Oduor aomba Mathare walaze Nakumatt wapande nafasi ya 4 KPL
NA CECIL ODONGO
MSHAMBULIZI wa Mathare United Chrispin Oduor amesema kwamba timu hiyo ina uwezo wa kuibwaga Nakumatt FC na kupunguza pengo la alama tano kati yao na Sofapaka FC inayoshikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la KPL.
Vijana wa kocha Francis Kimanzi watapepetana na Nakumatt Jumamosi Agosti 18 ugani Camp Toyoyo wakilenga kupunguza pengo hilo hadi alama moja na hilo liatatimia iwapo watadumisha ushindi dhidi ya Sharks jinsi walivyofanya katika mechi ya mkondo wa kwanza walipowabwaga 3-2.
Mathare United hatimaye walimaliza ukame wa mechi nane bila ushindi baada ya kuilaza Kariobangi Sharks 2-1 katika mechi ya KPL iliyosakatwa ugani Camp Toyoyo Agosti 12.
“Tuko tayari kupigana kwa jino na ukucha kupata alama zote tatu. Nakumatt ni timu iliyoimarika sana lakini tukitia bidii jinsi tulivyofanya katika mechi zilizopita tutaibuka washindi,” akasema Oduor kupitia mtandao wa klabu hiyo.
Ingawa Oduor ameyatia wavuni mabao manne hadi sasa, idadi hiyo ni chini mno ikilinganishwa na msimu wa 2016/17 alipocheka na nyavu za wapinzani mara 11.
Hata hivyo, sogora huyo amechangia pakubwa mabao 38 yaliyofungwa na Mathare msimu wa 2017/18 ikiwemo bao alilolifunga dhidi ya Sharks.
“Bao nililolifunga katika mechi dhidi ya Sharks limenitia motisha sana na nalenga kufanya vivyo hivyo katika mechi ya Jumamosi,” akaongeza Oduor.
Mathare United wanashikilia nafasi ya sita katika msimamo wa jedwali la KPL kwa alama 38 alama sawa na Ulinzi Stars walio katika nafasi ya tano ingawa United wanadunishwa na idadi ya mabao.