Mabao saba TZ ikiilemea Burundi Dar
Na Geoffrey Anene
RWANDA imeandikisha ushindi wa pili mfululizo kwenye mashindano ya soka ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 mwaka 2019 kwa kuzaba Burundi 4-3 jijini Dar es Salaam, Tanzania, Jumatatu.
Moise Nyarugabo aliongoza Rwanda kuvuna alama tatu dhidi ya majirani Burundi kwa kutikisa nyavu mara mbili. Alianzisha maangamizi haya dakika ya 23 kabla ya kuona lango tena dakika ya 55 baada ya Rodrigue Isingizwe na Keddy Nsanzimfura kucheka na nyavu dakika ya 43 na 44, mtawalia. Burundi ilijibu kupitia Arsene Irankunda dakika ya 27, Munaba Edson (60) na Iratanga Flavier (67).
Rwanda, ambayo ilikamilisha mechi hii na wachezaji 10 baada ya Jean Ishimwe kulishwa kadi ya pili kwenye mechi hiyo dakika za lala-salama, ina alama sita baada ya kusakata mechi mbili.
Ilisakama Sudan 3-1 kupitia mabao ya Nyarugabo, Isingizwe na Ishimwe katika mechi ya ufunguzi Agosti 11. Sudan ilipata bao la kufuta machozi kutoka kwa Mohamed Badr.
Rwanda inaongoza Kundi A kwa alama sita nayo Tanzania ni ya pili kwa alama tatu ilizopata kwa kukung’uta Burundi 2-1 Agosti 11. Tanzania inatumia mashindano haya kujipima nguvu kwa sababu ilifuzu moja kwa moja kwa Kombe la Afrika kama mwenyeji.
Kundi B linaleta pamoja Kenya, Sudan Kusini, Djibouti, Ethiopia na Uganda. Sudan ililima Djibouti 2-1 nayo Uganda ikapepetwa 1-0 na Ethiopia katika mechi za kwanza za kundi hili Agosti 12. Kenya itaanza kampeni yake dhidi ya Sudan Kusini mnamo Agosti 14.
Mshindi wa mashindano haya ya Afrika Mashariki na Kati ataungana na Tanzania mwaka 2019. Ikiwa Tanzania itaibuka bingwa wa Afrika Mashariki na Kati, nambari mbili atajikatia tiketi.