Mshindi kati ya Gor na Ingwe kuumiza nyasi dhidi ya Hull City Mei 13

Na CECIL ODONGO

KLABU ya Hull City ya Uingereza itapambana na mshindi kati ya wapambe wa ligi Gor Mahia na AFC Leopards katika mechi inayotarajiwa kusakatwa Mei 13, 2018.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Klabu ya Hull City inayoshiriki kwenye ligi ya daraja la pili kucheza mechi dhidi ya wachezaji kutoka taifa letu.

Mwaka wa 2017 timu hiyo ilivaana na kikosi cha KPL All Stars  na kushinda kwa mabao 2-1.

Kikosi cha Hull City kinatarajiwa kutua hapa nchini Mei 11 kwa maandalizi ya mechi inayosubiriwa kwa hamu na ghamu na wapenzi wa soka hapa nchini.

Hata hivyo kutachezwa soka ya kusisimua kati ya watani wa tangu jadi Gor Mahia na AFC Leopards Mei mosi uwanjani Afraha Kaunti ya Nakuru. Mshindi katika mtanange huo atakuwa na fahari na tija ya kukutana na kikosi cha Hull City.

Katibu katika Wizara ya Michezo Kirimi Kaberia amewapa matumaini wapenzi wa soka kwamba uwanja wa kimaitaifa wa Moi Kasarani utakuwa tayari na utatumika kuandaliwa kwa mechi hiyo kubwa.

“Tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba uwanja wa Kasarani ambao umekuwa ukikarabatiwa unakuwa tayari kabla ya siku ya mchuano huo. Tutazuru uwanja huo kukagua hali lakini kufika mwezi Juni mwaka 2018 lazima shughuli za ukarabati ziwe zimeisha,”  akawaambia wanahabari.

Nyanja za Nyayo na Kasarani zimekuwa zikifanyiwa ukarabati na Klabu nyingi zinazoshiriki KPL zimekuwa zikitatizika kuhusu nyanja za kuchezea mechi za ligi.

Matokeo duni yazidi kumwandama Okumbi

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Stanley Okumbi anazidi kuandamwa na matokeo mabaya baada ya Rwanda kubandua timu yake ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 nje ya michuano ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika mwaka 2019, Jumamosi.

Okumbi, ambaye aliongoza timu ya taifa ya watu wazima Harambee Stars katika ziara mbovu ya Morocco mwezi Machi ilikolimwa na wanyonge Jamhuri ya Afrika ya Kati (3-2) na kutoka sare dhidi ya Comoros (1-1), alishuhudia timu yake mpya ya Under-20 ikitoka 0-0 dhidi ya Rwanda uwanjani Nyamirambo jijini Kigali hapo Aprili 21 na kufungiwa nje ya raundi ya pili kupitia bao la ugenini.

Rising Stars, jinsi timu hiyo ya Kenya inafahamika, ilikuwa imekabwa 1-1 uwanjani Kenyatta mjini Machakos katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya kwanza mnamo Aprili 1, 2018. Iliaga mashindano kwa bao la ugenini.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza, Richard Odada alifungia Rising Stars dakika ya saba kabla ya Rague Byikingiro kusawazishia Rwanda dakika ya mwisho.

Rwanda sasa inasonga mbele kumenyana na mabingwa wa Afrika Zambia katika raundi ya pili.

Manvir Baryan ashinda mbio za magari Afrika Kusini

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Manvir Baryan ameibuka mshindi wa mbio za magari za Afrika duru ya Afrika Kusini, Jumamosi.

Baryan, ambaye alitawazwa mfalme wa Mbio za Magari za Afrika mwaka 2017 akishirikiana na mwelekezi wake Drew Sturrock katika gari la aina ya Skoda Fabia, alianza duru hii ya tatu kwa kumaliza sehemu ya kwanza katika nafasi ya sita.

Hata hivyo, aliimarika na kushinda sehemu za pili na tatu, akatupwa nafasi ya nane katika sehemu ya nne, akarejea nambari moja sehemu ya tano, akateremka hadi nambari tatu sehemu ya sita na kumaliza mkondo huo wa kwanza uliojumuisha kilomita 105.9 kwa kushikilia nafasi ya sita katika sehemu ya saba.

Alianza mkondo wa pili na lala salama kwa kurukia nambari mbili katika sehemu ya nane na kuteremka nafasi moja katika sehemu wa tisa. Alitawala sehemu ya 10 na kumaliza sehemu ya 11 katika nafasi ya tatu. Alishinda sehemu ya 12 na tena 13 na 14 na 15 (mwisho). Mkondo wa pili ulijumuisha kilomita 114.6.

Baryan alikamilisha mbio hizi za kilomita 220.5 kwa saa 2:47:43.9, dakika 3:14 mbele ya mabingwa wa duru hii ya Afrika Kusini mwaka 2017 Guy Botterill aliyeshiriikiana na Simon Vacy-Lyle katika gari la aina ya Toyota Etios.

Mathew Vacy-Lyle na mwekelezi wake Rikus Fourie waliridhika katika nafasi ya tatu pia wakiendesha Toyota Etios.

Walifuatwa na Leroy Gomes/Riyaz Latife (Mitsubishi Evo 9), AC Potgieter/Nico Swartz (Volkswagen Polo), JJ Potgieter/ Tommy du Toit (Ford Fiesta), Kleevan Gomes/Zunaid Khan (Mitsubishi Evo 9), Lee Rose/Elvene Vonk (Ford Escort), Tjaart Conradie/Mari van der Walt (Toyota Elios) nao Jacques du Toit na mwelekezi wake Ronald Rens wakafunga 10-bora (Volkswagen Polo).

Madereva 30 walianza mashindano, lakini 17 pekee ndiyo walimaliza. Wengine walijiuzulu katika sehemu mbalimbali za mashindano kutokana na matatizo mbalimbali.

Ushindi wa Manvir unafufua matumaini yake ya kutetea taji lake hasa baada ya kukosa kumaliza duru ya Afrika ya Safari Rally mwezi Machi nchini Kenya injini ya gari lake ilipojaa maji.

Kenya U-17 yatinga nusu fainali licha ya kupigwa 1-0 na Somalia

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeingia nusu-fainali ya mashindano ya soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yanayopamba moto nchini Burundi licha ya kuendelea kuandikisha matokeo mabaya.

Baada ya kupepeta Burundi 4-0 katika mechi ya ufunguzi ya Kundi A na kukabwa 0-0 na Ethiopia katika mechi ya pili, vijana wa kocha Michael Amenga walinyukwa 1-0 na Somalia katika mechi yao ya mwisho ya makundi Ijumaa.

Dhidi ya Burundi, Kenya ilivuna ushindi kupitia mabao ya Isaiah Abwal (mawili), Christopher Raila na Nicholas Omondi mnamo Aprili 14.

Mabao ‘yalikauka’ katika sare tasa dhidi ya Ethiopia hapo Aprili 17 kabla ya mambo kuharibika hata zaidi ilipozamishwa 1-0 na Somalia kupitia bao la Farhan Mohamed Ahmed lililopatikana dakika ya 15.

Kenya ilijkatia tiketi kwa kumaliza mechi za makundi ya pili kwa alama nne. Somalia ilikamilisha juu ya jedwali kwa alama saba. Ilipewa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ethiopia katika mechi ya ufunguzi baada ya Ethiopia kupatikana imechezesha wachezaji watatu waliopitisha umri wa miaka 17.

