ULIMBWENDE: Mbinu 8 bora za kulainisha ngozi
Na MAGGY MAINA
BILA shaka mtu aliye na akili razini huhitaji ngozi laini na nyororo ili kujipa ujasiri wa kukabiliana na changamoto za kila siku pale kazini au nyumbani.
Hata hivyo, mbinu au njia tunazotumia wakati mwingine hutuacha na matokeo tusiyoyatarajia. Ni kwa sababu tumeumbwa sote tofauti na tunadhani kuwa kwa kutumia njia iliyomletea mwenzetu matokeo bora itatusaidia, lakini matokeo huwa kinyume kabisa.
Hizi hapa njia nane za kufuata ambazo zitakusaidia; haijalishi ni aina gani ya ngozi ulio nayo.
- Mlo
Vitu unavyokula vina mchango mkubwa katika ngozi na afya yako kwa ujumla. Ili kupata ngozi nzuri iliyo laini, nyororo na inayong’aa inabidi uache vyakula na vinywaji vinavyotengenezwa viwandani, wanga, mafuta na sukari na badala yake kula protini, matunda, mboga na kunywa maji kwa wingi.
Hakikisha unakunywa maji si chini ya glasi nane kwa siku na matunda pamoja na mboga kila unapopata mlo.
Matunda na mboga za matawi husaidia oksijeni kuzunguka vizuri mwilini na kwenye ngozi kuliko mafuta au kipodozi chochote unachoweza kupaka.
Protini husaidia kujenga ulinzi zaidi katika seli za ngozi ambayo ngozi inahitaji kukabiliana na ukavu wa ngozi. Nayo maji husaidia mzunguko mzuri wa damu mwilini na kusaidia vinyweleo kupumua vizuri, hivyo kuzuia bakteria chini ya ngozi.
- Muda wa kupumzika
Watu wengi hawatambui umuhimu wa usingizi katika kutunza ngozi na kuzuia kuzeeka haraka. Usingizi ni muhimu kwa ngozi yako sana, hakikisha unapata muda wa kutosha kulala usiopungua masaa 8. Kifiziolojia, ngozi inafanya kazi kubwa sana wakati wa mchana katika kutunza mwili, kukabiliana na mionzi ya jua, kukabiliana na vijidudu mbalimbali kama bacteria na virusi na kutizamia joto la mwili. Ngozi hujijenga wakati mwili umepumzika ili kuweza kuendelea kuchunga mwili wa mwanadamu ipasavyo.
- Acha kujichubua
Kutumbua chunusi na vipele ni tabia tulio nayo sisi wanadamu. Mara nyingi matokeo yake huwa ni kuwa na makovu na wekundu. Kufanya hivi pia huchangia bakteria kusambaa na kuharibu ngozi hata katika maeneo ambayo hayakuwa na matatizo.
Japokuwa ni ngumu kutotumbua chunusi, ni vyema ikiwa italazimu ufanye hivyo, tumia kitambaa safi kutoa chunusi na wala sio vidole au kucha kwa sababu ya uchafu uliopo kwenye kucha na vidole. Yaani hatuwezi kuamini mikono yetu kwa asilimia 100.
Ukiwa na chunusi unashauriwa kumuona mtaalamu wa afya ya ngozi ili akupe tiba ya uhakika.
- Usafi kwanza
Osha uso wako. Watu wengi hukimbilia kuosha nyuso zao harakaharaka na sio vizuri kusafisha uso juujuu kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa uchafu kubaki, hasa wanawake ambao wanatakiwa kutambua umuhimu wa nyuso zao. Basi ni bora ukatenga muda wa kutosha katika kuosha na kutunza uso.
Kusafisha uso mara zisizopungua mbili kwa siku ni vizuri kwa utunzaji wa ngozi yako ya uso.
Baada ya kufanya hivyo ni muhimu upake mafuta kiasi. Mafuta ni kwa ajili ya kulainisha na kung’arisha ngozi. Hata ijapokuwa una ngozi ya mafuta mengi, ni vizuri kutafuta mafuta ya ngozi yako (oily skin).
- Tunza vizuri macho yako
Watu wengi hupaka kiasi kidogo cha mafuta chini ya macho bila kujua faida tunazoziacha kwa kutokufanya hivyo.Kuna mistari (mikunjo) ambayo inaanzia kwenye jicho na ambayo muda mwingine husogea hadi kwenye maeneo ya karibu na nywele. Paka mafuta ya kutosha chini ya macho. Aidha, fanya ni kama unajimasaji kuanzia kwenye kona karibu na pua mpaka kwenye mfupa wa shavuni (cheekbone) kuzunguka jicho lote.
- Barafu
Barafu ni moja kati ya vitu muhimu katika kutunza ngozi. Licha ya upatikanaji rahisi pia ina uwezo wa kutunza ngozi yako bila gharama.
Faida za kutumia barafu katika utunzaji wa ngozi yako ni kwamba; Ukiumia au kujichuna kwenye ngozi waweza kutumia barafu kupunguza wekundu na kupunguza mwasho katika eneo lile.
Sote tunajua unapochubuka au kuumia kuna mwasho ambao tunahisi katika eneo lile la jeraha. Ukitumia barafu itakusaidia. Pia barafu unaweza ukaitumia kupunguza ukubwa wa matundu katika ngozi hasa pale mtu alikuwa amekamua chunusi.
Barafu husaidia kuvuta ngozi ilisiwe imeacha matundu ambayo muda mwingine hayapendezi kuonekana. Ila kumbuka wakati wa kutumia barafu zungusha maeneo tofauti kwasababu huunguza pale inapoachwa sehemu moja. Pia ni vizuri kuweka aloevera katika maji utakayo gandisha kwa ajili ya barafu (hiari yako).
- Tumia mafuta yanayofaa ngozi yako
Moja kati ya njia za kutapa ngozi laini na nyororo ni kutumia mafuta ambayo yametengenezwa kwaajili ya kupaka kwenye ngozi na sio ya nywele au ya kupikia.
Kutumia mafuta ya ngozi husaidia kung’arisha ngozi na muonekano mzuri ambao sio wa mafuta. Mafuta ya ngozi hayazibi vinyweleo vya ngozi, hivyo huruhusu ngozi kupumua na kutoa taka mwili kupitia vitundu hivyo na yanasaidia kupunguza uzajishaji wa mafuta katika uso hasa kwa wale wenye ngozi za mafuta.
Kumbuka kupaka mafuta mara mbili kwa siku katika uso safi; yaani baada ya kusafisha uso vizuri ndipo unashauriwa upake mafuta. Ukizingatia hilo utaona mabadiliko katika ngozi yako.
- Sunscreen
Kwa wale wenye matatizo ya kuungua wakiwa kwenye jua asubuhi, ni muhimu wawe wakipaka mafuta ya kuzuia mionzi ya jua (sunscreen) inayopenya kwenye ngozi na kuharibu ngozi yako. Na pale unapokuwa nje, hakikisha unajizuia na jua kwanzia mavazi yako; vaa miwani ya kuzuia miale mikali ya jua na kofia pana inayozuia jua kupiga usoni.