Fatma ataka klabu za akina dada zijiunge kushiriki ligi ya Kwale

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KLABU zinazotaka kushiriki kwenye Ligi ya FKF Kaunti ya Kwale zimepewa hadi Oktoba 15, 2021, kuthibitisha kushiriki ili zipangwe kwenye ratiba ya ligi hiyo inayotarajia kuanza rasmi hapo Oktoba 23, 2021.

Mwakilishi wa soka ya akina dada wa Shirikisho la Soka la Kaunti ya Kwale, Fatma Tuli amesema ni klabu tano pekee hadi sasa ndizo zimethibitisha kushiriki kwenye ligi ya kaunti hiyo na akatoa ombi kwa klabu nyingine zijitokeze na kuthibitisha kushiriki kwao.

Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu, Fatma amesema kuwa klabu tatu ambazo tayari zimeshathibitisha kushiriki katika ligi hiyo kutoka kaunti ndogo ya Msambweni ni Ukunda Queens, Barcelona na Ukunda Starlets.

Amesema klabu mbili za kaunti ndogo ya Lungalunga ambazo zimeshakubali kushiriki ni Lungalunga United Ladies FC na Dogo Dogo Ladies FC.

“Ninaamini klabu nyingi zaidi hasa kutoka kaunti nyingine ndogo za Kinango na Matuga zitajitokeza kushiriki,” akasema Fatma.

Fatma alisema mwisho wa kuthibitisha kushiriki kwenye ligi hiyo ni Oktoba 15 na siku itakayofuatia asubuhi kutafanyika mkutano hapo Kombani baina ya maafisa wa FKF Kwale na wawakilishi wa klabu za Msambweni na Matuga.

Siku hiyo hiyo ya Oktoba 16 saa nane mchana kutakuwa na mkutano wa klabu za Lungalunga na maafisa wa FKF Kwale utakaofanyika Kibaoni.

Mnamo Oktoba 17, 2021, kutakuwa na mkutano kama huo lakini na klabu za Kinango ambao utafanyika mjini Samburu.

Sutton athubutu kusema Salah anapiku Ronaldo na Messi katika orodha ya wanasoka bora zaidi duniani kwa sasa

Na MASHIRIKA

FOWADI wa zamani wa Blackburn Rovers, Chris Sutton, amekiri kwamba Mohamed Salah ndiye mchezaji bora zaidi duniani kwa sasa na kuibua mjadala kuhusu iwapo kweli sogora huyo wa Liverpool na timu ya taifa ya Misri anawapiku Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Kwa mujibu wa Alan Shearer ambaye ni mfumaji wa zamani wa Uingereza, bao la Salah dhidi ya Manchester City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Oktoba 3, 2021 ni mojawapo ya magoli bora zaidi kuwahi kushuhudiwa katika ulingo wa soka enzi hii.

Hadi kufikia sasa, Salah, 29, amefungia Liverpool mabao tisa kutokana na mechi tisa msimu huu.

“Katika kipindi hiki cha sasa, Salah ndiye mchezaji bora zaidi duniani. Mgongo wake unasomwa na Ronaldo kisha Messi,” akasema Sutton kwa kusisitiza kwamba itawachukua Kylian Mbappe na Neymar muda mrefu zaidi kabla ya kuanza kulinganishwa na watatu hao.

Baada ya kufunga bao lake la 100 katika EPL mnamo Septemba, Salah alifunga mojawapo ya magoli yake bora zaidi dhidi ya Manchester City katika sare ya 2-2 iliyosajiliwa na Liverpool dhidi ya mabingwa hao watetezi mnamo Oktoba 3, 2021 ugani Anfield.

“Kinachomweka Salah mbele ya Ronaldo na Messi ni uthabiti wake wa kipindi kirefu. Mchezo wake unatabariki na makali yake hayashuki ovyo. Ni mchezaji wa kutegemewa uwanjani na fursa nyingi anazozipata huishia kuzaa mabao,” akaeleza Sutton.

Mbali na kufunga mabao tisa hadi sasa, Salah ambaye ni mchezaji wa zamani wa Chelsea na AS Roma, pia amechangia mabao matatu kambini mwa Liverpool muhula huu.

Anajivunia wastani wa mabao 21 kila msimu katika kipindi cha mihula mitatu iliyopita katika kampeni za EPL na msimu wa 2017-18 ndio uliomshuhudia akifunga magoli mengi zaidi ligini (32).

“Si rahisi kwa mwanasoka yeyote kuendeleza uthabiti huo katika soka ya sasa ambayo ina ushindani mkali,” akaongeza Sutton katika kauli iliyoungwa mkono na beki Micah Richards aliyewahi kuchezea pamoja na Salah kambini mwa Fiorentina ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo 2015.

Kufikia sasa muhula huu, Neymar amefungia waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) bao moja pekee kutokana na mechi tisa za kampeni za Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1). Kwa upande wake, Messi amefungia miamba hao wa Ufaransa goli moja pekee la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Man-City.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Familia ya Glazer kuuza hisa 9.5 milioni za Man-United kwa Sh21.4 bilioni

Na MASHIRIKA

WAMILIKI wa Manchester United wametoa fursa kwa mashabiki wao kujinunulia hisa 9.5 milioni za thamani ya Sh21.4 bilioni.

Mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) walitaarifu Soko la Hisa la New York kuhusu mauzo ya hisa hizo kwa majina ya wakurugenzi wa klabu Kevin Glazer na Edward mnamo Oktoba 5, 2021.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hakuna mafao yoyote ambayo Man-United itapata kutokana na mauzo ya hisa hizo.

Man-United ilitoa tangazo hilo miezi mitano baada ya mechi yao ya EPL dhidi ya Liverpool kuahirishwa kutokana na vurugu na fujo za waliokuwa wakilalamikia maamuzi ya vinara kuingiza kikosi kwenye kipute kipya cha European Super League (ESL). Joel Glazer ambaye ni mmoja kati ya wenyeviti wa Man-United alihusika pakubwa katika mchakato wa kujumuisha kikosi chake kwenye ESL.

Mnamo Machi 2021, Avram Glazer aliuza hisa nyingine za thamani ya Sh10.9 bilioni katika kikosi cha Man-United. Jumla ya hisa zote ambazo sasa zinauzwa na Man-United ni asilimia nane pekee ya zile zinazomilikiwa na familia ya Glazer ambayo kwa sasa imesalia na asilimia 69 ya hisa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Vipusa wa Barcelona wapokeza Arsenal kichapo cha kwanza tangu Februari 2021

Na MASHIRIKA

ARSENAL walipoteza mechi kwa mara ya kwanza tangu Februari 2021 baada ya mchezaji wao wa zamani, Asisat Oshoala kuongoza Barcelona kuwatandika 4-1 katika mchuano kufungua kampeni za Kundi C kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Barcelona waliwekwa kifua mbele na Mariona Caldentey aliyekamilisha krosi ya Oshoala katika dakika ya 31 kabla ya Alexia Putellas kufunga bao la pili kunako dakika ya 42 baada ya kushirikiana tena na Oshoala ambaye ni raia wa Nigeria.

Oshoala mwenyewe alipachika wavuni goli la tatu mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kuandaliwa pasi nzuri na Mariona.

Ingawa Frida Maanum alipania kurejesha Arsenal mchezoni katika dakika ya 74, chombo chao kilizamishwa kabisa na Lieke Martens aliyefungia Barcelona bao la nne kunako dakika ya 84.

Putellas angalifanya mambo kuwa 5-1 mwishoni mwa kipindi cha pili lakini penalti yake ikapanguliwa na kipa Manuela Zinsberger.

Oshoala, 26, alichezea Arsenal kuanzia Machi 2016 hadi Februari 2017 na kuwasaidia kunyanyua Kombe la FA. Hivyo, hakusherehekea bao alilowafunga waajiri wake hao wa zamani mnamo Jumanne usiku uwanjani Johan Cruyff.

Iliwachukua Arsenal dakika 55 kabla ya kuelekeza kombora langoni mwa Barcelona japo fataki hiyo kutoka kwa Vivianne Miedema ikadhibitiwa vilivyo na kipa Sandra Panos. Mbali na Miedema, mchezaji mwingine wa Barcelona aliyemtatiza Sandra ni Nikita Parris.

Chini ya kocha Jonas Eidevall, Arsenal walishuka dimbani kwa ajili ya mchuano huo wakipigiwa upatu wa kusajili matokeo bora ikizingatiwa ubora wa fomu yao katika mechi za awali ambapo walishinda mechi nane kutokana na michuano minane ya mashindano yote.

Arsenal waliokuwa wamefunga wastani wa mabao matatu katika kila mchuano kabla ya kuvaana na Barcelona, walipigwa kwa mara ya mwisho mnamo Februari 2021 na hawakuwa wamepigwa kutokana na mechi 20.

