• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 5:55 AM
TAHARIRI: Wabakaji hawafai huruma yoyote

TAHARIRI: Wabakaji hawafai huruma yoyote

NA MHARIRI

KESI za unajisi zimeendelea kuwa janga humu nchini kiasi kwamba siku haipiti bila kusikia kisa kimeripotiwa cha kutamausha, pamoja na kesi mahakamani zikirundikana zikisubiri kuamuliwa.

Katika kesi ya jana mahakamani Eldoret, pasta aliyeshtakiwa kunajisi mtoto wa umri wa miaka mitano alifika kupokea hukumu akifanya sarakasi za kunyunyiza ‘mafuta ya upako’ akisema alisingiziwa kitendo hicho. Hata hivyo, mahakama ilimsukumia kifungo cha maisha kwa kosa hilo.

Suala la ubakaji na haswa unajisi wa watoto limekuwa donda sugu katika siku za hivi punde, jambo linaloibua wasiwasi kwa wazazi na mijadala kwenye kumbi nyingi kuhusu ni nini haswa kinachoendelea katika dunia ya leo.

Watoto wachanga, wengine hata wa umri usiofikirika wanadhulumiwa kimapenzi. Endapo gumzo linarudi kwenye maudhui yasiyo na mashiko kwamba “waume wanachochewa kuwa wabakaji kwa sababu ya mavazi mabaya ya wanawake”, unajiuliza kwa kweli ni nini mwanamume mzima aliona kilichomvutia kimapenzi kwa mtoto wa miaka mitano.

Bila shaka ikija suala la unajisi na ubakaji, kigezo huwa sio ‘kuvutiwa’ vile bali huwa ‘kuadhibu’ au ‘kudhulumu’ mwathiriwa kwa sababu za kihalifu.

Lakini kama jamii tunafaa tuepuke kwa vyovyote vile kudhalilisha mazungumzo ya mkazo kuhusu kupambana na janga la dhuluma za kimapenzi kwa kupatia kipau mbele visa vya mshukiwa ‘kusingiziwa’.

Ni kweli, kuna wakati mwingi ambapo washukiwa, ambao kwa mara nyingi huwa wanaume, hujikuta kusingiziwa visivyo kosa la unajisi na kuna watu wengi walioathiriwa zaidi kimaisha kutokana na kuwekelewa makosa.

Ila kama taifa tutakuwa tunahatarisha kuingia kwenye mtengo hatari wa kudunisha athari kamilifu zinazowakumba waathiriwa wa ubakaji na unajisi.

Ukweli ni kwamba mwanamke na haswa watoto hubadilikiwa kabisa na maisha pindi anapokuwa mwathiriwa wa ubakaji na unajisi. Maisha hupoteza maana kwa kuathirika kisaikolojia, kimwili na kikazi kwa sababu bado jamii ni ile ile itakayowaangalia kama walio na upungufu fulani.

Tunapaswa tutie bidii kikamilifu kupambana na dhuluma za kimapenzi na wanaopatikana na hatia wapewe hukumu nzito zaidi kwa sababu hatungependa kukuza familia ambayo haitambui wala kuthamini umuhimu wa maadili na haki.

You can share this post!

MUTANU: Serikali idhibiti bei ili kupunguzia Mkenya mzigo...

Jeff Koinange taabani kwa kumuuliza Atwoli maswali ya...

adminleo