Gor yakanusha kutorokwa na Walusimbi
Na CECIL ODONGO
UONGOZI wa Mabingwa mara 16 wa KPL Gor Mahia umejitokeza kimasomaso na kukanusha vikali taarifa zilizoibuka kuhusu kuuzwa kwa kiungo Godfrey Walusimbi kwa mibabe wa soka nchini Afrika Kusini, Kaizer Chiefs.
Wulusimbi kwa sasa yuko Afrika Kusini na inatarajiwa atasaini mkataba na majigina hao wa ligi ya Absa iwapo wataafikiana kuhusu kanuni na sheria za kufanya kazi nchini humo
Hata hivyo Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Omondi Aduda, amesema kwa mwanadimba huyo ni mali yao na hawajapokea ofa kutoka kwa timu yoyote inayopania kutwaa huduma zake.
“Nataka niweke swala hili wazi kwa mashabiki wetu kwamba Walusimbi ni mchezaji wetu na ana mkataba nasi kwa muda wa mwaka moja na nusu. Hatujapokea wasilisho lolote kutoka kwa klabu yotote inayopania kumsajili,” akasema Aduda.
Vile vile alishtumu Kaizer Chiefs kwa kutofuata sheria iwapo wanataka huduma za Walusimbi kwa sababu hawajaiandikia Gor Mahia barua rasmi ili kuwaelezea nia yao.
“Hakuna sheria iliyofuatwa na kile kinachofanyika sasa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za Shirikisho la Soka Duniani, FIFA,” akaongeza Aduda.
Majagina hao wa soka ya Afrika Kusini wanasemekana kuvutiwa sana na kiwangi cha uchezaji wa Walusimbi na wanamwona kama dawa mjarabu kwa difensi yao inayovuja sana.
Walusimbi amekuwa mhimili mkubwa kwa kikosi cha K’Ogalo katika mechi za ligi na michuano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho Barani Afrika(CAF).