Vipusa wa Arsenal watakuwa wenyeji wa Hoffenheim ya Ujerumani katika mchuano wao ujao kundini mnamo Oktoba 14, 2021 huku Barcelona wakitua Denmark kumenyana na Koge. Hoffenheim walitandika Koge 5-0 katika mchuano mwingine wa Kundi C mnamo Oktoba 5, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Serge Aurier ajiunga na Villarreal ya Uhispania

Na MASHIRIKA

BEKI wa zamani wa Tottenham Hotspur, Serge Aurier, amejiunga na kikosi cha Villarreal kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Beki huyo raia wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 28, alikuwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Spurs kutamatika mwishoni mwa Agosti 2021.

Chini ya kocha Unai Emery, Villarreal ambao ni washikilizi wa taji la Europa League, watakuwa huru kurefusha kandarasi ya Aurier kwa miaka miwili zaidi mwishoni mwa msimu huu wa 2021-22. Hivyo, upo uwezekano mkubwa kwamba beki huyo wa kulia atuhudumu kambini mwa Villarreal hadi mwaka wa 2024.

Aurier alichezea Spurs kwa kipindi cha miaka minne baada ya kusajiliwa kutoka Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwa Sh3.6 bilioni mnamo Agosti 2017.

Kufikia sasa, Villarreal wanashikilia nafasi ya 11 kwenye msimamo wa jedwali la La Liga baada ya kujizolea alama 11 kutokana na mechi saba za ufunguzi wa kampeni za muhula huu. Japo walijituma vilivyo dhidi ya Manchester United kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Septemba 29, 2021, walipokezwa kichapo cha 2-1 katika mchuano huo wa mkondo wa kwanza uwanjani Old Trafford.

Aurier ataingia kambini mwa waajiri wake wapya baada ya kukamilika kwa mechi mbili zijazo za kimataifa zitakazokutanisha Ivory Coast na Malawi nyumbani na ugenini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Nilimtusi Neymar, lakini si kwa ubaya – Mbappe

Na MASHIRIKA

KYLIAN Mbappe amekiri kwamba aliwahi kumtusi mwanasoka mwenzake kambini mwa Paris Saint-Germain (PSG), Neymar Jr.

Akihojiwa na kituo cha RMC Sport mnamo Oktoba 4, 2021 nchini Ufaransa, Mbappe, 22, aliungama kumfananisha Neymar na makalio. “Nilimtusi. Naam, nilimfananisha na makalio kwa kuwa hakutaka kunipa mpira uwanjani hata wakati nilipokuwa katika nafasi nzuri ya kufunga,” akasema.

Mechi iliyokuwa ikirejelewa na Mbappe ni ile ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) iliyokutanisha waajiri wake PSG na Montpellier mnamo Septemba 2021.

PSG walishinda mechi hiyo ya Ligue 1 dhidi ya Montpellier 2-0 na kupata motisha ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Manchester City katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Baada ya kutambua baadaye jinsi matusi hayo yalivyosambazwa mitandaoni, ilinilazimu kumzungumzia Neymar kuhusiana na kauli niliyotoa kumhusu,” akasema Mbappe kwa kukiri kwamba kuvurugika kwa uhusiano wake pia na Olivier kambini mwa Ufaransa huenda kukamchochea kuacha kuchezea timu hiyo ya taifa kwa muda.

“Tumebadilishana matusi mengi uwanjani. Ni kawaida kwa wanasoka kufanya hivyo kwa sababu ya mapenzi kwa timu na kiu ya kutaka kushinda mechi husika. Matusi mengine huchochewa na hasira ya kuona tunavyoelekea kupoteza mechi ambayo vinginevyo tungeshinda iwapo mwenzangu angenipa pasi ya kufunga bao,” akaeleza Mbappe.

“Hata hivyo, haina maana kwamba namdhalilisha Neymar kwa kumtusi. Namheshimu sana na ninamstahi kutokana na mafanikio yake kitaaluma,” akaongeza Mbappe.

“Nimekuwa katika ulingo wa soka kwa muda kiasi cha kufahamu kwamba ukweli wa jana haubadiliki kuwa uongo leo au hata kesho.”

“Iwapo ningeambiwa na mtu kwamba Lionel Messi angewahi kuja kuwa mwanasoka wa PSG, basi nisingeamini kabisa. Hivyo ukweli ni kwamba hakuna mchezaji ajuaye mustakabali wake kitaaluma. Mambo hutokea na mabadiliko hudumu,” akasema Mbappe.

“Kwa sasa mustakabali wangu si jambo ninalolipa kipaumbele. Tayari nimepoteza nguvu na muda mwingi wa kujibu tetesi za kila sampuli muhula huu. Hali hiyo ya kuandamwa mara kwa mara na maswali inachosha na kuchusha,” akaongeza sogora huyo anayehemewa pakubwa na Real Madrid.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Harambee Stars yawasili Morocco kuvaana na Mali inayoandamwa na majeraha

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Harambee Stars imewasili nchini Morocco huku wenyeji Mali wakisemekana huenda wakakosa huduma za wachezaji wanne timu hizi zitakapokabiliana ugani Agadir nchini Morocco hapo Oktoba 7.

Stars ya kocha Engin Firat iliondoka jijini Nairobi mnamo Jumatatu usiku na kuwasili Morocco mnamo Jumanne alasiri.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Mali, Cheick Doucoure (Lens, Ufaransa), Lassana Coulibaly (Salernitana, Italia) na Yves Bissouma (Brighton, Uingereza), wameumia.

Kiungo Doucoure aliumia kifundo dhidi ya Reims mnamo Oktoba 1. “Lens imethibitisha kujiondoa kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Mali,” gazeti la L’Essor lilisema Oktoba 5.

Coulibaly, ambaye pia ni kiungo, alijeruhiwa katika kipindi cha kwanza cha mechi ya Ligi Kuu nchini Italia dhidi ya Genoa mnamo Oktoba 2. “Alifanyiwa uchunguzi wa jeraha hilo hapo Oktoba 4 ambao ulifichua kuwa alichanika misuli. Kwa hivyo, kuna hofu kuwa huenda akakosa mechi zote mbili dhidi ya Kenya,” gazeti hilo liliongeza.

Kiungo Bissouma hajachezea Brighton tangu Septemba 19 alipoumia dhidi ya Leicester. “Kwa sasa, habari si nzuri kambini mwa Mali kwa sababu ya majeraha. Ilitarajiwa kuwa majeruhi hao watakuwa wamepona kabla ya mechi za kufa-kupona dhidi ya Kenya.”

Gazeti hilo linasema kuwa timu ya Mali maarufu kama Eagles ilianza kukusanyika jijini Agadir mnamo Oktoba 4 ilipokaribisha makipa Djigui Diarra (Young Africans, Tanzania) na Mohamed Niare (Stade Malien), kiungo Alou Dieng (Al Ahly, Misri) na mshambuliaji wa kati Adama Traore “Malouda” (Sheriff, Moldova).

Katika mechi hiyo ya Kundi E ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022, kocha Mturuki Firat atawategemea wachezaji kama mshambuliaji Michael Olunga (Al Duhail, Qatar), kiungo Kenneth Muguna (Azam, Tanzania) na beki Joash Onyango (Simba SC, Tanzania).

Naye kocha Mohamed Magassouba atawategemea Hamari Traore (Rennes, Ufaransa), Falaye Sacko (Vitoria Guimaraes, Ureno), Diadie Samassekou (Hoffenheim, Ujerumani).

Mshambuliaji wa Mali, Kevin Lucien Zohi anayecheza nchini Ureno pia huenda akakosa mechi dhidi ya Kenya, lakini kutokana na stakabadhi za usafiri. Mali imekalia juu ya jedwali kwa alama nne ikifuatiwa na Kenya na Uganda (mbili kila moja) nayo Rwanda ni ya mwisho kwa alama moja.

Watford waajiri kocha Claudio Ranieri kujaza pengo la Xisco Munoz

Na MASHIRIKA

WATFORD wamemteua kocha mzoefu raia wa Italia, Claudio Ranieri, kuwa mrithi wa Xisco Munoz aliyetimuliwa uwanjani Vicarage Road mnamo Oktoba 3, 2021 baada ya kuhudumu kambini mwa kikosi hicho kwa kipindi cha miezi 10 pekee.

Chini ya Munoz ambaye ni raia wa Uhispania, Watford walirejea katika EPL mwishoni mwa msimu wa 2020-21 baada ya kutamalaki kampeni za Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship).

Hadi kutimuliwa kwake, Munoz alikuwa ameongoza Watford kujizolea alama saba kutokana na mechi saba za EPL msimu huu. Matokeo hayo yalikuwa yamewaweka Watford katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa jedwali.

Familia ya Pozzo ambayo inamiliki Watford, inabadilisha kocha wa kikosi hicho kwa mara ya 14 tangu 2012.

Kuajiriwa kwa Ranieri aliyeagana na Sampdoria ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mwishoni mwa msimu wa 2020-21, kutamshuhudia akirejea EPL baada ya kuongoza Leicester kunyanyua ufalme wa kipute hicho mnamo 2015-16.

