HabariSiasa

Orodha ya viongozi vinyonga Kenya

July 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

WANASIASA wa Kenya huwa vigumu kutabirika kutokana na tabia yao ya kubadili misimamo mara kwa mara kulingana na jinsi mazingara ya kisiasa yanavyowafaa.

Hili limedhirika katika matukio ya majuzi, ambapo wanasiasa waliokuwa wakijionyesha mbele ya Wakenya kuwa maadui ambao hawawezi kuketi meza moja, sasa wanaimba wimbo mmoja.

Tabia hii inazua masuala ya iwapo kweli wanasiasa wa Kenya wana misimamo ya kisiasa na kimawazo ama wanabadilika kulingana na kile wanachoona ni muhimu kwao binafsi.

Katika siku za majuzi, waliokuwa wameapa kuwa hawatawahi kushirikiana, sasa wamebadilisha nia ili kuokoa maisha yao ya kisiasa.

1. Raila Odinga

Tangu uchaguzi mkuu wa 2013, Raila Odinga na Rais Uhuru walikuwa wakirushiana lawama na kukosoana vikali. Uhasama wao wa kisiasa ulionekana kufikia kilele mwaka jana Bw Odinga alipokosa kumtambua Uhuru kama rais na akajiapisha Januari mwaka huu.

“Siwezi kushirikiana na wezi,” Bw Odinga alinukuliwa akisema kwenye mikutano mingi ya hadhara.

Lakini Machi 19, aligeuza msimamo na kumtambua Uhuru Kenyatta kama Rais na sawa wawili hao wanashirikiana katika kile wanachosema ni kuleta umoja wa kitaifa, kupiga vita ufisadi na kufanikisha Ajenda Nne Kuu za maendeleo.

2. Kalonzo Musyoka

Mwaka jana, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alitangaza kuwa hangeshirikiana kwa vyovyote na Serikali ya Jubilee.

“Wanataka nijiunge na Jubilee lakini hakuna kitakachonifanya nibadilishe nia na kushirikiana nao. Mimi siwezi kuhongwa na hakuna vitisho vitakavyonifanya kubadilisha nia. Siwezi kusaliti msimamo wangu kwa kushirikiana na serikali isiyoheshimu haki za watu na inayoamini katika hongo na vitisho kubakia mamlakani,” alisema Bw Kalonzo akihutubia baraza kuu la chama chake kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Kauli hii ni tofauti na msimamo aliotoa Jumamosi alipoongoza baraza kuu la chama kutangaza Wiper kitaunga mkono serikali: “Sasa ni uamuzi wa baraza kuu la chama cha Wiper kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta katika juhudi zake za kubadilisha Kenya. Wabunge wetu wataongozwa na uamuzi huu,” Bw Musyoka alitangaza.

3. Aden Duale

Kiongozi wa wengi katika bunge Aden Duale ni mmoja wa viongozi wa Jubilee waliomkosoa vikali kiongozi wa ODM, Raila Odinga mwaka jana.

Baada ya muafaka wa Bw Odinga na Rais Kenyatta, Bw Duale alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza kumsifu waziri huyo mkuu wa zamani akimtaja kama mwanasiasa mtajika.

“Raila Odinga ni nembo, mwanasiasa mtajika ambaye ana sifa za kulinda,” alisema Bw Duale.

4. Gavana Hassan Joho

Kwenye kampeni za mwaka jana, Gavana Hassan Joho wa Mombasa, ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha ODM, hangeonana ana kwa ana na Rais Kenyatta.

“Mimi ni adui nambari moja wa Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto. Jubilee imeshindwa kutuongoza na hatutawapa nafasi ya kuendelea kuwa mamlakani,” alisema Bw Joho katika bustani ya Uhuru Park mwaka jana.

Baada ya muafaka wa Bw Odinga na Rais Kenyatta, Bw Joho amekuwa mstari wa mbele kuuchangamkia na hata kuzika tofauti zake na waziri Najib Balala ambaye mwaka jana alisema sio wa hadhi yake kisiasa.

“Tutashirikiana nawe, tutashirikiana na serikali yako kuimarisha maisha ya watu wa Mombasa na Kenya. Awali, tulikuwa tukishambuliana kwa maneno. Lakini sasa tunataka kuzungumza ili tupate suluhu ya matatizo yetu,” alisema Bw Joho alipomkaribisha Rais mjini Mombasa mnamo Juni mwaka huu.

5. Moses Wetang’ula

“Bw Ruto ni mtu anayejifanya, asiye na huruma na ni kinaya kwake kufunza NASA na Wakenya maadili mema. Tunashauri Wakenya kuchukulia Ruto kimzaha,” Bw Wetangula alisema mapema mwaka huu.

Hali ilikuwa tofauti alipohojiwa juzi na kusema atashirikiana na wanasiasa wote akiwemo Bw Ruto.

6. Ababu Namwamba

Mnamo 2013, Namwamba alitangaza uaminifu wake kwa Raila Odinga lakini mwaka jana alijiunga na Jubilee.

Mwingine aliyekuwa na msimamo mkali ila akabadilika baadaye ni aliyekuwa Seneta wa Mombasa, Hassan Omar