• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:20 PM
Baada ya kuilambisha sakafu Gor, Bandari sasa wasema ligi ni yao

Baada ya kuilambisha sakafu Gor, Bandari sasa wasema ligi ni yao

NA CECIL ODONGO

KOCHA wa Bandari FC  Bernard Mwalala anaamini kwamba timu hiyo inaweza kutwaa ubingwa wa KPL msimu huu baada ya kuwalisha kichapo mabingwa mara 16 Gor Mahia Jumanne Agosti 7, 2018.

Akizungumza baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Gor, mkufunzi huyo wa zamani wa Nzoia Sugar FC alieleza matumaini makubwa kwamba watafikia K’Ogalo ambao wanawazidi kwa alama 11 uongozini.

“Hakuna timu ambayo imetwaa ubingwa wa KPL tayari. Ninaamini miujiza  na nafahamu kwamba sisi bado ni wagombezi halisi wa ligi. Tuna uwezo wa kushinda ubingwa huo Gor wakizidi kuteleza nasi tushinde,” akasema Mwalala baada ya mechi hiyo.

Aidha Mkufunzi huyo alifichua kwamba hawakuangazia rekodi ya Gor Mahia ya kutoshindwa kabla ya mechi  na hiyo iliwapa ujasiri wa kutwaa ushindi.

“Hatukushughulishwa na rekodi yao ya kutoshindwa, tulishiriki mechi hiyo tukilenga ushindi jinsi tunavofanya katika mechi nyingine. Nafurahi sana mbinu zetu zilifanya kazi,” akaongeza Mwalala.

Bandari hawajapoteza mechi yoyote tangu Bernard Mwalala apokezwe usukani wa kuinoa na tayari amewaongoza katika mechi tano za ligi.

Timu hiyo kutoka Pwani watakutana na Tusker FC ugenini Jumapili Agosti 12 katika uwanja wa Ruaraka wakilenga kupunguza uongozi wa Gor ligini.

Kwa sasa Bandari wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 45 baada ya kujibwaga uwanjani mara 26 huku Gor Mahia wakiwa kileleni kwa alama 56 baada ya kusakata mechi 23.

You can share this post!

Kocha wa timu ya taifa U-17 asema kikosi kitatinga fainali

Kadi nyekundu zatema wachezaji 4 nje ya KPL

adminleo