Kibarua chake cha kwanza akidhibiti mikoba ya Watford ni mechi ya EPL itakayowakutanisha na Liverpool uwanjani Vicarage Road mnamo Oktoba 16, 2021.

Ranieri anajivunia tajriba pevu na uzoefu mpana katika ulingo wa ukufunzi na Watford itakuwa klabu yake ya 21 kusimamia katika kipindi cha miaka 35 iliyopita ya ukocha. Katika kipindi hicho, amenyanyua mataji manane, likiwemo Kombe la Italian Cup alilolitwaa mnamo 1998-1998 akiwanoa Fiorentina pamoja na ufalme wa Super Cup alioutia kapuni mnamo 2004-05 akidhibiti mikoba ya Valencia.

Ranieri ambaye ameajiriwa kwa mkataba wa miaka miwili na Watford, amewahi pia kuwa kocha wa Chelsea na Fulham.

Ingawa anastahiwa pakubwa kambini mwa Leicester, kikosi hicho kilimfuta kazi mnamo 2017 baada ya msururu wa matokeo duni yaliyosaza klabu hiyo na alama moja pekee juu ya mduara wa vikosi vitatu vya mwisho zikisalia mechi 13 pekee kwa msimu wa 2016-17 kutamatika.

Baada ya kutimuliwa na Leicester, alitua kambini mwa Nantes katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kabla ya kurejea EPL kudhibiti mikoba ya Fulham mnamo 2018. Hata hivyo, alihudumu kambini mwa Fulham kwa siku 106 pekee kabla ya kikosi hicho kumpiga kalamu kikiwa katika hatari ya kushuka ngazi kwenye EPL.

Munoz aliyefurushwa na Watford baada ya kikosi chake kupigwa 1-0 na Leeds United mnamo Oktoba 2, 2021, ndiye kocha wa kwanza wa EPL kupigwa kalamu msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Niliwaomba PSG waniachilie ili niyoyomee Real Madrid – Kylian Mbappe

Na MASHIRIKA

FOWADI matata raia wa Ufaransa, Kylian Mbappe, amekiri kwamba aliwasilisha ombi la kuagana na Paris Saint-Germain (PSG) mwishoni mwa msimu uliopita wa 2020-21 baada ya Real Madrid kufichua azma ya kuwania huduma zake.

Ingawa hivyo, ameshikilia kwamba anafurahia maisha yake jijini Paris na kubwa zaidi katika maazimio yake kwa sasa ni kumakinikia majukumu yake kambini mwa PSG.

Ofa mbili za Sh21 bilioni na Sh23 bilioni zilizotolewa na Real kwa ajili ya maarifa ya Mbappe, 22, mnamo Julai na Agosti 2021 zilikataliwa na PSG.

Katika mahojiano yake na wanahabari wa RMC Sport nchini Ufaransa mnamo Oktoba 4, 2021, Mbappe alifichua kwamba alipania sana kuondoka uwanjani Parc des Princes kabla ya kampeni za muhula huu kuanza ili kuepuka hali ambapo angeagana na PSG bila ada yoyote baada ya mkataba wake wa sasa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2022-23.

“Nilitaka PSG waniuze ili wapate pesa nzuri za kutafuta mrithi wangu pale kambini. Msimamo wangu ulikuwa wazi na wa kweli. Nilitaka kuondoka,” akatanguliza.

“Sikufurahia madai ya PSG kwamba niliwapa taarifa za kutaka kukatiza uhusiano nao mwishoni mwa Agosti. Niliwasilisha ombi langu kwao mapema Julai.”

“Niliwapa habari hizo mapema sana ili wawe na muda wa kutosha kujipanga. Matamanio yangu yalikuwa ni kuondoka PSG kwa uzuri kwa sababu naamini bado tungehitajiana katika siku za usoni,” akaongeza Mbappe.

Nyota huyo aliyesaidia Ufaransa kunyakua ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, anajivunia kufungia PSG jumla ya mabao 136 kutokana na mechi 182 tangu ajiunge nao kutoka AS Monaco mnamo Agosti 2017.

“Naheshimu maamuzi ya PSG kutonitia mnadani. Hiki ni kikosi ambacho kimekuwa na mchango mkubwa katika makuzi yangu kitaaluma. Nimefurahia sana kipindi cha miaka minne ambapo nimekuwa hapa, na bado naona fahari tele.”

“Niliwaambia PSG kwamba nilikuwa tayari kusalia kambini mwao na kuwachezea kwa kujitolea iwapo hawakuwa radhi kuniachilia kutafuta hifadhi mpya kwingineko,” akaongeza.

Kusalia kwa Mbappe kambini mwa PSG kunafanya kikosi hicho kujivunia maarifa ya mafowadi mahiri zaidi duniani wakiwemo Neymar Jr na Lionel Messi aliyejiunga nao mnamo Agosti 2021 baada ya kuagana ghafla na Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Leeds United wakung’uta Watford na kusajili ushindi wao wa kwanza ligini msimu huu

Na MASHIRIKA

LEEDS United walisajili ushindi wao wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kuwacharaza Watford 1-0 mnamo Jumamosi uwanjani Elland Road.

Bao la pekee na la ushindi katika mechi hiyo lilipachikwa wavuni na beki Diego Llorente aliyekuwa akirejea ulingoni baada ya kupona jeraha. Llorente aliyejeruhiwa paja wakati wa mechi ya awali dhidi ya Liverpool, alichuma nafuu kutokana na masihara ya mabeki wa Watford na kujaza kimiani mpira uliombabatiza Juraj Kucka.

Ingawa Watford walifunga bao katika kipindi cha pili, goli hilo halikuhesabiwa na refa kwa madai kwamba lilifumwa wavuni wakati ambapo kipa Illan Meslier alikuwa amechezewa vibaya.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Leeds United kuondoka uwanjani Elland Road wakijivunia alama tatu kwenye kampeni za muhula huu. Stuart Dallas alipata nafasi nyingi za kufunga mabao ila juhudi zake zikazimwa na kipa wa Watford, Ben Foster ambaye pia aliwajibishwa mara kadhaa na fowadi wa zamani wa Manchester United, Daniel James.

Leeds United kwa sasa wanashikilia nafasi ya 16 jedwalini kwa alama sita sawa na Crystal Palace. Watford kwa upande wao wanakamata nafasi ya 14 kwa alama saba sawa na Leicester City ya kocha Brendan Rodgers.

Mshindi wa zamani wa taji la Ballon d’Or, Hegerberg, arejea ulingoni baada ya jeraha kumweka nje kwa miezi 20

Na MASHIRIKA

MSHINDI wa zamani wa taji la Ballon d’Or, Ada Hegerberg wa Olympique Lyon, amesema hatawahi kuchukulia soka kama suala la kimzaha baada ya kupona jeraha lililomweka mkekani kwa kipindi cha miezi 20 iliyopita.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amejumuishwa katika kikosi kinachojiandaa kuvaana na BK Hacken ya Uswidi kwenye mechi ya makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba 5, 2021.

Hegerberg ambaye ni raia wa Norway, hajatandaza soka katika mchuano wowote tangu Januari 2020 baada ya kupata jeraha baya la misuli ya mguu.

“Nimekomaa vilivyo kama mwanamke na mwanasoka. Nimejifunza mengi ambayo yananipa nguvu ya kujituma ipasavyo kwa kipindi cha miaka kadhaa ijayo kitaaluma,” akasema Hegerberg.

Sogora huyo alitawazwa malkia wa Ballon d’Or katika makala ya kwanza ya tuzo hiyo kwa wanawake mnamo 2018.

Hegerberg alisaidia Lyon kunyanyua mataji manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara nne mfululizo. Lyon ambao ni miamba wa soka nchini Ufaransa walitia kapuni taji jingine la UEFA mnamo 2019-20 baada ya Hegerberg kupata jeraha.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Liverpool, Manchester City nguvu sawa ligini

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester City pamoja na Liverpool walitarajia kudengua Chelsea kudengua Chelsea kileleni mwa jedwali waliposhuka dimbani kupimana ubabe uwanjani Anfield mnamo Jumapili.

Hata hivyo, sare iliyosajiliwa na vikosi hivyo ilidumisha masogora wa kocha Thomas Tuchel kileleni mwa jedwali la EPL.

Man-City walitamalaki kipindi cha kwanza cha mchezo ila wakapoteza nafasi nyingi za wazi. Waliadhibiwa baadaye na Sadio Mane aliyeshirikiana vilivyo na Mohamed Salah katika dakika ya 59.

Hata hivyo, uongozi wa Liverpool ulidumu kwa dakika 10 pekee kabla ya Phil Foden kumzidi ujanja James Milner na kukamilisha krosi ya Gabriel Jesus.

Salah alifungia Liverpool bao la pili katika dakika ya 76 kabla ya kombora lililovurumishwa na Kevin De Bruyne katika dakika ya 81 kumbabatiza beki Joel Matip na kujaa ndani ya lango lililokuwa chini ya ulinzi wa Alisson Becker.