Ilitoka sare tasa dhidi ya Burundi katika mechi ya pili kabla ya kukumbusha Kenya taji halikuja kwa urahisi kwa kuipiga 1-0. Ilitumia mfumo wa kucheza wa mabeki watano, viungo wanne na mshambuliaji mmoja (5-4-1) kuangamiza Kenya.

Burundi ilikamilisha mechi zake za makundi kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Ethiopia, lakini matokeo haya hayakusaidia mataifa haya mawili kusalia mashindanoni.

Katika mechi za Kundi B, Uganda ilibwaga Sudan 3-0 na kuingia nusu-fainali kwa jumla ya alama nne baada ya kukaba Tanzania 1-1 katika mechi ya ufunguzi. Timu ya mwisho kufuzu kushiriki nusu-fainali itafahamika Jumapili pale Tanzania na Sudan zitakapoteremka uwanjani kumaliza udhia.

Kundi hili lilibaki na timu tatu baada ya Zanzibar kutimuliwa kwa kuwasili nchini Burundi na wachezaji 12 waliozidi umri wa miaka 17 katika kikosi chake.

Ethiopia na Zanzibar zilipigwa faini ya Sh500,252 na Sh1,500,757, mtawalia.

‘Wachezaji wa raga waliombaka msanii wakamatwe’

GEOFFREY ANENE

MWENDESHA mashtaka mkuu wa Kenya ameamrisha kukamatwa na kushtakiwa kwa wachezaji wawili wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande waliotuhumiwa kwa ubakaji, shirika la habari la Capital FM limeripoti Ijumaa.

Wachezaji hao Frank Wanyama na Alex Olaba kutoka klabu ya Kenya Harlequins wanatuhumiwa kumbaka mwanamuziki Wendy Kemunto mnamo Februari 10, 2018 katika jumba moja mtaani Kilimani jijini Nairobi.

Kupitia mtandao wake wa Instagram, Kemunto alidai Wanyama na rafiki yake walimbaka wakibadilishana siku yake ya kuzaliwa Februari 10 na kumuacha akiwa mjamzito.

Kemunto hakutaka kupiga ripoti kwa polisi kuhusu kisa hiki akihofia hakitachukuliwa kwa uzito, lakini baada ya kuenea kwenye mitandao ya kijamii, habari hizo zilifikia afisi ya Mwendesha mashtaka mkuu wa Kenya na akaahidi kuchunguza kesi hiyo hadi haki itendeke.

Kitengo cha ujasusi kimefanya uchunguzi wake na kutoa taarifa Ijumaa kwamba wachezaji hao watiwe nguvuni na kushtakiwa. Tovuti ya Capital FM imesema kwamba mwanamuziki huyo alidai alipewa dawa za kumfanya apoteze fahamu na wachezaji hao na kisha kushawishiwa kuingia katika nyumba moja na kubakiwa humo.

Harlequins ilithibitisha Aprili 3 kwamba ilipokea malalamishi kuhusu wachezaji hao ambao imeajiri. Iliongeza, “Kama mojawapo ya klabu kongwe nchini na inayoheshimika, tunafuata sheria za maadili zinazostahili kufuatwa kikamilifu na wachezaji na maafisa wa klabu. Kenya Harlequins pia haikubali kabisa tabia ya aina yoyote ya unyanyasaji wa kimapenzi,” klabu hiyo ilisema.

Kulingana na tovuti ya Shujaa Pride, Wanyama, ambaye jina lake la utani ni ‘Animal’ ama ‘magician’, alizaliwa Oktoba 20 mwaka 1994 na kujiunga na Shule ya Upili ya Nakuru High kabla ya kusomea “Actuarial science” katika Chuo Kikuu cha Strathmore na Sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Olaba, ambaye alisomea Shule ya Upili ya Alliance, ni mchezaji wa zamani wa klabu ya Strathmore Leos.

Rangers yalenga nafasi ya 3 ikimenyana na SoNy Sugar

Na CECIL ODONGO

KOCHA wa Klabu ya Posta Rangers Sammy ‘Pamzo’ Omollo amesema kwamba anatarajia upinzani mkali kutoka kwa Klabu ya SoNy Sugar katika pambano kali ya ligi siku ya Jumapili Uwanjani Awendo Green Stadium.

Omollo ambaye alishinda ubingwa wa ligi mwaka wa 2012.akinoa wanamvinyo Tusker, amewataka vijana wake kutowadharau wanaSoNy ambao msimu huu wanaonekana kusuasua ligini.

Wakiwa na motisha ya hali ya juu baada ya kuwashinda viongozi wa ligi Mathare United, Klabu ya Posta Rangers itaazimia kuishinda mechi hiyo ili kupaa hadi nafasi ya tatu ligini.

“SoNy Sugar imekuwa timu imara ligini na unapofikiri wako katika hali ngumu hapo ndipo watakapokubana na kukufunga haswa wakiwa nyumbani,” akasema Kocha Omollo.

Aliongeza kwamba wachezaji wa klabu hiyo ya Awendo watakuwa katika hali nzuri lengo lao likiwa kujitahidi kuridhisha kocha wao mpya.

Kwa upande wao SoNy wataweka mzaha kando katika jitihada zao za kujinasua kutoka eneo hatari la kuteremshwa ngazi kwenye msimamo wa jedwali la ligi.

Wakiwa na mkufunzi mpya Patrick Odhiambo aliyetoka Klabu ya Chemelil kuchukua mahala pa kocha wao wa zamani Salim Babu, wanasukari hao watakuwa na ari ya kuboresha matokeo yao ya wiki jana walipolazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Sofapaka FC.

Katika msimamo wa jedwali SoNy wako katika nafasi hatari ya 16 huku Posta Rangers wanaohesabiwa kama wagombezi halisi wa taji la KPL wakijikita katika nafasi ya nne nyuma viongozi Mathare United, GorMahia na AFC Leopards.

“Tumejitayarisha na nina imani kwamba tutashinda na kupata alama zote tatu,” akasema Kocha Omollo.

Mechi hiyo itaanza saa tisa kamili siku ya Jumapili.

Kocha wa Chemelil awataka vijana wake kufuata maagizo

Na CECIL ODONGO

KOCHA wa muda wa Klabu ya Chemelil Charles Odera amewataka wanasoka wake kukumbatia mbinu zake mpya za ukufunzi ili wasibabaike uwanjani jinsi walivyofanya katika mechi yao ya Jumamosi dhidi ya limbukeni Wazito FC.

Mkufunzi huyo ambaye alichukua nafasi hiyo kutoka kwa Patrick Odhiambo aliyekimbilia majirani zao na wanasukari wenza SoNy Sugar kama kocha mpya.

Mechi hiyo ikiwa ya kwanza kwake, Kocha Odera alikiongoza kikosi hicho kuwachabanga Wazito FC mabao 3-1 katika uwanja wao wa nyumbani.

Odera ambaye enzi zake alichezea timu hiyo na hata kutwaa mkoba wa unahodha alisema japo walitwaa ushindi, hakuridhishwa na jinsi wachezaji wake walivyosakata kabumbu duni.

“Kwa leo hatukucheza soka yetu. Niliwapa maagizo ya jinsi ya kuwakabili wapinzani wetu lakini hawakuyafuata,” alisema Odera akishiriki katika mahojiano baada ya mechi hiyo.

Hata hivyo alama hizo ziliwawezesha Chemelil kuimarisha nafasi yao ligini wakiwa sasa wapo katika nafasi ya sita alama moja tu nyuma ya nambari tano Sofapaka FC japo bado wana mechi moja hawajacheza.

Klabu hiyo mbili zinatarajia kugaragazana siku ya Jumamosi kwenye mtanange mkali wa ligi katika uwanja wa Chemeli Sport Complex kuanzia saa saba mchana.

