IPSOS: Kibaki na Raila si wafisadi
Na PETER MBURU
WAKENYA wengi wanaamini kuwa kiwango cha ufisadi cha Rais mustaafu Mwai Kibaki na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ni cha chini mno, wakilinganishwa na viongozi wengine wa kisiasa waliopo ama waliowahi kuhudumu ambao wako uhai.
Kulingana na utafiti uliofanywa na kampuni ya Ipsos, ni asilimia tano tu ya wakenya ambao wanadhani viongozi hao walikuwa wafisadi, huku kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka aidha akioshwa na wakenya, kwani ni asilimia moja tu wanaodhani ni mfisadi.
Utafiti huo uliofanywa kati ya Julai 25 na Agosti 2 ulinuia kubaini wanavyodhani ama kujua kuhusu ufisadi nchini na matokeo yake yalitolewa jana.
Akitoa matokeo hayo katika makao makuu ya Ipsos, Lavington Jijini Nairobi jana, mtafiti mkuu wa kampuni hiyo Prof Tom Wolf aidha alisema wakenya wengi hawaamini kuwa wakubwa kwenye serikali na wafanyabiashara wenye umaarufu watahukumiwa.
“Ni asilimia 17 pekee ya wakenya ambao wanaamini kuwa kuna uwezekano kwa wale wanaochukuliwa kuwa ‘samaki wakubwa’ kuhukumiwa, huku asilimia 73 wakiamini hilo haliwezekani,” akasema Prof Wolf.
Kulingana na utafiti huo vilevile, bado asilimia 35 ya wakenya haiamini kuwa Rais Uhuru Kenyatta amejitolea kikamilifu kupigana na ufisadi, asilimia 27 yao wakiwa wafuasi wa chama chake cha Jubilee. Ni asilimia 21 pekee wanaoamini kwa uhakika kuwa Rais Kenyatta atafaulu kupunguza ufisadi nchini, huku 31 wakidhani tu ila bila kuwa na uhakika kuwa atatoboa.
Asilimia 17 ya waliohojiwa walisema haonyeshi dalili ila kuna uwezekano, huku ailimia 24 wakiwa na hakika kuwa hatafaulu.
Wengi wa waliohojiwa walitaja suala la kujihusisha na uongozi wa kisiasa na vitisho kutoka kwa watu wenye umaarufu, kama kikwazo kikuu cha vita dhidi ya ufisadi nchini.
“Jambo la kushangaza ni kuwa asilimia nne ya wakenya wanadhani kuwa hakuna chochote kitakachofanywa chaweza kumaliza ufisadi Kenya,” akasema mtafiti huyo.
Lakini asilimia 31 walipendekeza adhabu kali zaidi kwa wanaopatikana na hatia, 23 wakimtaka Rais kuwapiga kalamu wale wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi nao asilimia 17 wakipendekeza uhamasisho zaidi kwa umma.