Kufikia sasa, Liverpool ya kocha Jurgen Klopp inajivunia alama 15, moja pekee kuliko Chelsea ambao wamepoteza mechi moja na kuambulia sare mara moja kutokana na michuano saba iliyopita ya EPL msimu huu.

Man-City kwa upande wao wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 14 sawa na Manchester United, Everton na Brighton.

Ushindi kwa Man-City ungeshuhudia Liverpool wakipoteza mechi yao ya kwanza ligini muhula huu. Mabingwa hao wa EPL 2019-20 ndicho kikosi cha pekee ambacho hakijapigwa ligini hadi kufikia sasa muhula huu.

Man-City walishuka dimbani wakipania kujinyanyua baada ya Paris Saint-Germain (PSG) kuwalaza 2-0 katika mechi iliyopita ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Liverpool nao walikuwa wakilenga kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya FC Porto ya Ureno kwenye kipute hicho cha bara Ulaya ugani Estadio do Dragao.

Japo matokeo ya Liverpool katika UEFA yamekuwa yakiridhisha baada ya kufungua kampeni zao kwa ushindi wa 3-2 ugani Anfield, uthabiti wao ligini ulitikiswa na limbukeni Brentford waliowalazimishia sare ya 3-3 katika mchuano uliotangulia kabla ya kumenyana na Man-City.

Liverpool sasa hawajapoteza mechi katika jumla ya mapambano 11 yaliyopita ugani Anfield na wamefunga mabao 17 kutokana na mechi saba zilizopita ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

Rennes wapiga PSG breki kali katika kampeni za Ligue 1

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) walipokezwa kichapo cha kwanza katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Jumapili baada ya Rennes kuwatandika 2-0 ugani Roazhon Park.

Rennes waliokuwa wakichezea katika uwanja wao wa nyumbani waliwekwa kifua mbele na fowadi Gaetan Laborde mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Iliwachukua Rennes sekunde chache pekee mwanzoni mwa kipindi cha pili kupachika wavuni bao la pili baada ya Flavien Tait kujaza kimiani krosi safi aliyoandaliwa na Laborde.

Ingawa PSG walijitahidi kufunga bao la kuwarejesha mchezoni, juhudi zao zilizaa nunge huku goli la Kylian Mbappe likataliwa na refa aliyetumia teknolojia ya VAR kubainisha kwamba alicheka na nyavu akiwa ameotea. Mbappe kwa sasa hajafunga bao katika mechi tano zilizopita kwenye mapambano yote.

Chini ya kocha Mauricio Pochettino, PSG walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara licha ya kujivunia huduma za washambuliaji matata zaidi duniani – Mbappe, Neymar Jr na Lionel Messi.

Ushindi wa Rennes uliwapaisha hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1 kwa alama12 sawa na Olympique Lyon na AS Monaco. Ingawa PSG wangali wanadhibiti kilele cha jedwali kwa pointi 24, azma yao ya kuendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mechi tisa za ufunguzi wa kampeni za Ligue 1 muhula huu ilipigwa breki kali. Rennes watavaana na Metz katika mchuano wao ujao ligini huku PSG wakitarajiwa kujinyanyua dhidi ya Angers kampeni za ligi kuu mbalimbali zitakaporejelewa baada ya pumziko linalopisha michuano ya kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

PSG walishuka dimbani kuvaana na Rennes wakijivunia ushindi katika mechi nne mfululizo – rekodi iliyowawezesha kufungua mapema pengo la alama sita kuliko nambari mbili Lens kileleni mwa jedwali. Mojawapo ya mechi zilizovunia PSG ufanisi huo ni ushindi wa 2-0 dhidi ya Manchester City kwenye kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku ugani Parc des Princes, Ufaransa.

Messi alitumia gozi hilo la UEFA kufungua rasmi akaunti yake ya mabao kambini mwa PSG waliomsajili mwanzoni mwa muhula huu kutoka Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Kwa upande wao, Rennes walishuka ugani wakipania kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi katika mechi mbili za awali ligini.

Kikosi hicho kilikuwa pia na motisha ya kuendeleza makali yaliyokiwezesha kusajili uahindi wa kwanza katika Europa Conference League mnamo Alhamisi iliyopita baada ya kutoka nyuma na kutandika Vitesse ya Ligi Kuu ya Uholanzi 2-1.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Firat atatangaza kikosi cha Harambee Stars kusafiri Morocco kuvaana na Mali mchujo wa kuingia Kombe la Dunia

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Mturuki Engin Firat ametaja kikosi chake cha mwisho cha Harambee Stars kitakachovaana na Eagles ya Mali kwenye mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 nchini Morocco mnamo Oktoba 7.

Mshambuliaji wa klabu ya Al Duhail, Michael Olunga, ambaye ni nahodha, ataongoza utafutaji wa mabao akisaidiana na mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya msimu uliopita Eric Kapaito aliyenunuliwa na Arba Minch City nchini Ethiopia mwezi uliopita pamoja na chipukizi Henry Meja anayetarajiwa kujiunga na klabu ya AIK nchini Uswidi mwezi Januari 2022.

Joash “Berlin Wall” Onyango kutoka Simba SC nchini Tanzania, kipa Farouk Shikalo wa KMC nchini Tanzania na kiungo Ismael Gonzalez anayecheza soka ya malipo nchini Uhispania, ni baadhi ya majina yanayorejea kikosini baada ya kukosa sare tasa dhidi ya Uganda na 1-1 dhidi ya Rwanda mwezi uliopita.

Waliotemwa kutoka kikosi cha 34 waliotajwa Septemba 29 ni kipa James Saruni (Ulinzi Stars), mabeki Samuel Olwande (Kariobangi Sharks), Frank Odhiambo (Gor Mahia), Patila Omoto (Kariobangi Sharks), Keagan Ndemi (Bandari), Reagan Otieno (KCB), Musa Masika (Wazito) na mshambuliaji Sydney Lokale (Kariobangi Sharks). Ovella Ochieng hakuachiliwa na klabu yake ya Marumo Gallants, Afrika Kusini.

Stars imeratibiwa kusafiri nchini Morocco mnamo Oktoba 4 usiku. Mchuano huo utachezewa ugani Agadir kabla ya marudiano uwanjani Nyayo jijini Nairobi mnamo Oktoba 10.

Mali inaongoza Kundi E kwa alama nne baada ya kuchapa Rwanda 1-0 na kutoka 0-0 dhidi ya Uganda katika mechi zake mbili za kwanza. Kenya na Uganda zinafuatana katika nafasi ya pili na tatu mtawalia kwa alama mbili nayo Rwanda inavuta mkia kwa alama moja.

Kikosi cha Harambee Stars kinachosafiri Morocco:

Makipa – Ian Otieno, Brian Bwire, Faruk Shikalo;

Mabeki – Joseph Okumu, Joash Onyango, David Owino Odhiambo, Johnstone Omurwa, Eugene Asike, Daniel Sakari, David Owino Ambulu, Abud Omar, Eric Ouma, Bolton Omwenga;

Viungo – Richard Odada, Lawrence Juma, Ismael Gonzalez, Kenneth Muguna, Duke Abuya, Boniface Muchiri, Eric Zakayo, Phillip Mayaka, Abdalla Hassan;

Washambuliaji – Michael Olunga, Henry Meja, Eric Kapaito.

Watford wamfuta kazi kocha Xisco Munoz

Na MASHIRIKA

WATFORD wamemfuta kazi kocha Xisco Munoz baada ya kujivunia huduma zake kwa kipindi cha miezi 10 pekee.

Mkufunzi huyo raia wa Uhispania mwenye umri wa miaka 41 alisaidia kikosi hicho kupanda ngazi hadi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2020-21 baada ya kuajiriwa Disemba 2020.

Munoz anatimuliwa na Watford siku moja baada ya kikosi hicho kupigwa 1-0 na Leeds United katika EPL na hivyo kusazwa katika nafasi ya 15 kwa alama saba kutokana na mechi saba za hadi kufikia sasa.

“Matokeo ya hivi karibuni ya kikosi hajakuwa ya kuridhisha. Bodi ya usimamizi imefikia maamuzi ya kumtimua Xisco na uongozi unamshukuru kwa mchango wake kikosini,” ikasema sehemu ya taarifa ya Watford.

Watford wametiwa makali na wakufunzi watano tofauti chini ya kipindi cha miaka miwili iliyopita. Kikosi hicho kilichobanduliwa na Stoke City kwenye kipute cha Carabao Cup mnamo Septemba 2021, sasa kitamenyana na Liverpool katika mchuano wao ujao ligini mnamo Oktoba 16, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Real Madrid watandikwa katika La Liga kwa mara ya kwanza msimu huu

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walipoteza mchuano wao wa kwanza katika kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu baada ya kucharazwa 2-1 na Espanyol ugenini mnamo Jumapili.

