Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Jumuiya ya Waswahili inaomboleza majohari adhimu wa Kiswahili

August 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PROF KEN WALIBORA

JUMAPILI imeanza kwangu kwa kupokea tanzia ya Prof Mwenda Mukuthuria (pichani), mwanataaluma wa Kiswahili aliyejitolea sabili kuisukuma mbele taaluma hii.

Punde si punde majukwaa ya mtandaoni yamemiminikiwa risala za rambirambi kwa kuondokewa na mwenzetu katika tasnia ya Kiswahili. Ni masikitiko makubwa kwa kweli.

Nitamkumbuka Mwalimu Mukuthuria kwa idili yake katika shughuli za Chama cha Kiswahili cha Taifa (Chakita). Sanduku langu la baruapepe limesheheni zake baruapepe tele za kusambaza habari za Chakita.

Aidha akisambaza taarifa zozote zenye kuwapa wengine fursa za kujikuza kitaalamu, si makongomano yasiyo ya Chakita, si nafasi za ajira. Kama kuna sifa moja kubwa aliyokuwa nayo ni kutojifikiria yeye peke yake, kuwafikiria wengine.

Alikuwa, kama marehemu Peter Mugambi na Paul Musau wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, miongoni mwa wasomi waliowahi kunialika kusema na wanafunzi wao vyuoni.

Kama nilivyowahi kusema hivi karibuni, Mugambi na Musau walinialika KU. Kwa upande wake, Mwalimu Mukuthuria alinialika alipokuwa anafundisha bewa kuu la Chuo Kikuu cha Mount Kenya, mjini Thika. Wanafunzi wake wa mikondo anuwai ya masomo walioujaza ukumbi tele nikatangamana nao katika hafla ambayo isingekuwapo bila ukarimu wake mwalimu huyu.

Mara ya mwisho kusema naye ni mapema mwaka huu barabara kati ya Narok na Mai Mahiu ilipoziba kutokana na maporomoko ya ardhi. Prof Mukuthuria alinieleza kwa mapana na marefu vile alivyonaswa katika mtafaruku wa usafiri maana alikuwa safirini kutoka Chuo Kikuu cha Maasai Mara alikofanya kazi ya uamidi (dean) kuelekea Nairobi.

Kwa kweli alinisimulia kisa hicho kwa muda mrefu, kiasi cha dakika ishirini au nusu saa hivi. Kamwe sikujua kwamba hii ingekuwa mara ya mwisho kusema naye.

Jumuiya ya “Waswahili” inaombeleza kuondokewa na mwenzao. Tunaiombea faraja aila ya Prof Mwenda Mukuthuria katika kipindi hiki cha majonzi makubwa. Poleni sana kwa kupatwa na msiba huu.

Ila mara hii mikuroro ya misiba haishi. Hivi punde nimesikia pia kwamba Mwalimu Kamunde wa Chuo Kikuu cha Kenyatta naye ameenda njia ya marahaba. Msimu wa misiba huu. Sina budi kuwapa pole wote wanaohusika na msiba huu.

Misiba hii inaikumba jumuiya ya “Waswahili” inatukumbusha sisi wanadamu jinsi tulivyo dhaifu. Nimetazama kauli za rambirambi wanazotoa Waswahili kutoka ndani na nje ya nchi na kuhisi kwamba tu wamoja—abiria katika dau moja. Nimeona risala za rambirambi kutoka Namibia, Tanzania, Marekani na kwengineko zikiwataja kwa wema wenzetu waliotuacha mkono.

Isitoshe, nimeona miito ikitolewa kuchangisha hela na kuzipitishia kwa wafawidhi mahususi ili kutoa pole kwa familia husika. Mimi hili nalifasiri kama ishara ya mshikamano mwafaka baina ya wadau wa Kiswahili.

Ila sharti tukiri kwamba vilevile huwa tuna tofauti zetu na husuda zetu ambazo inabidi kuzizika katika kaburi la sahau na kukakania kuimarisha zaidi ushirikiano na udugu katika karaha na raha, na uhai na kifo.