TATU CITY: Malumbano bungeni kuhusu ukwepaji wa ushuru wa Sh6 bilioni
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wanaochunguza madai kwamba wakurugenzi wa kampuni ya ujenzi wa nyumba ya Tatu City, walikwepa ushuru walilumbana wakati wa kikao cha kumhoji mmoja wa wakurugenzi wake, Vimal Shah.
Wanachama wa kamati ya bunge kuhusu Ardhi walirushiana cheche za maneno Alhamisi wakati Bw Shah alipotakiwa kujibu madai ya Mbunge wa Cherangany Joshua Kutuny kuhusu ukwepaji ushuru.
Jaribio la Kutuny kumtaka Bw Shah ajibu shutuma kwamba amewasajili wageni kama wenye hisa wa Tatu City, lilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanachama wengine wa kamati hiyo ya ardhi.
“Inadaiwa kwamba serikali ilipoteza zaidi ya Sh6 bilioni kutokana na ada za stempu na ukwepaji ushuru. Kilicho muhimu hapa ni masilahi ya umma, watu ambao wanakwepa ushuru mheshimiwa mwenyekiti,” akasema Kuttuny.
Wanachama wengine waliingilia kati na kumshambulia Bw Kuttuy kwa maneno.
“Umepotoka. Unazungumzia ukwepaji ushuru upi? Tumekuwa tukiwasikiza mashahidi wengi kuhusu suala hili na hatujakumbana na madai kama haya. Nahashon Nyaga alikuwa hapa na akasema haukuwa ukwepaji ushuru bali kucheleweshwa kwa malipo,” Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino akasema.
“Hatuwezi kusema kuwa baadhi ya wakurugenzi wa Tatu City walikwepa ushuru ilhali suala hili bado linachunguzwa. Tuendelea na mahojiano na ikiwa na ukweli utabainika baadaye,” akasema Mbunge wa Likoni Bi Mishi Mboko.
Wabunge waliendelea kulaumiana huku kukiibuka madai kuwa baadhi yao walikuwa wakilinda masihali fulani katika suala hilo. Ilimbidi Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt Rachel Nyamai kuingilia kati na kukomesha majibizano hayo.
Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi ambaye alionekana kushangazwa na tabia za wenzake alisema malumbano hayo yalikuwa yakishusha hadhi ya asasi ya bunge.
“Wengine wetu wanatafakari kujiuzulu kama wabunge kutokana na tabia kama hizi. Huenda majina yetu yakaharibiwa kufuatia malumbano kama hayo. Yeyote aliyefika mbele yetu anafaa kupewa nafasi ya kijieleza,” akasema Mbunge huyo wa chama cha ODM.
Bw Shah alikama madai kuwa wakurugenzi wa Tatu City walikwepa kulipa ushuru kwa serikali, akisema hamna makosa kwake kuhusu kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bidco Afrika na mkurugenzi wa Tatu City.
Mnamo Julai 25, Mwenyekiti wa Tatu City Nyaga na mmiliki wa hisa Stephen Mwagiru walifika mbele ya kamati ya hiyo ya ardhi ambapo waliiomba iingilie kati ili kulinda masilahi ya Wakenya katika mpango huo wa nyumba.
Waliwasuta makurugenzi wa asili ya kigeni kwa kukwepa kulipa ushuru.
Udanganyifu
Bw Mwangiru aliwasilisha stakabadhi zilizoonyesha kiasi cha pesa zilizodaiwa kulipwa na baadhi ya wawekezaji na kiasi cha pesa ambazo zilionyesha katika rekodi za wizara ya ardhi.
“Tuligundua udanganyifu uliofanyika wakati wa usajili wa hatimiliki ya ardhi katika Wizara ya Ardhi. Nina stakabadhi zinazoonyesha kuwa ardhi ambayo imeuzwa kwa bei ya Sh1 bilioni inadaiwa kuuzwa kwa Sh200 milioni, lengo likiwa ni kukwepa ada ya stampu na ulipaji ushuru wa mapato,” Mwagiru akasema.
Kamati hiyo ardhi inachunguza ukweli kuhusiana na malalamishi yaliyowasilishwa mbele yake na wakazi 1,300 wa Kiambu kupitia Mbunge wao Jude Njomo.
Wanaitaka Bunge la Kitaifa kuingilia kati kuwazuia wawekezaji wa kigeni katika Tatu City kutwaa ardhi yao.
Nyaga, Mwagiru na Shah ni wakurugenzi watu katika kampuni za Tatu City na Kofinaf Company Ltd, ambazo zina uhusiano wa karibu na zinamilikiwa na wenyehisa ambao ni wa asili ya Kenya na mataifa ya kigeni.