Baada ya kupokezwa kichapo hicho Klabu ya Wazito ambayo wanashiriki msimu wao wa kwanza ligini sasa wameteremka hadi katika nafasi 12 kwenye msimamo wa jedwali la ligi.

Kenya yalazimishwa sare tasa na Ethiopia U-17

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeambulia sare tasa dhidi ya Ethiopia katika mechi yake ya pili kwenye mashindano ya soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 yaliyoingia siku yake ya nne nchini Burundi hapo Aprili 17, 2018.

Vijana wa kocha Michael Amenga walitafuta ushindi bila mafanikio. Ushindi ungewapa Wakenya tiketi ya kushiriki nusu-fainali wakiwa bado wanasalia na mechi moja ya Kundi A dhidi ya Somalia hapo Ijumaa.

Kenya ilianza kampeni kwa kunyuka Burundi 4-0 Aprili 14 nayo Somalia ilipata alama tatu na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ethiopia katika mechi yake ya ufunguzi Aprili 15.

Ethiopia ndiyo ilishinda Somalia uwanjani 3-1, lakini ikakonywa alama hizo baada ya kupatikana na hatia ya kuchezesha wachezaji watatu waliozidi umri wa miaka 17. Burundi na Somalia zilipangiwa kumenyana katika meci nyingine Aprili 17.

Kikosi cha Kenya: Wachezaji 11 wa kwanza – Maxwell Mulili (kipa), Lawrence Otieno, Telvin Maina, Christopher Raila, Arnold Onyango, Nicholas Omondi, Patrick Ngunyi, Hillary Okoth, Isaiah Abwal, Lesley Otieno, Mathew Mwendwa.

Wachezaji wa akiba – Brian Olango, Costah Anjeo, Nesta Wangema, Michael Abongo, Felix Chabaya, Daniel Ochieng, Said Musa.

Pigo kwa Gor Tuyisenge kukosa stakabadhi za kusafiri Afrika Kusini

Na GEOFFREY ANENE

GOR Mahia imepata pigo kubwa kabla ya mechi yake ya marudiano dhidi ya SuperSport United kwenye Kombe la Mashirikisho baada ya Jacques Tuyisenge, ambaye ameisaidia kushinda mechi tatu zilizopita, kukosa stakabadhi za kusafiri Afrika Kusini.

Mabao ya Mshambuliaji huyu kutoka Rwanda yalisaidia mabingwa mara 16 wa Kenya, Gor, kuzamisha Vihiga United 1-0 (Machi 31), SuperSport 1-0 (Aprili 8) na Wazito 1-0 (Aprili 11).

Yuko katika orodha ya wachezaji sita tegemeo, ambao kocha Dylan Kerr atakosa huduma zao.

Tatizo la stakabadhi za usafiri pia limefungia nje mvamizi wa Ivory Coast, Ephrem Guikan kuenda mjini Pretoria. Winga matata Godfrey Walusimbi bado amegoma kuchezea Gor hadi pale atakapolipwa ada ya uhamisho.

Kiungo Ernest Wendo yuko nje kwa sababu ya kulishwa kadi za njano katika mechi mbili zilizopita, moja dhidi ya Esperance katika Klabu Bingwa na dhidi ya SuperSport katika Kombe la Mashirikisho. Mabeki Wellington Ochieng’ na Karim Nizigiyimana wanauguza majeraha.

Mshindi kati ya Gor na SuperSport ataingizwa katika mojawapo ya makundi manne ya raundi ya 16-bora. Pia atajihakikishia tuzo ya Sh27 milioni.

Kirui kujizolea mamilioni kwa kusalia kileleni mwa jedwali

Na GEOFFREY ANENE

LICHA ya kupoteza ubingwa wa mbio za Boston Marathon hapo Jumapili jioni, Mkenya Geoffrey Kirui anaongoza vita vya kujinyakulia tuzo ya Sh25 milioni kwenye Marathon Kuu Duniani (WMM) ya msimu wa 11.

Kirui, ambaye alijishindia Sh7.5 milioni kwa kumaliza makala ya 122 ya Boston Marathon katika nafasi ya pili, yuko juu ya jedwali kwa alama 41. Alipata alama 25 kwa kushinda Riadha za Dunia mnamo Agosti 6, 2017 na kujiongezea alama 16 kwa kumaliza wa pili nyuma ya Mjapani Yuki Kawauchi mjini Boston.

Bingwa wa Marathon Kuu Duniani wa msimu wa 11 atafahamika baada ya mbio za London Marathon nchini Uingereza hapo Aprili 22, 2018. Matumaini yake ya kushinda Marathon Kuu Duniani yatategemea sana matokeo ya Wakenya wenzake Daniel Wanjiru na Eliud Kipchoge.

Wanjiru yuko jijini London kutetea taji naye Kipchoge alishinda Berlin Marathon nchini Ujerumani mwaka 2017. Wawili hawa wamezoa alama 25. Mshindi hupata alama 25 kwa hivyo wawili hawa wanaweza kufikisha alama 50.

Bingwa wa Tokyo Marathon nchini Japan, Dickson Chumba na mshindi mpya wa Boston Marathon Kawauchi pia wana alama 25, lakini hawashiriki mbio za London. Makala ya 38 ya London Marathon hapo Aprili 22 yanatarajiwa kuwa moto kwa sababu yamevutia Wanjiru, Kipchoge na mahasimu wakubwa wa Kenya, Mo Farah (Uingereza) na Kenenisa Bekele (Ethiopia).

Vita vya taji la wanawake jijini London pia vinatarajiwa kuwa vikali. Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya marathon ya wanawake pekee Mary Keitany (saa 2:17:01) atakabililiana na Muethiopia bingwa wa Chicago Marathon Tirunesh Dibaba (Ethiopia). Wawili hawa wanaongoza jedwali la wanawake la Marathon Kuu Duniani kwa alama 41 kila mmoja. Kipchoge anatafuta taji lake la tatu mfululizo la Marathon Kuu Duniani baada ya kushinda msimu wa tisa na 10.

Keitany pia ni bingwa mara mbili wa Marathon Kuu Duniani. Alishinda msimu wa sita na tisa.

Msimamo wa Marathon Kuu Duniani (5-bora):

Wanaume

Geoffrey Kirui (Kenya) alama 41

Dickson Chumba (Kenya) 25

Yuki Kawauchi (Japan) 25

Daniel Wanjiru (Kenya) 25

Eliud Kipchoge (Kenya) 25

Wanawake

Mary Keitany (Kenya) alama 41

Tirunesh Dibaba (Ethiopia) 41

Ruti Aga (Ethiopia) 32

Rose Chelimo (Bahrain) 25

Shalane Flanagan (Marekani)

Matokeo ya Boston Marathon (2018):

Wanaume

Yuki Kawauchi (Japan) saa 2:15:58

Geoffrey Kirui (Kenya) 2:18:23

Shadrack Biwott (Marekani) 2:18:35

Tyler Pennel (Marekani) 2:18:57

Andrew Bumbalough (Marekani) 2:19:52

Scott Smith (Marekani) 2:21:47

Abdi Nageeye (Uholanzi) 2:23:16

Elkanah Kibet (Marekani) 2:23:37

Reid Coolsaet (Canada) 2:25:02

Daniel Vassallo (Marekani) 2:27:50

Wanawake

Desiree Linden (Marekani) 2:39:54

Sarah Sellers (Marekani) 2:44:04

Krista Duchene (Canada) 2:44:20

Rachel Hyland (Marekani) 2:44:29

Jessica Chichester (Marekani) 2:45:23

Nicole Dimercurio (Marekani) 2:45:52

Shalane Flanagan (Marekani) 2:46:31

Kimi Reed (Marekani) 2:46:47

Edna Kiplagat (Kenya) 2:47:14

Hiroko Yoshitomi (Japan) 2:48:29

Wabunge wa Kenya waduwazwa 3-1 na wenzao wa Uturuki

Na GEOFFREY ANENE

BUNGE FC imepoteza raundi ya kwanza ya mechi ya kirafiki dhidi ya Uturuki baada ya kulimwa 3-1 katika klabu ya michezo ya Parklands jijini Nairobi, Jumanne.