Raul de Tomas aliwaweka wenyeji kifua mbele katika dakika ya 17 baada ya kukamilisha krosi safi aliyoandaliwa na Adrian Embarba. Aleix Vidal aliongezea Espanyol bao la pili baada ya kumzidi Nacho maarifa na kumpiku kipa Thibaut Courtois kwa ujanja katika dakika ya 60.

Real walifutiwa machozi na mfumaji mahiri raia wa Ufaransa, Karim Benzema dakika 19 kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa. Ingawa Real Madrid walipepetwa, masogora hao wa kocha Carlo Ancelotti bado wanadhibiti kilele cha jedwali la La Liga kwa alama 17 sawa na Real Sociedad na mabingwa watetezi Atletico Madrid.

Kichapo hicho kilikuwa cha pili mfululizo kwa Real kupokezwa chini ya kipindi cha wiki moja baada ya limbukeni Sheriff Tiraspol ya Moldova kuduwaza mabingwa hao mara 13 wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa kichapo cha 2-1 katika mechi ya Kundi D ya kipute hicho mnamo Septemba 28, 2021 uwanjani Santiago Bernabeu.

Masogora wa Ancelotti sasa hawajashinda mechi yoyote kutokana na tatu zilizopita ikizingatiwa kwamba waliambulia sare tasa dhidi ya Villarreal katika mmchuano wao wa awali ligini.

Ingawa Benzema na Eder Militao walivurumisha makombora mazito langoni mwa Espanyol katika kipindi cha pili, fataki hizo zilidhibitiwa vilivyo na kipa Diego Lopez. Bao ambalo Benzema alifungia Real lilikuwa lake la tisa kutokana na mechi tisa za hadi kufikia sasa msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

Bayern Munich wapigwa ligini kwa mara kwanza katika uwanja wa nyumbani baada ya mechi 30

Na MASHIRIKA

EINTRACHT Frankfurt walipokeza Bayern Munich kichapo cha kwanza baada ya mechi 30 za kutoshindwa kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) uwanjani Allianz Arena mnamo Jumapili kwa kuwakomoa 2-1.

Ingawa Bayern Munich waliwekwa uongozini na Leon Goretzka katika dakika ya 29, nahodha wa Frankfurt Martin Hinteregger alirejesha kikosi chake mchezoni kunako dakika ya 32 kabla ya Filip Kostic kuzamisha chombo cha wenyeji wao katika dakika ya 93.

Ushindi huo wa Frankfurt ulikuwa wao wa kwanza kusajili ligini muhula huu na wa kwanza tangu mwaka wa 2000 dhidi ya Bayern ugenini.

Licha ya kichapo, Bayern ambao walipoteza mechi katika uwanja wao wa nyumbani kwa mara ya mwisho mnamo Novemba 2019, walisalia kileleni mwa jedwali la Bundesliga kwa alama 16 sawa na Bayer Leverkusen na moja zaidi nyuma ya Borussia Dortmund na SC Freiburg wanaofunga orodha ya nne-bora.

Bao ambalo Goretzka aliwafungia Bayern lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na mshabuliaji matata raia wa Poland, Robert Lewandowski. Goli hilo lilikuwa la kwanza kwa Goretzka kufungia waajiri wake muhula huu.

Hinteregger alichuma nafuu kutokana na masihara ya mabeki wa Bayern na kumwacha hoi kipa Manuel Neuer katika dakika ya 32 na kusawazisha mambo.

Ingawa Bayern walipania kurejea mchezoni, juhudi zao zilizimwa na kipa wa Frankfurt, Kevin Trapp aliyepangua makombora mazito aliyoelekezewa na Lewandowski, Serge Gnabry na Leroy Sane mwanzoni mwa kipindi cha pili. Frankfurt kwa sasa wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama nane sawa na Stuttgart na Hoffenheim.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

DIMBA NYANJANI: Huyu ‘Mbappe’ wa Young Bulls atisha Ligi ya Kitaifa

Na CHARLES ONGADI

WAKATI Ligi ya Kitaifa Daraja la Kwanza ikiwa pua na mdomo kutamatika kuna huyu straika chipukizi anayegonga vichwa vya habari kwa ustadi wake wa kupachika mabao.

Alex Kazungu Mwalimu, 19, maarufu kama ‘Mbappe’ wa timu ya Young Bulls FC ya Malindi, Kaunti ya Kilifi amedhihirisha kuwa moto wa kuotea mbali kwa ufungaji wa mabao.

Licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika ligi hii yenye ushindani mkali, chipukizi huyu yuko kifua mbele kwa ufungaji mabao akiwa na jumla ya mabao 21.

“Ndoto yangu ni kucheza katika ligi kuu na timu ya taifa kabla ya kuyoyomea ughaibuni kusaka lishe poa,” asema kwa makeke straika huyu jembe.

Wakati Young Bulls ilipokutana kwa mara ya kwanza na Gor Mahia Youth jijini Nairobi, benchi ya kiufundi ya K’Ogalo ilivutiwa sana na uchezaji wake.

Katika pambano hili, ‘Mbappe’ aliwasumbua sana madifenda wa Gor Youth licha ya kupata ushindi wa 3-0 katika mtanage huu.

Katika pambano la marudio katika uga wa Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Shanzu, timu hizi mbili ziliagana sare ya 1-1 huku ‘Mbappe’ akipachika bao hilo la Young Bulls.

Afisa mmoja wa K’Ogalo ambaye hakutaka kutajwa jina, alikiri waziwazi kwamba ‘Mbappe’ ni kama lulu inayosakwa na wengi kutokana na thamani yake.

Aidha, ‘Mbappe’ kwa upande wake anafichua kiu yake ni kuisakatia Bandari FC ama Wazito FC ila anakiri endapo K’Ogalo itamfikia na mkataba mzuri atakubali.

‘Mbappe’ alianza kusakata kabumbu akiwa na umri wa miaka saba (7) pekee akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ya Matsangoni, Kilifi mwaka wa 2007.

Pindi alipojiunga na shule ya upili ya Katana Ngala, Kilifi mwaka wa 2014, Matsangoni FC iliyokuwa ikishiriki ligi ya FKF Pwani kaskazini ilimsajili.

‘Mbappe’ alifaulu kuisaidia Matsangoni FC kushinda ligi ya FKF Pwani kanda ya kaskazini lakini timu hiyo haikuweza kujimudu kufedha kushiriki Ligi ya Kitaifa Daraja la pili.

Lakini ‘Mbappe’ alisajiliwa na Shanzu United FC iliyokuwa katika ligi ya taifa Daraja la Pili ambapo aliisaidia timu hiyo kutamba kabla ya kunyakuliwa na Congo Boys FCmwaka 2019.

Baada ya kipindi kifupi tu alivunja uhusiano wake na Congo Boys na kurudi Malindi alikojiunga na Young Bulls.

‘Mbappe’ asema bidii mazoezini imekuwa ndio siri ya mafanikio yake katika soka huku akiwahimiza wenzake hasa jimo a Pwani kujituma kila mara mazoezini.

“Siri ya ubora wangu ni mazoezi makali. Huwa nahakikisha kila asubuhi na jioni nawatangulia wenzangu uwanjani ili kujifua kinyama,” asema shabiki huyu wa Chelsea ya Uingereza.

Anaongeza kusema kila siku anahakikisha amefanya mazoezi zaidi ya wenzake kwa kuanza mapema na kumaliza kuchelewa.

DIMBA: Ramsdale ‘nyani’ mpya asiyecheka na mtu Emirates

Na GEOFFREY ANENE

AARON Christopher Ramsdale ni mmoja wa makipa wanaojizolea umaarufu kwenye ulimwengu wa soka.

Amejitokeza kuwa shujaa mpya kambini mwa Arsenal msimu huu wa 2021-2022 ambao ungali mbichi, baada ya kushinda mechi zake nne za kwanza tangu awasili mwezi Agosti.

Alikuwa michumani wanabunduki wa Arsenal wakimiminia West Bromwich Albion mabao 6-0 katika kipute cha Carabao Cup mnamo Agosti 25; pia katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Norwich (Septemba 11) na Burnley (Septemba 18) ligini.

Kipa Aaron Ramsdale asherehekea ushindi wa kwanza wa Arsenal msimu huu, dhidi ya Norwich City katika uwanja wa nyumbani Emirates jijini London, Uingereza, Septemba 2021. Picha/ Maktaba

Umaarufu wake ulipanda zaidi alipowakatisha tamaa majirani Tottenham Hotspur katika gozi la London kaskazini ambalo Arsenal ilitawala 3-1 Septemba 26.

Kipa huyu chipukizi alizaliwa Mei 14, 1998.

Alivutiwa kufanya majukumu ya kulinda lango na Mwingereza mwenzake Ben Foster, ambaye ni shujaa wake. Foster, 38, anachezea Watford.

Yeye ni mmoja wa makipa waliovuma nchini Uingereza.Ramsdale si wa kwanza kuwa mchezaji katika familia yake.

