Ukosefu wa hela waikosesha Gor usingizi kuhusu safari ya Algeria
NA CECIL ODONGO
MABINGWA mara 16 wa KPL Gor Mahia hawana uhakika wa kusafiri hadi Algeria na kuwajibikia mechi yao ya mwisho ya makundi dhidi ya USM Algier Agosti 29 kutokana na ukame wa fedha kambini mwao.
K’Ogalo wanahitaji Sh 6.1 milioni kufanikisha safari hiyo na ombi walilolituma kwa serikali kuingilia kati na kuwanunulia tiketi za usafiri kupitia Shirikisho la Soka nchini FKF bado halijajibiwa.
Katika barua hiyo iliyotumwa kwa Katibu katika wizara ya michezo Kirimi Kaberia, Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF Robert Muthomi anafafanua kwa mapana na marefu jinsi mabingwa hao wanavyozidi kung’aa kati mashindano hayo na kuiomba wizara iwanunulie tiketi za ndege ili wawajibikie ratiba hiyo.
“Gor Mahia wanashikilia uongozi wa kundi lao na iwapo watawajibikia mechi hiyo na kutwaa ushindi, watautokomeza ukame wa miaka 30 tangu klabu kutoka Kenyai ifuzu kwa awamu ya robo fainali ya mechi za CAF,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia Omondi Aduda alithibitisha kwamba hawajapokea habari zozote kutoka kwa serikali wala FKF ingawa muda unazidi kutokata Agosti 29 kukaribia.
Vile vile alilalamika kwamba bei ya tiketi za ndege imepanda na kufikia kati ya Sh 135,000 na Sh 156,000 tangu waandike barua huku akasisitiza kwamba kwa kuwa wanawakilisha serikali ingekuwa bora wakinunuliwa tiketi hizo.
“Tunaenda kama wawakilishi wa serikali na kwa kuwa tutakuwa watu 30 tunahitaji 6.1 milioni kugharimia kila kitu,” akasema Bw Aduda.
Aidha afisa huyo alifafanua kwamba bajeti ya kuandaa mechi dhidi ya Rayon Sports siku ya Jumapili Agosti 19 na mechi za ugenini za KPL katika miji ya Kisumu, Nakuru na Mombasa kwa muda wa wiki mbili imehakikisha wanasalia bila kitu katika akaunti zao.
Gor Mahia watahitaji ushindi dhidi ya USM Alger ili kujihakikishia nafasi katika robo fainali ya kipute hicho baada ya kuchapwa na Rayon Sports Jumapili.