Vijana wa kocha Sylvester Ochola walipata bao la kufutia machozi kutoka kwa Seneta wa kaunti ya Kakamega, Cleophas Malala dakika tatu kabla ya kipenga cha mwisho kilie.

Timu ya Wabunge wa Kenya almaarufu Bunge FC ikipiga picha kabla ya kumenyana na wenzao kutoka Uturuki hapo Aprili 17, 2018. Picha/Geoffrey Anene

Katika mchuano huu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa haya, Uturuki iliizidi Bunge na chenga za maudhi na pasi za uhakika katika uwanja telezi baada ya mvua kunyesha jijini Nairobi mapema asubuhi.

Bunge haikuwa imetulia kabla ya kujipata bao moja chini baada ya Ibrahim Halil Yildiz kucheka na wavu dakika ya kwanza.

Timu ya Uturuki yapiga picha kabla ya kuvaana na Bunge FC katika mechi ya kirafiki uwanjani Parklands. Picha/Geoffrey Anene

Kenya ilipata nafasi murwa dakika chache baadaye, lakini Mbunge wa Rarieda Otiende Amolo hakukamilisha vyema ikabu kutoka kwa Mbunge wa Homa Bay, Peter Kaluma.

Uturuki kisha ilipata nafasi ya kuimarisha uongozi wake dakika mbili kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika pale Bunge ilifanya masihara ndani ya kisanduku chake na kutunuku wageni hao penalti.

Mwenyekiti wa Chama cha Urafiki cha Wabunge wa Kenya na Uturuki, Adan Keynan akijiandaa kupeana kombe kwa washindi Uturuki. Picha/Geoffrey Anene

Yildiz alivuta mkwaju huo kwa mguu wake wa kushoto, lakini kipa Jimmy Okwiri alikuwa macho na kuipangua. Hata hivyo, walinzi wa Bunge hawakumakinika na Sarikaya akahakikisha Uturuki haipotezi nafasi hiyo na kuiweka mabao 2-0 juu.

Huku muda ukiipa Bunge kisogo, Mbunge wa Nyali, Mohammed Ali alivuta krosi nzuri, lakini Victor Munyaka (Machakos Town) akapiga mpira hafifu uliodakwa na kipa.

Wabunge wa Kenya na Uturuki katika picha ya pamoja uwanjani Parklands. Picha/Geoffrey Anene

Sarikaya, ambaye alikuwa mwiba kwa timu ya Kenya kwa chenga zake na kasi pembeni kushoto, alipachika bao la tatu dakika ya 53 baada ya Okwiri na wenzake kuzembea.

Malala aliondolea Bunge aibu ya kumaliza mechi bila bao alipofuma wavuni ikabu safi kutoka pembeni kulia. Bunge ilipata frikiki hiyo baada ya nahodha Daniel Wanyama (Webuye West) kuangushwa nje ya kisanduku.

Kombe rembo lililowaniwa na timu ya Bunge FC na Uturuki. Picha/Geoffrey Anene

Timu hizi zinafanya mpango wa kuwa na mechi ya marudiano katika mji wa Antalya ama Istanbul. Bunge imeapa kulipiza kisasi ugenini. 

Madoya ahakikishia Zoo kuwa itasalia ligini

Na CECIL ODONGO

KIUNGO wa Klabu ya Zoo Kericho Michael Madoya amewahakikishia mashabiki wa timu hiyo kwamba hawatateremshwa ngazi mwisho wa msimu.

Madoyo ambaye alituzwa kama kiungo bora mbunifu mwaka 2017, alisikitikia matokeo mabaya ambayo yamekuwa yakisajiliwa na timu hiyo lakini akasema bado mwanya wa kujiimarisha upo.

Zoo Kericho Jumapili walionyesha kwamba si wanyonge katika ligi jinsi inavyodhaniwa baada ya kutoka nyuma na kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya miamba wa soka AFC Leopards.

Hadi sasa klabu hiyo kutoka Kaunti ya Kericho imeweza kushinda mechi mbili kati ya kumi iliyocheza na wanashikilia nafasi ya 17 kwenye msimamo wa jedwali la ligi inayoshirikisha timu 18.

“Kila timu huwa na wakati wake mgumu ambapo huwa wanalemewa lakini sisi kipindi hicho kinaelekea kuisha haswa baada ya sare dhidi ya AFC Leopards,” akasema kiungo huyo ambaye kando na talanta ya soka alisomea uanahabari.

Aidha alisisitiza kwamba hana presha zozote za kufikia kiwango chake cha mwaka 2017 na cha muhimu anacholenga ni kuisaidia timu kupata matokeo bora.

“Mimi sizingati kuibuka bora katika hiki ama kile lengo langu kuu ni kusaidia timu hii iepuke kuteremshwa ngazi,” akasema katika mahojiano baada ya mechi yao na Ingwe.

Zoo walipandishwa ngazi mwisho wa msimu jana baada ya kumaliza wa kwanza katika ligi ya daraja la pili na wanakibarua kigumu cha kuhakisha wanashinda mechi nyingi zilizosalia ili kutoka katika hatari ya kuteremshwa ngazi kufikia mwisho wa msimu.

Wabunge wa Kenya kuchuana na wenzao kutoka Uturuki

Na GEOFFREY ANENE

WABUNGE wa Kenya wataweka suti zao kando kwa mechi ya kirafiki dhidi ya wenzao kutoka Uturuki hapo Aprili 17, 2018.

Mchuano huu utasakatwa katika klabu ya michezo ya Parklands jijini Nairobi.

Bunge FC ya Kenya, ambayo imekuwa ikishiriki mashindano ya Afrika Mashariki kwa miaka kadhaa sasa, inatarajiwa kuwakilishwa na wabunge kama Kanini Kega (Kieni), Daniel Wanyama (Webuye West) na Otiende Amollo (Rarieda), miongoni mwa wengine.

Wabunge kutoka Uturuki wamekuwa humu nchini kwa karibu juma moja kufanya mazungumzo jinsi ya kuimarisha uhusiano kati ya mataifa haya katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu na biashara.

Mwenyekiti wa Chama cha Kirafiki cha Wabunge kutoka Uturuki na Kenya, Mahmut Kacar anatarajiwa kuongoza timu ya Waturuki.

Spika wa Bunge la kitaifa Justin Muturi atafungua rasmi mchuano huo wa kihistoria saa mbili asubuhi.

GOLD COAST AUSTRALIA: Lionesses wamumunywa kama pipi na New Zealand

Na GEOFFREY ANENE

LIONESSES ya Kenya imeanza kampeni yake ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa kunyolewa bila maji 45-0 dhidi ya New Zealand mjini Gold Coast, Ijumaa.

Warembo wa kocha Kevin Wambua walizidiwa nguvu, mbio na hata maarifa katika vipindi vyote viwili na kupoteza mchuano huo wa Kundi A kupitia miguso ya Portia Woodman (mitatu), Nial Williams (miwili), Gayle Broughton (moja) na Kelly Brazier (moja). Tyla Nathan-Wong alipachika mikwaju mitano kati ya sita aliyopiga.