Amefuata nyayo za babake Nick aliyekuwa mtimkaji wa mbio za mita 400 kuruka viunzi, naye mamake Caroline alikuwa mchezaji wa netiboli.Safari ya Ramsdale katika ulingo wa soka ilianza akiwa na umri wa miaka saba.

Kipa huyo, kwa jina la utani Ramsy, alipata kunoa talanta yake katika shule ya makipa ya Fred Barber, shule ya upili ya Sir Thomas Boughey na akademia ya Marsh Town na pia Bolton Wanderers.

Alikuwa Bolton kwa kipindi kirefu cha miaka mitano. Hata hivyo, kimo chake hakikuridhisha Bolton na ikamuachilia.Klabu nyingine kadhaa pia zilimkataa kwa sababu ya kukosa kuwa na urefu mzuri.

Alitiwa moyo na wazazi wake pamoja na nduguze Oliver na Edwards kuendelea kutafuta kuwa kipa.

Vyakula maalum vilimsaidia kuongeza umbo lake. Muda si muda Sheffield ilipiku Huddersfield katika kuwania huduma zake. Ilimpa udhamini wa kusoma na kuendeleza talanta yake ya ukipa.

Kandarasi ya kwanza ya soka ya malipo aliyotia saini ilikuwa Julai 2016 akijiunga na timu ya watu wazima ya Sheffield United, kutoka ile ya wachezaji wasiozidi miaka 18.

Alikaa ugani Bramall Lane kwa miezi sita, ikiwemo kuanza maisha katika timu ya watu wazima kwa ushindi wa 6-0 dhidi ya Leyton Orient mnamo Novemba 2016.

Sheffield, ambayo wakati huo ilikuwa katika ligi ya daraja ya tatu, iliuzia Bournemouth mnyakaji huyo kwa Sh150 milioni pekee mnamo Januari 2017. Bournemouth ilikuwa Ligi Kuu (EPL) wakati huo.

Baada ya kuona hachezeshwi ugani Dean Court, Ramsdale aliitisha waajiri wake ruhusa ya kutafuta klabu ya daraja ya chini ili apate uzoefu. Alipelekwa Chesterfield kwa mkopo wa miezi mitano msimu 2017-2018.

Miezi saba iliyofuata, alikuwa kambini Bournemouth kabla kujiunga na AFC Wimbledon kwa mkopo wa miezi mitano msimu 2018-2019.Ramsdale alirejea ugani Dean Court msimu 2019-2020 na kuwa kipa nambari moja wa Bournemouth.

Alinyakuliwa na Sheffield kwa Sh2.6 bilioni baada ya msimu mgumu na Bournemouth, aliyoichezea michuano 37 ikishushwa ngazi kwa kumaliza EPL ndani ya mduara hatari.

Mambo pia hayakuwa mazuri kwake msimu 2020-2021 wakati Sheffield ilitemwa kutoka EPL.

Wachanganuzi wa soka pamoja na mashabiki walikosoa Arsenal vikali ilipoamua kumsaini kwa karibu Sh3.6 bilioni mwezi Agosti, kwa kandarasi itakayokatika Juni 2025.

Hata hivyo, wengi wamelazimika kufyata ndimi zao ugani Emirates baada ya Ramsdale kuandikisha ushindi mara nne mfululizo.

Kocha Mikel Arteta aliamua kumpa fursa ya kuanza mechi baada ya Mjerumani Bernd Leno kupoteza michuano ya kwanza ya ligi dhidi ya Brentford, Chelsea na mabingwa watetezi Manchester City kwa jumla ya magoli 9-0.

Matunda ya kuamua kutupa Leno kitini na kumtumia Ramsdale yamekuwa yakionekana.

Mabao ya Emile Smith Rowe, Pierre-Emerick Aubameyang na Bukayo Saka pamoja na kazi safi michumani ilishuhudia Arsenal ikizima maadui wao Tottenham 3-1 katika Debi ya North London wikendi ya Septemba 26.

Vijana wa kocha Nuno Espirito Santo walikuwa wamepigiwa upatu kulemea Arsenal.Kwa sasa, vita vya kipa nambari moja ugani Emirates kati ya Ramsdale na Leno vinaonekana kuegemea upande wa Mwingereza huyo.

Kimataifa, Ramsdale anawakilisha Uingereza. Alikuwa katika kikosi cha Kombe la Euro 2020 kujaza nafasi ya majeruhi Dean Henderson, lakini sasa anabisha kuonja mechi yake ya kwanza.

Hii ni baada ya kocha Gareth Southgate kumjumuisha katika kikosi kitakachovaana na Andorra (Oktoba 9) na Hungary (Oktoba 12) kwenye kampeni za kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.

Inakisiwa yeye hula mshahara wa Sh6.4 milioni kila wiki (Sh335 milioni kila mwaka) ugani Emirates.

DIMBA NYANJANI: Amazon Tigers shabaha yao kunogesha Ligi Kuu ya KPL ndani ya miaka 4

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Amazon Tigers ni kati ya vikosi vilikuwa vikishiriki mechi za Kundi A kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu.

Amazon, yenye makazi yake katika eneo la Ongata Rongai, Kaunti ya Kajiado, iliasisiwa mwaka 2001.

Kocha na mwanzilishi John Makori, maarufu Mack Deck, anasema alianzisha klabu kwa lengo la kuleta pamoja wachezaji chipukizi ili kukuza talanta zao za soka.

Anadokeza kuwa ukosefu wa ufadhili mara nyingi huchangia wachezaji kuachana na soka. Kocha huyu anasema endapo watapata ufadhili anaamini wanajipatia kipindi cha miaka minne ili kutimiza azimio lao la kufuzu Ligi Kuu nchini (KPL).

Kwenye kampeni za ngarambe ya NWRL msimu uliokamilika wikendi jana, kikosi hicho kilimaliza nafasi ya nne kwa alama 50.

“Tunajituma kwa udi na uvumba katika juhudi za kunoa wachezaji hawa chipukizi maana furaha yetu ni kuona wengi wakinyakuliwa na timu za KPL na hata za ughaibuni,” kocha huyo alieleza.

Amazon Tigers imepoteza wachezaji kadhaa mwaka huu akiwamo Malul Mangar, Zakari Chuang na Victor Opi ambao wameyoyomea Sudan Kusini.

Pia yupo Douglas Omwenga ambaye sasa huchezea Waterworks inayoshiriki Ligi ya Kitaifa Daraja ya Pili. Kwenye harakati za kupalilia talanta za chipukizi klabu hii imefanikiwa kubeba mataji kadhaa ikiwemo Mwathi Cup 2012 na Henry Wuruyu Cup.

Pia imeibuka ya pili kwenye ngarambe ya Laiser Hill Memorial Cup na Ngong Community Policing Cup.

Makori asema uchefuchefu wa kifedha ndiyo changamoto kubwa zaidi kwao, ikizingatiwa kuwa gharama ya kushiriki mechi za ligi inazidi kuwa ghali kila mwaka.

“Tangu mwanzo hatujapata mfadhili, ni wasamaria wema hutuchangia,’’ akaongeza na kutoa wito kwa wahisani kujitokeza kuwapiga jeki katika mikakati ya kunoa talanta zinazoinukia nchini.

Amazon inajivunia kunoa makucha ya wachezaji kadhaa akiwamo Roy Okal (Sofapaka FC) ambayo hushiriki Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL).

Wengine wakiwa Justine Mioda wa SoNY Sugar (FKF-PL) na Emmanuel Onyanja aliyechezea Muhoroni Youth, AFC Leopards na sasa yupo nchini Rwanda ambako hupigia klabu ya APR.

Pia yupo Steve Mwangi ambaye hushiriki soka la kulipwa nchini Omar.

Kadhalika anasema imekuza Charles Odero ambaye ndiye kocha wa klabu ya Juakali FC. Kwenye harakati za kupalilia talanta za wachezaji chipukizi klabu hii imefanikiwa kubeba mataji kadhaa ikiwamo Mwathi Cup 2012 pia Henry Wuruyu cup ilikoshinda Club 46 FC kwa mabao 2-0 katika fainali.

Pia imeibuka ya pili kwenye ngarambe ya Laiser Hill Memorial Cup na Ngong Community Policing Cup.

Anasema uchefuchefu wa kifedha ndiyo changamoto kubwa zaidi kwao, hususan kwa sababu gharama ya kuandaa mechi za Ligi inazidi kuwa ghali kila mwaka.

”Kusema ukweli ukosefu wa fedha za kugharamia shughuli za michezo ndio tatizo kubwa kwetu maana tangia nianzishe klabu hii hatujawahi kupata mfadhili mara nyingi wasamaria wema ndio hutuchangia,” akasema na kutoa wito kwa wahisani kujitokeza kuwapiga jeki kwenye mikakati ya kunoa kucha za wachezaji wanaokuja.

Brighton na Arsenal waumiza nyasi bure katika mechi ya EPL ugani Amex

Na MASHIRIKA

KOCHA Graham Potter amesema ujasiri ulioonyeshwa na vijana wake katika sare tasa iliyosajiliwa na Brighton dhidi ya Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi ugani Amex ni ishara ya uthabiti wa kikosi hicho.

