• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
ONYANGO: Mjadala wa kuhalalisha bangi haufai kupuuzwa

ONYANGO: Mjadala wa kuhalalisha bangi haufai kupuuzwa

Na LEONARD ONYANGO

BUNGE la 12 linazidi kujizolea aibu tele. Hivi karibuni baadhi ya waheshimiwa walipokea mlungula wa Sh10,000 kila mmoja kutupilia mbali ripoti ya sukari ya magendo iliyodaiwa kusheheni sumu.

Wakati wa Kombe la Dunia, baadhi ya wabunge walitumia mamilioni ya walipa ushuru na kuandamana kiguu na njia hadi Urusi kwenda kushuhudia fainali.

Walituhadaa kwamba wanaenda kujifunza jinsi ya kuandaa mikutano au matamasha makubwa.

Waliporejea humu nchini wabunge hao ambao wengi wao ni wanachama wa Kamati ya Michezo Bungeni inayoongozwa na mbunge wa Machakos Mjini Victor Munyaka ‘wakaiba’ ripoti za watu mitandaoni, wakaweka majina yao na kuiwasilisha bungeni!

Bunge linafaa kujiondolea aibu hii kwa kufanya ziara zitakazosaidia Kenya kustawi kiuchumi na kuwapunguzia Wakenya gharama ya maisha.

Hivyo, basi kuna haja ya wabunge kuzuru mataifa ambayo yamehalalisha matumizi ya bangi ili kujifunza jinsi Kenya inaweza kujipatia mapato kutokana na zao hilo ambalo limeharamishwa hapa nchini.

Mjadala kuhusu ikiwa bangi inafaa kuhalalishwa au la umekuwepo kwa muda mrefu lakini hakuna utafiti uliofanywa kubaini njia tunazoweza kutumia kuhakikisha kuwa serikali inajipatia ushuru kutokana na zao hili.

Mjadala huo ulifufuliwa wiki iliyopita na mwanauchumi David Ndii aliyetaka serikali kuhalalisha bangi ili kujipatia mapato badala kuendelea kuiharamisha ilhali biashara yake imenoga mitaani na inatumiwa na maelfu ya Wakenya.

Kwa mfano, inakadiriwa kuwa nchi ya Canada iliyohalalisha uvutaji wa bangi miezi miwili iliyopita huenda ikajipatia mapato ya zaidi ya Sh385 bilioni (Dola za Canada 5 bilioni) kwa mwaka.

Mataifa mbalimbali, yakiwemo Zimbabwe, Ureno, Lebanon, Argentina, Colombia, Mexico, yamehalalisha bangi kwa ajili ya matibabu.

Nchini Uruguay ambapo pia bangi imehalalishwa, watu wa umri wa miaka 18 ndio wanaruhusiwa kuvuta kiasi fulani cha bangi kwa wiki.

Watumiaji wa zao hilo huchukuliwa alama za vidole kila wanapoenda kununua katika maduka maalumu kuhakikisha kuwa hawapitishi kiasi kilichoruhusiwa na serikali kwa wiki.

Licha ya kuharamishwa, bangi inapatikana kwa urahisi katika maeneo mbalimbali humu nchini haswa katika mitaa ya mabanda.

Jambo la kusikitisha ni kwamba hata watoto wamekuwa wakivuta bangi kiholela. Wafanyabiashara walaghai wanaojihusisha na biashara hiyo haramu wanavuna mamilioni ya fedha huku serikali ikiambulia patupu.

Kuhalalishwa kwa zao hilo, hata kama ni kwa ajili ya matumizi ya matibabu, kutasaidia serikali kujipatia mapato na kudhibiti biashara hiyo.

Wakati umewadia kwa Mamlaka ya Kukabiliana na Matumizi ya Dawa za Kulevya (Nacada) kushirikiana na idara nyinginezo kuendesha utafiti ili kubaini jinsi Kenya inaweza kujipatia mapato ya ziada kutokana na bangi badala ya kuwatoza Wakenya ushuru wa juu kila uchao.

You can share this post!

Kizimbani kwa kutumia jina la Ruto kuiba vipakatilishi 2,800

NGILA: Kampuni ziheshimu taarifa za siri za Wakenya

adminleo