Zilipokutana na kwa mara ya kwanza katika Michezo ya Olimpiki jijini Rio de Janeiro, Brazil, mwaka 2016, Kenya ilipapurwa 52-0 na New Zealand katika mechi za makundi. Inamaanisha kwamba Kenya bado haijapata kufunga alama yoyote dhidi ya mabingwa hawa mara nne wa Raga za Dunia.

Mechi ijayo ya Kenya itakuwa dhidi ya Canada saa sita na dakika 11 adhuhuri. Canada ilinyuka mabingwa wa Afrika, Afrika Kusini 29-0 katika mechi yake ya ufunguzi. Ilifunga miguso yake mitano kupitia Brittany Benn, Caroline Crossley, Hannah Darling, Sara Kaljuvee na Charity Williams. Nahodha Ghislaine Landry aliongeza mikwaju miwili.

Kenya itakamilisha mechi zake za makundi dhidi ya Afrika Kusini mnamo Aprili 14.

Wanawake kutoana jasho Mei 26 Kombe la Afrika raga

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Raga ya Afrika (Rugby Afrique) limetangaza tarehe za Kombe la Afrika la wachezaji saba kila upande la wanawake la mwaka 2018.

Taarifa kutoka shirikisho hilo limesema kwamba kombe hilo litaandaliwa Mei 26 na Mei 27 jijini Gaborone nchini Botswana.

Orodha ya mataifa yanayotarajiwa kushiriki kombe hili inajumuisha Afrika Kusini (mabingwa watetezi), Kenya, Botswana, Uganda, Zimbabwe, Morocco, Tunisia, Senegal, Madagascar na Mauritius.

Afrika Kusini ilizaba Kenya 17-12 katika fainali Septemba mwaka 2017 mjini Tunis nchini Tunisia.

Kombe hili litatumika kuchagua mwakilishi wa Bara Afrika katika makala yajayo ya Michezo ya Olimpiki yatakayofanyika jijini Tokyo nchini Japan mwaka 2020.

Kenya ilipeperusha bendera ya Afrika katika Olimpiki jijini Rio de Janeiro nchini Brazil mwaka 2016. Ilipata tiketi baada ya Afrika Kusini kujiondoa. Afrika Kusini imepiga Kenya katika fainali nne mfululizo za Afrika.

Jijini Rio, Lionesses ilinyukwa 52-0 na New Zealand, ikalemewa 40-7 na Ufaransa na kupoteza 19-10 dhidi ya Uhispania katika mechi za makundi. Ilipigwa 24-0 na Japan katika mechi za nusu-fainali ya kuorodhesha nambari tisa hadi 12 kabla ya kuzima Colombia 22-10 na kumaliza katika nafasi ya 11.

GOLD COAST AUSTRALIA: Matokeo ya aibu kwa Kenya mita 400 kuruka viunzi

Na GEOFFREY ANENE

PACHA Nicholas Bett na Aron Koech wameambulia pakavu katika mbio za mita 400 za kuruka viunzi kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola mjini Gold Coast, Australia, Alhamisi.

Bingwa wa dunia mwaka 2015, Bett, alivuta mkia baada ya kukamilisha umbali huo kwa sekunde 51.00. Licha ya kutopata matokeo mazuri tangu ufanisi huo wake jijini Beijing nchini Uchina miaka mitatu iliyopita, Bett alikuwa amepigiwa upatu kushindia Kenya medali.

Alikosa Riadha za Dunia za mwaka 2017 jijini London, Uingereza, kutokana na jeraha. Koech alikuwa jijini London, lakini hakufanya vyema. Aliondolewa mashindanoni katika nusu-fainali.

Mjini Gold Coast, Koech alimaliza katika nafasi ya sita kwa sekunde 50.02. Kyron McMaster kutoka Visiwa vya British Virgin, ambaye mwaka 2017 aliondolewa mashindanoni kwa kuvunja sheria za kutobadilisha laini jijini London, ametwaa ubingwa kwa sekunde 48.25.

Jeffery Gibson, ambaye alimaliza Riadha za Dunia katika nafasi ya tatu mwaka 2015, amenyakua nishani ya fedha kwa sekunde 49.10 naye Mjamaica Jaheel Hyde akaridhika na shaba kwa sekunde 49.16.

Kocha mpya wa Simbas atambulishwa

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA mpya wa timu yake ya raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Simbas, Ian Snook, ametambulishwa rasmi kwa umma jijini Nairobi, Alhamisi.

Raia wa New Zealand, Snook ameajiriwa kwa kandarasi ya mwaka mmoja. Atafanya kazi na raia mwenzake wa New Zealand, Murray Roulston pamoja na Wakenya Wangila Simiyu, Charles Ngovi, Christopher Makachia, Richard Ochieng’ na Dominique Habimana.

Snook na Roulston waliwasili nchini Kenya hapo Aprili 9. Snook anajaza nafasi ya raia wa Afrika Kusini, Jerome Paarwater, ambaye Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) lilimtema Desemba mwaka 2017.

Taarifa kutoka KRU zinasema kwamba majukumu makubwa ya raia hao wa New Zealand ni kuongoza Kenya katika kampeni ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2019.

“Wana ujuzi wa zaidi ya miaka 50 kati yao katika kazi ya ukufunzi katika viwango mbalimbali kutoka mataifa yanayokuwa na pamoja na timu ya taifa ya New Zealand,” KRU imesema.

Snook na Roulston watashughulikia idara za mashambulizi na ulinzi, mtawalia. Hata hivyo, Snook ndiye kocha mkuu.

Ratiba ya Simbas ya Kombe la Afrika (2018):

Juni 23 – Morocco vs. Kenya (ugenini)

Juni 30 – Kenya vs. Zimbabwe (nyumbani)

Julai 7 – Kenya vs. Uganda (nyumbani)

Agosti 11 – Kenya vs. Tunisia (nyumbani)

Agosti 18 – Namibia vs. Kenya (ugenini)

Shujaa kumenyana na Tonga Kombe la Dunia

Na GEOFFREY ANENE

DROO ya Kombe la Dunia ya raga ya wachezaji saba kila upande imefanywa, huku Shujaa ya Kenya ikikutanishwa na kisiwa cha Tonga katika mechi yake ya ufunguzi mnamo Julai 20, 2018 mjini San Francisco, Marekani.

Vijana wa kocha Innocent Simiyu hawakupata tiketi ya moja kwa moja ya raundi ya 16-bora baada ya kumaliza katika nafasi ya tisa katika orodha ya matokeo ya Raga ya Dunia ya msimu 2016-2017 na 2017-2018 hapo Aprili 11.

Mshindi kati ya Kenya na Tonga atakutana na Scotland katika raundi ya 16-bora.

Afrika Kusini, Fiji, New Zealand, Uingereza, Marekani, Australia, Argentina na Scotland zilipata tiketi za bwerere kushiriki mechi za raundi ya 16-bora baada ya kumaliza misimu hiyo miwili ya Raga ya Dunia (hadi duru ya Hong Kong Sevens mwaka 2018) katika nafasi nane za kwanza, mtawalia.

Mshindi kati ya Canada na Jamaica atalimana na Argentina, Australia inasubiri mshindi kati ya Ufaransa na Papua New Guinea, nazo Wales na Zimbabwe zitapigania tiketi ya kukutana na Marekani.

Atakayeibuka mshindi kati ya Samoa na Hong Kong atavaana na Uingereza, nayo New Zealand itapambana na mshindi kati ya Urusi na Uganda, ambayo inanolewa na Mkenya Tolbert Onyango.

