Habari

Njama ya wanafunzi waliofeli KCSE kujipea 'A' yaanikwa

August 8th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

Wazazi wametahadharishwa kuhusu tabia mpya miongoni mwa wanafunzi, haswa wa shule za upili, ya kubadili alama kwenye matokeo ya mitihani ambapo wanajiongezea ili kuwahadaa wazazi wao kuwa wamefuzu.

Hivyo basi, mzazi anapasa kuwa makini anapopewa matokeo ya mitihani na mwanaye, kwa kuwa uwezekano kuwa alama zimebadilishwa uko juu.

Muhula huu, visa vingi vimeripotiwa vya wanafunzi kufika katika maduka ya kutoa huduma za kompyuta (cyber), wakiwataka wahudumu kuwabadilishia alama ili ziwe bora zaidi. Wengi wa wanafunzi wanaotafuta huduma hizi ni wale waliofeli.

Japo baadhi ya wahudumu wanakataa kutoa huduma hizo zinazokiuka maadili, kunao wanaoweka pesa mbele na kutekeleza matakwa ya wanafunzi wengi.

Inavyofanyika ni kuwa, mwanafunzi anafika kwenye ‘Cyber’ na kuwasilisha karatasi ya matokeo kisha inawekwa kwenye mitambo ya kompyuta na kukarabatiwa kiteknolojia, huku alama mbovu zikiboreshwa, bila ya kuadhiri mambo muhimu kwenye karatasi kama mihuri ya shule na sahihi za walimu.

Waziri wa elimu Amina Mohamed sasa ameelezea kughadhabishwa na tabia hiyo ya wanafunzi, ambayo tayari imewapotosha wazazi wengi.

Bi Mohamed alisema vingi vya visa hivyo vimeripotiwa katika afisi za elimu za kaunti, akiwataka wazazi kuhakikisha ikiwa gredi wanazokabidhiwa na wanao ni sahihi ama zilikarabatiwa.

“Lazima tukomeshe tabia hii kwa kila hali kwani haina manufaa katika sekta yetu ya elimu,” akasema Bi Mohamed.

Waziri huyo alieleza huzuni yake kuwa wanafunzi wa shule za upili wameamua kufanya wizi wa mitihani ama matokeo yake kwa kila njia.

“Hatutaki hali ambapo mwanafunzi anapata alama ya ‘A’ lakini ifikapo mitihani iliyo na umuhimu maishani, anaishia kupata alama za chini kushinda waliokuwa wakipata alama za B,” Bi Mohamed akaeleza washikadau wa elimu.

Aliwasihi wanafunzi kuzikubali alama wanazopata katika mitihani, na kufanya bidii kuziinua ikiwa hazijawaridhisha.

Alisema serikali itawachukulia hatua wale wanaochangia katika kukarabati matokeo ya wanafunzi na kuunda vyeti ghushi vya shule, akiongeza kuwa serikali itaunda mtandao utakaochapisha wote waliohitimu nchini.