Brighton almaarufu The Seagulls walionekana kuwazidi Arsenal maarifa katika takriban kila idara japo wakashindwa kutumia vyema nafasi kadhaa za wazi walizozipata katika kipindi cha kwanza kupitia Dan Burn, Leandro Trossard, Neal Maupay, Shane Duffy na Pascal Gross.

“Tulijaribu kila kitu. Naamini mashabiki walifurahia sana mechi hiyo kwa sababu tulionyesha ukakamavu japo tulikosa alama tatu muhimu,” akasema Potter.

Fursa ya pekee ya kufunga ambayo Arsenal ya kocha Mikel Arteta ilipata katika kipindi cha kwanza ni jaribio la Pierre-Emerick Aubameyang aliyepania kukamilisha krosi ya Bukayo Saka.

Kombora la kiungo mvamizi Emile Smith Rowe lilidhibitiwa kirahisi na kipa wa Brighton, Robert Sanchez. Matokeo hayo yalisazwa Brighton katika nafasi ya tano jedwalini kwa alama 14 sawa na Manchester United, Liverpool na Everton waliowalazimishia Man-United sare ya 1-1 katika mechi nyingine ya EPL mnamo Jumamosi.

“Huu ni msingi thabiti tunaojitahidi kuweka kikosi. Alama 14 kutokana na mechi saba ni mwanzo mzuri kwa Brighton ligini. Muhimu zaidi kwa sasa ni kuendeleza ukakamavu huo kwa sababu matokeo ya hadi sasa yanatuaminisha zaidi,” akasema Potter.

Arsenal walijibwaga ugani kwa ajili ya mechi hiyo wakipigiwa upatu wa kushindi ikizingatiwa ubora wa matokeo yao katika mechi ya awali iliyowapa ushindi wa 3-1 dhidi ya Tottenham Hotspur.

Ingawa Brighton walielekeza makombora 21 langoni mwa Arsenal, ni mawili pekee kati ya hayo yalionekana kumtatiza kipa Aaron Ramsdale, 23.

Ni Manchester City na Chelsea pekee ambao wanajivunia rekodi ya kupiga jumla ya mechi tisa za EPL bila ya kufungwa katika viwanja vyao vya nyumbani mwaka huu wa 2021. Brighton kwa upande wao wamesakata michuano minane bila kufunga bao ugani Amex.

Arsenal wamepachika wavuni mabao matano pekee katika mechi saba za ufunguzi wa msimu huu, hiyo ikiwa idadi ya chini zaidi kufikia hatua kama hii ya msimu tangu 1986-87.

Chelsea wapepeta Southampton na kupaa hadi kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

CHELSEA walifunga mabao mawili mwishoni mwa kipindi cha pili na kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Southampton katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyochezewa uwanjani Stamford Bridge.

Masogora hao wa kocha Thomas Tuchel walitumia mechi hiyo kujinyanyua baada ya chombo chao kuzamishwa ligini na Manchester City katika mchuano wa awali kisha kupokezwa kichapo kingine cha 1-0 na Juventus katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Timo Werner na Ben Chilwell walifunga katika dakika sita za mwisho baada ya Southampton ya kocha Ralph Hasenhuttl kushuhidia wanasoka wake wakipunguzwa hadi 10 pekee nahodha James Ward-Prowse alipomchezea visivyo kiungo Jorginho.

Chipukizi Trevoh Chalobah aliyepokezwa malezi ya soka katika akademia ya Chelsea aliwaweka waajiri wake kifua mbele kunako dakika ya tisa baada ya Ruben Loftus-Cheek na Chilwell kushirikiana vilivyo katika safu ya mbele.

Chelsea walitamalaki mchezo huo kwa kumiliki asimilia kubwa ya mpira. Hata hivyo, mabao yao mawili yalikataliwa na refa baada ya teknolijia ya VAR kubainisha kwamba Romelu Lukaku alicheka na nyavu za Southampton akiwa ameotea naye Werner alifunga baada ya Cesar Azpilicueta kumkabili vibaya Kyle Walker-Peters.

Tino Livramento ambaye ni mchezaji wa zamani wa Chelsea alichezewa visivyo na Chilwell ndani ya kijisanduku na hivyo kusababisha penalti iliyotumiwa na Ward-Prowse kusawazisha mambo katika dakika ya 61.

Japo Ward-Prowse awali alikuwa ameonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumkabili Jorginho vibaya, adhabu hiyo iliongezwa hadi kuwa kadi nyekundu baada ya refa Martin Atkinson kurejelea tukio hilo kwenye VAR.

Chelsea hawajawahi kupoteza mechi mbili mfululizo katika EPL tangu mikoba yao itwaliwe na Tuchel aliyejaza pengo la Frank Lampard aliyetimuliwa kwa sababu ya matokeo duni mnamo Januari 2021.

Rekodi hiyo ni ishara ya jinsi Chelsea wamepata uthabiti zaidi chini ya mkufunzi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund na Paris Saint-Germain (PSG).

Tuchel alikifanyia kikosi chake kilichozamishwa na Juventus mabadiliko matano huko Werner akitegemewa katika safu ya mbele nao Chilwell na Loftus-Cheek wakiwajibishwa kwa mara ya kwanza ligini msimu huu.

Southampton sasa wanaanza likizo fupi itakayopisha mechi za kimataifa wakiwa na rekodi mbovu ya kukosa ushindi kutokana na mechi saba zilizopita za EPL chini ya Hasenhuttl ambaye ni raia wa Austria.

Inter Milan waingia nafasi ya pili Serie A baada ya kutoka nyuma na kucharaza Sassuolo ugenini

Na MASHIRIKA

INTER Milan walipaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya kutoka nyuma na kuwakung’uta Sassuolo 2-1 mnamo Jumamosi.

Fowadi Edin Dzeko alitokea benchi katika kipindi cha pili na kusawazishia Inter katika dakika ya 58 kabla ya Lautaro Martinez kufunga bao la ushindi kupitia penalti ya dakika ya 78.

Awali, Domenico Berardi alikuwa amewaweka Sassuolo kifua mbele kupitia penalti ya dakika ya 22. Bao hilo lilikuwa la tatu kwa sogora huyo raia wa Italia kufungia waajiri wake ligini muhula huu.

Mechi hiyo ilimpa Dzeko jukwaa maridhawa ya kuandikisha rekodi mpya ya kuwa mwanasoka wa kwanza wa Inter kufunga mabao sita kutokana na mechi saba za kwanza tangu Ronaldo de Lima afanye hivyo mnamo 1997-98.

Sassuolo walijipata uongozini baada ya Berardi kumwacha hoi kipa Samir Handanovic kupitia penalti iliyosababishwa na tukio la Milan Skriniar kumchezea visivyo Jeremie Boga ndani ya kijisanduku.

Bao hilo liliwapa Sassuolo motisha ya kucheza kwa kujituma zaidi huku wakivuruga mipango yote ya wageni wao kurejea mchezoni katika kipindi cha kwanza. Jaribio la pekee la Inter langoni mwa Sassuolo katika kipindi cha kwanza ni wakati ambapo kombora la Nicolo Barella lilipanguliwa na kipa Andrea Consigli kunako dakika ya 39.

Zaidi ya kujizolea alama tatu muhimu, Inter waliendeleza rekodi ya kufunga angalau mabao mawili katika kila mchuano kwa kufanya hivyo katika mechi yao ya 12 mfululizo ligini.

MATOKEO YA SERIE A (Oktoba 2, 2021):

Torino 0-1 Juventus

Sassuolo 1-2 Inter Milan

Salernitana 1-0 Genoa

Juventus waponyoka na alama tatu katika gozi la Serie A dhidi ya Torino jijini Turin

Na MASHIRIKA

JUVENTUS walifunga bao mwishoni mwa kipindi cha pili na kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Torino katika gozi la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) lililowakutanisha Jumamosi usiku jijini Turin.

Manuel Locatelli aliwapachikia wenyeji Juventus bao hilo la pekee na la ushindi katika dakika ya 86 licha ya Torino kusalia thabiti katika kipindi kirefu cha mchezo na kunyima wenyeji wao fursa nyingi za kufunga magoli.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Juventus kukamilisha bila kufungwa bao msimu huu na hivyo, walifaulu kukomesha rekodi yao ya awali ya kufungwa katika mechi 21 mfululizo.

Chini ya kocha Massimiliano Allegri, Juventus kwa sasa wanashikilia nafasi ya nane kwenye msimamo wa jedwali la Serie A kwa alama 11 sawa na Lazio na Atalanta. Ni pengo la pointi saba ndilo linatamalaki kati yao na viongozi wa jedwali, Napoli.

Juventus wangalifunga mabao zaidi katika mechi hiyo ila bahati ikakosa kusimama na wanasoka Moise Kean,  Weston McKennie na Juan Cuadrado walioshuhudia fataki zao zikidhibitiwa na kipa Vanja Milinkovic-Savic.