Japan na Uruguay zitapigania tiketi ya kumenyana na Fiji nayo Jamhuri ya Ireland itakabana koo na Chile kupata tiketi ya kushindania nafasi ya kuingia robo-fainali dhidi ya Afrika Kusini.

Kenya ilifika nusu-fainali ya makala mawili yaliyopita. Ilimaliza katika nafasi ya tatu mwaka 2009 nchini Urusi nyuma ya mabingwa Wales na nambari mbili Argentina. Shujaa ilikamilisha makala ya mwaka 2013 katika nafasi ya nne nyuma ya New Zealand, Uingereza na Fiji zilizomaliza katika nafasi tatu za kwanza, mtawalia.

Harambee Stars: Kutoka 105 hadi 113 FIFA

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars ya Kenya imeporomoka nafasi nane kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Ijumaa.

Baada ya kulipuliwa 3-2 na Jamhuri ya Afrika ya Kati na kukabwa 1-1 na Comoro mwezi Machi, Kenya imetupwa kutoka nafasi ya 105 hadi 113.

Jamhuri ya Afrika ya Kati imepaa nafasi sita hadi nambari 115 nayo Comoro imeshuka nafasi tisa hadi 141.

Wapinzani wa Kenya katika mashindano ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019, Ghana wamepaa nafasi tatu hadi nambari 51 duniani nao Sierra Leone na Ethiopia wakateremka kutoka 98 hadi 102 na 137 hadi 145, mtawalia.

Uganda inaongoza katika eneo la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) katika nafasi ya 74 duniani baada ya kuimarika nafasi nne. Kenya ni ya pili katika Cecafa.

Inafuatwa na Rwanda (nafasi ya 123 duniani baada ya kushuka nafasi 13), Sudan (nafasi ya 126 duniani baada ya kuteremka nafasi tisa), Tanzania (imeruka juu nafasi tisa hadi 137 duniani), Ethiopia, Burundi (imeshuka nafasi tatau hadi 145 duniani), Sudan Kusini iko chini nafasi moja hadi nambari 155 nayo Djibouti inashikilia nafasi ya 198 baada ya kuporomoka nafasi 11.

Eritrea na Somalia zinavuta mkia katika nafasi ya 207 baada ya kushuka nafasi moja.

Tunisia inasalia nambari moja barani Afrika baada ya kupaa nafasi tisa hadi 14 duniani. Inafuatiwa na Senegal (chini nafasi moja hadi nambari 28 duniani), DR Congo (iko juu nafasi moja hadi 38 duniani), Morocco imesalia nafasi ya 42, Misri imeteremka nafasi mbili hadi nambari 46, Nigeria imeimarika nafasi tano hadi nambari 47 nayo Cameroon iko katika nafasi moja na Ghana baada ya kusalia nambari 51 duniani.

Kuna mabadiliko makubwa katika mduara wa timu 10-bora duniani. Ujerumani na Brazil zinasalia katika nafasi mbili za kwanza, mtawalia. Ubelgiji iko juu nafasi mbili hadi nambari tatu. reno na Argentina zimeshuka nafasi moja kila mmoja hadi nafasi za nne na tano nazo Uswizi na Ufaransa zimepaa nafasi mbili hadi nambari sita na saba, mtawalia.

Uhispania imeteremka nafasi mbili hadi nambari nane, Chile iko juu nafasi moja hadi nambari tisa nayo Poland, ambayo ililimwa 1-0 na Nigeria mnamo Machi 23, inafunga 10-bora baada ya kuteremka nafasi nne.

De Bruyne akiri mpinzani Salah ni moto wa kuotea mbali

Na AFP

KIUNGO mahiri, Kevin De Bruyne wa Manchester City amekubali kwamba mpinzani wake mkuu kwa vita vya Mchezaji Bora wa Mwaka EPL, Mohamed Salah ni moto wa kuotea mbali.

Habari zaidi zimesema kwamba Mbelgiji huyo amempigia kura Salah kumtaka ashinde tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Salah ameibukia kuwa mkali kutokana na ubora wake katika mechi za EPL na michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

De Bruyne amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo kutokana na mchango wake katika kikosi cha Pep Guardiola kuelekea ushindi wa ligi ya EPL.

Lakini Salah aliyetwaliwa na Liverpool akitokea AS Roma ameonekana kuwa tishio baada ya kufunga mabao 29, hata baada ya kutokuwa kikosini mwishoni mwa wiki dhidi ya Everton.

Nyota mwingine aliye kwenye vita vya kuwania tuzo hiyo ni Harry Kane wa Tottenham.

 

GOLD COAST AUSTRALIA: Ni shaba tu kwa bondia Christine

Na CHRIS ADUNGO

BONDIA Christine Ongare aliwaepushia wanamasumbwi wa Kenya aibu ya kuambulia pakavu kabisa katika ulingo wa ndondi baada ya kumdengua Jumatano Dulani Jayasinghe wa Sri-Lanka katika ukumbi wa Oxenford Studios.

Ongare ambaye kwa sasa ana uhakika wa kutia kapuni angalau nishani ya shaba, anataingia katika nusu-fainali ya pili mnamo Ijumaa adhuhuri dhidi ya Carly McNaul wa Ireland Kaskazini.

Licha ya kukabiliwa na presha ya kufanya vyema katika fani hiyo baada ya wawakilishi wengine 10 wa Kenya kubanduliwa mapema, Ongare alimzidi maarifa Jayasinghe kwenye robo-fainali ya kitengo cha uzani wa kilo 51.

Refa  Valeri Pastuhov kutoka Jamhuri ya Moldova alilazimika kusitisha mapema mchuano huo baada ya Ongare kumwelekezea Jayasinghe makonde yaliyomlemea mapema.

Elizabeth Andiego wa Kenya na mwenzake Lorna Simbi walibanduliwa na Millicent Agboegbulem (Nigeria) Marie-Jeanne Parent wa Canada mtawalia.

GOLD COAST AUSTRALIA: Unyonge wa Wakenya mbio za masafa mafupi

Na CHRIS ADUNGO

NDOTO za Kenya za kutia fora katika mbio za masafa mafupi kwenye makala ya 21 ya Michezo ya Jumuiya ya Madola zilizimika kabisa hapo Jumatano baada ya wanariadha waliokuwa wakipeperusha bendera ya taifa hili kutotamba katika fani hizo.

Mark Otieno Odhiambo na Millicent Ndoro walibanduliwa kwenye nusu-fainali za mbio za mita 200 kwa upande wa wanaume na wanawake mtawalia huku Maximila Imali akikamilisha mbio za mita 400 kwa muda wa sekunde 51.32 uliomweka katika nafasi ya tano nyuma ya Christine Botlogetswe wa Botswana (sekunde 51.17).

Mtimkaji Stephenie Mcpherson wa Jamaica aliridhika na nishani ya shaba katika mbio hizo baada ya kuambulia nafasi ya tatu kwa muda wa sekunde 50.93 nyuma ya mwenzake wa Jamaica, Anastasia Le-Roy aliyejinyakulia medali na fedha kwa kufikia ukingo baada ya sekunde 50.57.

Nyota wa Botswana, Amantle Montsho, ndiye aliyejizolea nishani ya dhahabu baada ya kuzitawala mbio hizo kwa sekunde 50.15. Mgongo wa Imali alifuzu kwa fainali ya jana baada ya kutawala kundi la pili kwenye nusu-fainali ya mbio hizo kwa sekunde 51.52, mbele ya mwanariadha mzawa wa Nigeria, Yinka Ajayi aliyevuta mkia katika fainali ya jana (52.26).

