Brazil.
Mbali na Man-City na Arsenal, sioni mpinzani yeyote mwingine wa Liverpool msimu ujao. Baada ya kumsajili kiungo Jorginho kutoka Napoli, Chelsea ambao wanaanza kuzoea maisha chini ya kocha mpya Maurizio Sarri, wamepotezewa dira na hatua ya Real kuanza kuwahemea nyota Eden Hazard, Willian na kipa Thibaut Courtois.
Chini ya Emery aliyemrithi Arsene Wenger uwanjani Emirates, Arsenal wanazidi pia kujiimarisha. Kikosi hicho tayari kimejinasia huduma za Stephan Lichtsteiner, Lucas Torreira, Bernd Leno, Sokratis Papastathopoulos na Matteo Guendouz.
Nikitarajia Tottenham kufunga orodha ya nne-bora mwishoni mwa kampeni za EPL mnamo 2018-19, nahisi kwamba changamoto ambazo kwa sasa zinawakabili Man-United na Chelsea zitawaponza hatimaye.
Badala ya kujishughulisha sokoni kama Klopp anavyofanya, Jose Mourinho wa Man-United bado analumbana na wachezaji Paul Pogba, Eric Bailly na Anthony Martial ambao huenda wakashawishika kuugura uwanja wa Old Trafford. Man-United kwa sasa wanahitaji winga mmoja, beki wa kati na mvamizi atakayesaidiana na Romelu Lukaku kuwateketeza mahasimu.