TZ na Rwanda waanza kipute kwa kishindo
Na GEOFFREY ANENE
WENYEJI Tanzania wamekanyaga Burundi 2-1 nao Rwanda wakalipua Sudan 3-1 katika siku ya kwanza ya mashindano ya soka ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika la wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 mwaka 2019.
Rwanda na Sudan zilitangulia kuteremka katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam saa nane mchana. Mabao ya Moise Nyarugabo dakika ya 30, Rodrigue Isingizwe (33) na Jean Rene Ishimwe (89) yalitosha kuipa Rwanda alama tatu muhimu na uongozi wa Kundi A. Sudan ilipata bao la kujiliwaza kupitia kwa Mohamed Badr Abaker dakika ya 71.
Tanzania, ambayo inatumia mashindano haya ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kujiandaa, ni mwenyeji wa mashindano ya Afrika (AFCON U/17) mwaka ujao. Serengeti Boys imelemea Burundi 2-1 kupitia mabao ya Kelvin Paul na Alistides Agiri Ngoda. Burundi imepata bao la kufuta machozi kutoka kwa Arthur Nibikora.
Kenya, ambayo iko chini ya kocha Michael Amenga, imetiwa katika Kundi B pamoja na Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini na Djibouti. Vijana wa Amenga wataanza kampeni yao dhidi ya Sudan Kusini mnamo Agosti 14 kabla ya kukutana na Djibouti (Agosti 17), Uganda (Agosti 19) na Ethiopia (Agosti 22) katika mechi zingine za kundi lao.
Mshindi wa mchujo huu wa eneo la Cecafa ama nambari mbili ikiwa Tanzania itanyakua taji, atajikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Afrika mwaka 2019.
Tanzania imefuzu moja kwa moja kuandaa mashindano hayo ya Afrika kama mwenyeji. Angola ilikuwa timu ya kwanza kujiunga na Tanzania. Ilishinda mchujo wa eneo la kusini mwa Afrika (Cosafa) kwa kupepeta Afrika Kusini 1-0 katika fainali Julai 29, 2018.