Ajayi alisalia kusoma migongo ya Anneliese Rubie (sekunde 52.03, Australia) na Hima Das (sekunde 51.32, India).

GOLD COAST AUSTRALIA: Wanaotegemewa na Kenya mita 800 kwa wanawake

Na CHRIS ADUNGO

WANARIADHA Margaret Nyairera Wambui, Eglay Nalyanya na Emily Cherotich Tuwei wanatazamiwa Alhamisi kufuzu kwa fainali za mbio za mita 800 kwa upande wa wanawake na kuiweka Kenya katika nafasi nzuri ya kujizolea nishani tatu kwa mpigo zitakazoipaisha kwenye msimamo wa jedwali la Michezo ya Jumuiya ya Madola nchini Australia. 

Nalyanya atakuwa wa kwanza kushuka uwanjani kuwania tiketi ya fainali kwa matarajio ya kumpiku bingwa wa Afrika Kusini, Caster Semenya aliyejizolea dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanawake mnamo Jumanne baada ya kumzidi maarifa Mkenya Beatrice Chepkoech.

Semenya aliyeweka rekodi mpya kitaifa na kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa kukata utepe baada ya dakika 4:00.71 katika mbio za Jumanne anapigiwa upatu kuitawala pia fani ya mita 800.

Ingawa hivyo, huenda akatolewa kijasho na Docus Ajok wa Uganda, Natalia Evangelidou (Cyprus), Keely Small (Australia), Angela Petty (New Zealand) na Mwingireza Alexandra Bell.

Wapinzani wengine watakaopeperusha bendera za mataifa yao katika Kundi la kwanza la mchujo ni Gayanthika Artigala Aberathna wa Sri-Lanka na Mariama Conteh wa Slovenia.

Kundi la pili linalomjumuisha Nyairera ndilo linalotazamiwa kutawaliwa na ushindani mkali zaidi kutoka kwa Natoya Goule wa Jamaica, Shelayna Oskan-Clarke (Uingereza) na Mganda Halima Nakaayi.

Wengine watakaonogesha kampeni za kufuzu kutoka Kundi hilo ni Tsepang Sello (Lesotho), Brittany Mcgowan (Australia), Agnes Abu (Ghana) na Ciara Mageean wa Ireland Kaskazini.

Tuwei anapigiwa upatu wa kutawala Kundi la tatu la mchujo ambalo litawashirikisha Lynsey Sharp wa Scotland, Georgia Griffith (Australia), Alice Ishimwe (Rwanda), Nimali  Arachchige (Sri-Lanka), Winnie Nanyondo (Uganda) na Mwingereza Adelle Tracey

GOLD COAST AUSTRALIA: Kibarua kizito kumbwaga Nijel Amos mita 800

Na CHRIS ADUNGO

KIBARUA kizito kitakachowasubiri Alhamisi alasiri Wakenya Jonathan Kitilit na Wycliffe Kinyamal nchini Australia ni jinsi ya kusuka njama itakayofaulu kuyazima makali ya mtimkaji mahiri wa Botswana, Nijel Amos katika fainali ya mbio za mita 800 kwa upande wa wanaume.

Amos, 24, aliwahi kumnyamazisha David ‘The King’ Rudisha ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 800 kwa kuitawala fani hiyo kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyoandaliwa jijini Glasgow, Scotland mnamo 2014.

Amos aliishindia Botswana medali ya kwanza katika Michezo ya Olimpiki kwa kujizolea nishani ya fedha katika Olimpiki za 2012 zilizondaliwa jijini London, Uingereza alishikilia uongozi wa Kundi la pili kwenye mchujo wa mbio hizo mnamo Jumanne kwa kusajili muda wa dakika 1:45.12.

Kitilit alifuzu kwa fainali ya leo baada ya kutawala Kundi la kwanza la mchujo wa nusu-fainali kwa muda wa dakika 1:47.27 mbele ya Jake Wightman wa Scotland aliyeambulia nafasi ya pili kwa muda wa 1:47.43.

Kinyamal aliongoza mchujo wa Kundi la tatu la nusu-fainali kwa muda wa dakika 1:45.56 mbele ya Mwingereza Kyle Langford ambaye pia alifuzu baada ya kuibuka wa pili kwa muda wa dakika 1:45.61.

Mtimkaji Cornelius Tuwei alikosa tiketi ya fainali na hivyo kukatiza ndoto za Kenya za kunyakua angalau nishani tatu kwenye mbio hizo za mita 800 baada ya kuzidiwa maarifa na wapinzani wake kwenye mchujo wa nusu-fainali.

Tuwei alimaliza wa tatu kwa muda wa dakika 1:47.10 nyuma ya Luke Mathews aliyesajili muda wa dakika 1:46.53.

GOLD COAST AUSTRALIA: Kenya kuzidi kusaka dhahabu

Na CHRIS ADUNGO

NISHANI ya dhahabu ilizidi kuwa telezi hapo Jumatano kwa kikosi cha riadha kinachopeperusha bendera ya Kenya katika makala ya 21 ya Michezo ya Jumuiya ya Madola inayoendelea jijini Gold Coast, Australia.

Hii ni baada ya Wakenya Fancy Cherono, Purity Cherotich Kirui na Celliphine Chepteek Chespol kuzidiwa maarifa na mtimkaji mzawa wa Jamaica, Aisha Praught, aliyetawala fainali ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

Chespol aliridhika na nishani ya fedha baada ya kukamilisha mbio hizo kwa muda wa dakika 9:22.61 nyuma ya Praught aliyejizolea dhahabu kwa kukata utepe mwishoni mwa dakika 9:21.00.

Kirui aliambulia medali ya shaba baada ya kusajili muda wa dakika 9:25.74 na kumpiku mwanariadha mzawa wa Uingereza, Rosie Clarke aliyemaliza katika nafasi ya nne kwa muda wa dakika 9:36.29.

Licha ya kusajili muda bora na wa kasi zaidi katika kampeni za msimu huu (9:46.27), Cherono aliambulia nafasi ya sita nyuma ya mwanaridha mzawa wa Australia, Genevieve Lacaze aliyefunga orodha ya tano-bora wa muda wa dakika 9:42.69.

Lennie Waite wa Scotland alivuta mkia wa fainali hiyo kwa muda wa dakika 10:21.72, nyuma ya Genevieve Lalonde (dakika 9:46.68, Canada), Iona Lake (dakika 9:58.92, Uingereza) na Victoria Mitchell (dakika 10:12.59, Australia).

Hadi kufikia sasa, Kenya imejizolea jumla ya medali sita baada ya kujitwalia nishani za shaba mnamo Jumapili iliyopita kupitia kwa mwanafunzi wa Kidato cha Nne, Edward Zakayo (mita 5,000) na Samuel Gathimba aliyetia fora katika matembezi ya kilomita 20.

Kipusa Stacy Ndiwa aliishindia Kenya nishani ya fedha mnamo Jumatatu katika mbio za mita 10,000 kwa upande wa wanawake zilizotawaliwa na mwanariadha wa Uganda, Stella Chesang’ aliyeandikisha muda wa dakika 31:45.30.

Watimkaji Sandrafelis Chebet na Beatrice Mutai waliotumainiwa kuzolea Kenya nishani nyinginezo katika mbio hizo za mita 10,000 waliambulia nafasi za nne na 10 kwa muda wa dakika 31:49.81 na 32:11.92 mtawalia.

Beatrice Chepkoech aliivunia Kenya medali ya pili ya fedha mnamo Jumanne baada ya  kumtoa kijasho bingwa wa Afrika Kusini, Caster Semenya aliyejizolea dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanawake.

