Fedheha Ushuru FC kukosa jezi za kuchezea
NA CECIL ODONGO
FANI ya soka nchini ilishuhudia aibu ya mwaka Jumatatu Agosti 20 wakati timu ya Ushuru FC inayoshiriki ligi ya Supa walipolazimika kutumia jezi yenye nembo ya ‘Boca Juniors’ waliyoazima katika mechi ligi hiyo dhidi ya Atlanta uwanjani Camp Toyo.
Imebainika kwamba sare za kawaida za wachezaji wa Ushuru FC zimezeeka kiwango cha kutotumika tena na uongozi wa washiriki hao wa zamani wa KPL hauonekani kushughulikia hilo na maslahi mengine ya wachezaji.
Kikosi hicho cha kocha Ken Kenyatta kiliishia kupoteza mechi hiyo 2-0, hii ikiwa pigo kwa juhudi zao za kufuzu kurejea KPL kwa kuwa sasa wameporomoka hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la NSL, alama tatu nyuma ya viongozi Western Stima.
Talanta FC waliyapata mabao yao kupitia wachezaji Emmanuel Mogaka na Rodgers Omondi. Awali walikuwa wamepoteza mechi dhidi ya nambari mbili Nairobi Stima kwa mabao 2-1 kabla ya kuagana sare ya 1-1 na Coast Stima ugani Camp Toyoyo.
Kulingana na moja wa wachezaji aliyeomba jina lake libanwe, usimamizi wa Ushuru FC umewatelekeza na kukataa kuheshimu mikataba yao.
“Kwanza wamepunguza marupurupu yetu na kuanza kuyatoza ushuru. Isitoshe wamekataa kutulipa bonasi zetu za kushinda mechi. Ushuru ni klabu kubwa, Iweje tukose sare, mipira na vifaa vingine muhimu katika soka?. Tumesikitika sana na hatuna motisha kabisa,” akasema mwanadimba huyo.
Msimu wa 2016/17 timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya tatu na ikawalazimu kucheza dhidi ya Thika United kwenye mechi ya kufuzu kuingia KPL ambayo walipoteza kwa mabao 2-1