Wachezaji 3 wa Rayon Sports wapigwa marufuku mechi ya Gor Mahia ikinukia

NA CECIL ODONGO

SHIRIKISHO la soka Barani Afrika (CAF) limewapiga marufuku wachezaji watatu wa Rayon Sports kwa kuzua  vita ndani ya uwanja wakati wa mechi yao dhidi ya Rayon Sports Julai 29.

Watatu hao, Yannick Mukunzi, Christ Mbondi na Kassim Ndayisenga waliadhibiwa kwa kupigwa marufuku na kutozwa faini ya hela za uhakika kutokana na matukio ndani ya uwanja wakati wa muda wa ziada wa mchezo huo.

Mukunzi amefainiwa Sh 1,000,000 na kupigwa marufuku ya mechi tatu huku Ndayisenga na Mbondi wakiadhibiwa vikali kwa kutumikia marufuku ya mechi mbili na faini ya Sh 550,000 kila moja.

Wachezaji hao sasa watakosa mechi ya pili ya mwisho ya makundi itakayowakutanisha na mabingwa mara 16 wa KPL nchini Gor Mahia Jumapili Agosti 19 katika uwanja wa MISC Kasarani, jijini Nairobi.

Masaibu hayo ya Rayon Sports huenda yakailetea K’Ogalo baraka kubwa kwa  kuwa mibabe hao wa KPLwanahitaji tu sare ya aina yoyote ili kufuzu hatua ya robo fainali ya kuwania ubingwa wa Kombe la mashirikisho barani Afrika.

Kwenye kipute dhidi ya USM Algiers, mabingwa hao wa ligi ya Rwanda waliongoza mechi hadi dakika ya 85 kupitia bao la dakika ya 28 la mshambulizi matata Ismaila Diara.

Hata hivyo uongozi wao ulikatizwa dakika ya 86 wakati Mohammed Hamia aliposawazishia USM.

Hata hivyo muda wa ziada ulishuhudia vita vikali, kasheshe na vitimbi uliohusisha wachezaji na benchi ya kiufundi za timu zote mbili. Hayo yalisababishwa na ikabu ya mchezaji wa Rayon Sports aliyeadhibiwa vikali na mwaamuzi wa mechi hiyo.