Kenya ina fursa ya kujiongezea medali zaidi hii leo wakati Aron Kipchumba Koech na bingwa wa dunia Nicholas Kiplagat Bett watakaponogesha fainali ya mbio za mita 400 kuruka viunzi.

Isitoshe, Wakenya Jonathan Kitilit na Wycliffe Kinyamal watategemewa sana kunyakulia Kenya nishani muhimu katika fainali ya mbio za mita 800 kwa upande wa wanaume.

Wazito wageuzwa wepesi na Gor

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Jacques Tuyisenge aliwafungia Gor Mahia bao muhimu lililowachochea kuwabamiza limbukeni Wazito FC 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu ya KPL iliyowakutanisha jana ugani Kenyatta, Machakos.

Ingawa ushindi huo wa Gor Mahia uliwadumisha katika nafasi ya pili jedwalini kwa alama 22, wafalme hao mara 16 wa taji la KPL walipunguza pengo la alama kati yao na viongozi Mathare United hadi pointi moja.

Nafuu zaidi kwa kocha Dylan Kerr ni kwamba Mathare United ambao watavaana na Posta Rangers wikendi hii wametandaza jumla ya michuano 10, miwili zaidi kuliko Gor Mahia. Tuyisenge alitoka benchi katika kipindi cha pili na kuwapa Gor Mahia ushindi muhimu kunako dakika ya 74 baada ya kukamilisha kwa kichwa mkwaju wa ikabu.

Gor Mahia walitumia mchuano huo kama jukwaa mwafaka zaidi la kujinoa kwa mechi ya marudiano dhidi ya SuperSport ya Afrika Kusini kwenye Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup).

Ushindi wa Gor Mahia kwa sasa unawasaza Wazito katika nafasi ya 12 jedwalini kwa alama 11. Baada ya kuvaana na Chemelil Sugar mwishoni mwa wiki hii, Wazito wamepangiwa kuonana na Mathare, Tusker na Sofapaka kwa usanjari huo.

Kwingineko, kocha Ken Odhiambo wa Bandari aliwatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo hapo jana kuhusu hali ya mwanasoka wa timu ya taifa ya Harambee Stars U-23, Nicholas Meja kwa kusisitiza kwamba amepona jeraha.

Odhiambo alisema kuwa Meja anaendelea na mazoezi yuko katika kikosi kinachotarajiwa kuondoka kuelekea Bungoma kwa mechi dhidi ya Nzoia Sugar itakayopepetwa uwanjani Sudi hapo Jumapili.

Aidha, alifichua kuwa kikosi chake kitakosa huduma za straika mkongwe Shaaban Kenga ambaye alijitonesha kisigino wakati wa mechi iliyopita dhidi ya Ulinzi Stars ugani Mbaraki Sports Club.

Kwa wakati huu, Bandari inashikilia nafasi ya tano ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi tisa, kushinda nne, kutoka sare mara tatu na kupoteza mechi mbili. Mastraika wake wamefunga mabao tisa na kikosi kimefungwa mabao manne.

Wakati uo huo, kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo wa Posta Rangers amekiri kwamba kurejea kwa nyota Dennis Mukaisi ni afueni kubwa itakayowapiga jeki vijana wake watakaovaana na Mathare United mwishoni mwa wiki hii.

Mukaisi anatazamia kupangwa katika kikosi cha kwanza baada ya jeraha kumweka mkekani kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita. Mvamizi huyo wa zamani wa Tusker na Leopards aliwajibishwa kwa mara ya kwanza msimu huu katika mchuano wa wikendi jana uliowashuhudia Rangers wakibamizwa 1-0 na Zoo Kericho.

Rangers kwa sasa wanashikilia nafasi ya saba jedwalini kwa alama 14.

Buffon: Michael Oliver ana jaa la taka rohoni, alifaa kula vibanzi na mashabiki

Na CHRIS ADUNGO

KIPA wa Juventus Gianluigi Buffon alimkejeli kwa kila aina ya maneno mazito refarii Michael Oliver baada ya timu yake kuaga mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya mikononi mwa Real Madrid.

Juventus ilijitahidi na kufunga mabao matatu, hali iliyosawazisha mabao ya jumla na kuwa 3-3 baada ya Mario Mandzukic kufunga mabao mawili na moja la Blaise Matuidi.

Lakini robo fainali hiyo iliamuliwa katika muda wa ziada baada ya dakika 90 kukamilika ambapo Cristiano Ronaldo alifunga penalti, baada ya kipa huyo mwenye miaka 40 akilishwa kadi nyekundu kwa kupinga vikali uamuzi wa kuipa Real Madrid penalti.

“Refarii anayejua kazi yake hawezi kuharibu ndoto ya timu ambayo imejitolea kwa jino na ukucha kwa dakika 90,” alichemka alipohojiwa na wanahabari.

“Binadamu hewazi kupiga filimbi katika tukio lenye shaka kama hilo, anaweza tu ikiwa ana jaa la taka ndani ya roho yake. Ikiwa hauna heshima yako mwenyewe, unafaa kuketi kule kwa mashabiki na kula vibanzi ukiwa na familia yako. Refa wa mechi hii hakuwa ametimu kuichezesha katika ngazi hii.

“Ningemwambia refa huyo kila aina ya neno baya wakati huo, lakini alifaa kuelewa kiwango cha hatari aliyokuwa akileta. Ikiwa hauwezi kufanya uamuzi wa ujasiri, basi unafaa kujumuika na mashabiki na ule vibanzi.

“Ikiwa hauna sifa zifaazo katik viwango vya juu, ni bora kwako utazame mechi ukiwa na mkeo na watoto mkila vibanzi kwa viti vya mashabiki. Ni swali la uzito wa hali ambao kila mja anafaa kuwa nao, kujua utachezesha mechi au la. Inamaanisha kukosa kujua msimamo wako na timu zinazocheza. Kwa ufupi, inamaanisha hujui lolote,” cheche za maneno zikamtoka Buffon.

 

Juventus yakabiliana na Real Madrid baada ya penalti chungu

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya Juventus Jumatano usiku ililazimika kuaga kipute cha Klabu Bingwa Ulaya baada ya refa kuipa Real Madrid penalti katika muda wa ziada.

Juventus tayari ilikuwa ishafunga mabao matatu ugenini Santiago na kusawazisha matokeo ya jumla kuwa 3-3  huku uwezekano wa muda wa ziada wa dakika 30 ukiwepo.

Lakini Medhi Benatia wa Juventus alionekana kumwangusha Lucas Vazquez ndani ya kisanduku baada ya kupokea pasi kwa kichwa kutoka kwa Cristiano Ronaldo.

Refa wa Uingereza Michael Oliver alizungukwa na wachezaji wa Juventus huku akimpa kadi nyekundu kipa Gianluigi Buffon hata kabla ya penalti kupigwa.

Ronaldo aliutia mpira ndani ya neti na kuiwezesha Real Madrid kufika nusu fainali kwa ujumla wa mabao 4-3.

Matokeo hayo yaliwaletea uchungu mwingi wachezaji wa Juventus na mashabiki kote duniani.

Baada ya mechi wachezaji wa Juventus waliwakabili wenzao wa Real wakighadhabishwa na uamuzi wa kuwabandua kwa shindano hilo, lakini Sergio Ramos alikuwepo kujaribu kutuliza hali.

Haijulikani iwapo UEFA itamchukulia hatua Ramos kwa kujitokeza baada ya mechi, ikizingatiwa alikuwa ashpigwa marufuku katika mechi hiyo.