Sasa Lukic na Rolando Mandragora nao walimshughulisha vilivyo kipa Wojciech Szczesny wa Juventus mwishoni mwa kipindi cha pili. Bao ambalo Locatelli alifungia Juventus lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Federico Chiesa.

Torino kwa sasa wanashikilia nafasi ya 11 kwa alama nane sawa na Bologna.

Atletico Madrid waendeleza masaibu ya Barcelona na kumzidishia kocha Koeman presha ya kupigwa kalamu

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), Atletico Madrid, waliwafikia Real Madrid kileleni mwa jedwali mnamo Jumamosi baada ya kukomoa Barcelona 2-0 katika matokeo yanayomweka kocha Ronald Koeman pembamba zaidi uwanjani Camp Nou.

Thomas Lemar alifungia Atletico bao la kwanza baada ya kushirikiana vilivyo na Joao Felix pamoja na Luis Suarez aliyefunga la pili dhidi ya waajiri wake wa zamani. Antoine Griezmann pia aliwajibishwa dhidi ya Barcelona ambao ni waajiri wake wa zamani ila aliletwa uwanjani mwishoni mwa kipindi cha pili.

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Barcelona kupoteza ligini muhula huu na sasa wanashikilia nafasi ya nane jedwalini kwa alama 12, tano nyuma ya Atletico wanaotiwa makali na kocha Diego Simeone.

Ingawa alama za Atletico zinawiana na zile za Real (17), Atletico wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na Real ya kocha Carlo Ancelotti.

Kabla ya kushuka dimbani kumenyana na Atletico, Barcelona walikuwa wameshinda mechi tatu na kuambulia sare mara tatu kisha kupokezwa vichapo vya 3-0 kutoka kwa Bayern Munich na Benfica kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Msururu wa matokeo hayo duni yanamweka Koeman katika presha ya kupigwa kalamu huku mikoba ya Barcelona ikianza tayari kuhusishwa na wakufunzi Andrea Pirlo, Antonio Conte na Xavi Hernandez.

Ingawa walizidiwa ujanja na wenyeji wao Atletico, Barcelona walipata nafasi kadhaa za kufunga mabao kupitia Philippe Coutinho, Frenkie de Jong na Memphis Depay waliomwajibisha kipa Jan Oblak katika vipindi vyote viwili vya mchezo.

Barcelona kwa sasa wanaingia mapumziko ya wiki mbili ili kupisha mechi za kimataifa na wanatarajiwa kurejea ugani mnamo Oktoba 17 watakaposhuka dimbani kumenyana na Valencia kwenye La Liga uwanjani Camp Nou.

“Iko kazi kubwa ya kufanywa kambini mwa Barcelona. Lakini haiwezi kufanywa katika kipindi cha siku moja. Inatubidi kujitahidi kuwaaminisha zaidi chipukizi wetu na kusalia na matumaini kwamba mafowadi wetu veteran watapona majeraha hivi karibuni na kurejea ulingoni mwa matao ya juu,” akasema Koeman ambaye ni raia wa Uholanzi.

Sahib asherehekea ‘bathdei’ kwa kutawala Autocross Nanyuki, Hamza abwaga babake Asad

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA mtetezi Sahib Omar alisherehekea kugonga umri wa miaka 35 kwa kushinda duru ya saba ya mashindano ya KCB Nanyuki Autocross katika eneo la Batian View, Jumapili.

Sahib tayari alinusia ushindi baada ya mpinzani wake mkuu Eric Bengi kushindwa kufikia muda wake katika mashindano ya kufuzu kushiriki fainali.Ushindi wa Sahib katika eneo la Nanyuki ulikuwa wa tatu msimu huu baada ya kutawala duru mbili katika eneo la Jamhuri Park jijini Nairobi.

Dereva huyo kutoka timu ya Ray Racing alivuna ushindi katika eneo la Batian akiendesha gari la Subaru Impreza GC8.

Alilemea Bengi katika mzunguko wa kwanza kwa sekunde 0.003. Sahib alishinda mzunguko wa pili sekunde mbili mbele ya Bengi kabla ya kumzidia maarifa tena kwa sekunde 0.005 katika mzunguko wa tatu.

Isitoshe, Sahib alizoa alama mbili za nyongeza kwa kuweka kasi ya juu ya siku (FTD) katika mzunguko wa pili alioumaliza kwa dakika 1:54.72.

Qahir Rahim apiga kona katika barabara zilizojaa matope katika eneo la Batian View mjini Nanyuki…PICHA/GEOFFREY ANENE

“Ninahisi vizuri sana kutwaa taji la Nanyuki katika siku yangu ya kuzaliwa nikisherehekea kufikisha miaka 35. Barabara zilikuwa telezi saa za asubuhi, lakini zilikauka baadaye mashindano yakiendelea. Kwa jumla, barabara hizi ni nzuri sana kupaisha magari,” alisema Sahib.

Kiongozi wa kitengo cha magari ya 4WD, Lovejyot Singh alizidiwa ujanja katika juhudi zake za kukamata nafasi mbili za kwanza baada ya gari lake kukumbwa na hitilafu.Naye, Yuvraj Rajput aliibuka mshindi katika kitengo cha Bambino kwa kumpiku mfalme wa raundi ya sita Karanveer Singh Rooprai.

Hamza Anwar alitawala kitengo cha wazi akimaliza mbele ya baba yake Asad Anwar.Kitengo cha Bambino kilikuwa na pacha John na Joline Jessel. Wawili hawa ni wajukuu wa bingwa wa kitengo cha magari cha Rally Raid mwaka 2010 Sammy Jessel.

Sam Karangatha aliandikisha ushindi wake wa tatu msimu huu katiia kitengo cha 2WD Non-Turbo akimzima hasimu wake Rajveer Thethy.

Jepkosgei ni malkia wa London Marathon, Kipchumba nambari mbili kitengo cha wanaume

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Joyciline Jepkosgei ndiye malkia mpya wa mbio za kifahari za London Marathon mwaka 2021 baada ya kuzikamilisha kwa saa 2:17:34 nchini Uingereza, Jumapili.

Bingwa huyo wa New York City Marathon, ambaye aliwahi kuwa mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 21, aliongeza kasi baada ya kilomita ya 35 na kujitoa kabisa katika kundi lililokuwa na Waethiopia Ashete Bekere na Degitu Azimeraw na mshikilizi wa rekodi ya dunia Mkenya Brigid Kosgei.

Kabla ya hapo, Jepkosgei, Mwisraeli Lonah Chemutai Salpeter aliye na asili ya Kenya, Bekere na Kosgei walikuwa wamebadilishana uongozi mara kadhaa. Hata hivyo, hakuna aliyepata jibu Jepkosgei alipochukua uongozi zikisalia kilomita saba.

Azimeraw na Bekere walifuatana katika nafasi ya pili na tatu mtawalia naye Kosgei, ambaye alishinda London Marathon mwaka 2019 na 2020, akakamilisha katika nafasi ya nne.

Kwa makala mawili mfululizo, wanaume kutoka Kenya waliambulia pakavu huku taji likienda Ethiopia. Vincent Kipchumba aliridhika katika nafasi ya pili kwa saa 2:04:28. Kipchumba pia alimaliza London Marathon nambari mbili mwaka 2020, nafasi moja mbele ya Muethiopia Sisay Lemma aliyeibuka bingwa mwaka huu kwa saa 2:04:01. Mosinet Geremew (2:04:41) alikamilisha katika nafasi ya tatu.

 

Matokeo (10-bora):

Kinadada – Joyciline Jepkosgei (Kenya) saa 2:17:34, Degitu Azimeraw (Ethiopia) 2:17:58, Ashete Bekere (Ethiopia) 2:18:18, Brigid Kosgei (Kenya) 2:18:40, Lonah Chemtai (Israel) 2:18:54, Valary Jemeli (Kenya) 2:20:35, Joan Chelimo (Kenya) 2:21:23, Zeineba Yimer (Ethiopia) 2:21:40, Tigist Girma (Ethiopia) 2:22:45, Charlotte Purdue (Uingereza) 2:23:26;

Wanaume – Sisay Lemma (Ethiopia) 2:04:01, Vincent Kipchumba (Kenya) 2:04:28, Mosinet Geremew (Ethiopia) 2:04:41, Evans Chebet (Kenya) 2:05:43, Birhanu Legese (Ethiopia) 2:06:10, Shura Kitata (Ethiopia) 2:07:51, Philip Sesemann (Uingereza) 2:12:58, Joshua Griffiths (Uingereza) 2:13:39, Matthew Leach (Uingereza) 2:15:31, Andrew Davies (Uingereza) 2:15:36.

 

Mkenya Njeru ashinda Kombe la Dunia mbio za kupanda milima Ndung’u atwaa taji la duru ya Zumaia nchini Uhispania

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Joyce Njeru na Geoffrey Ndung’u wamefagia mataji ya mbio za kupanda milima za kilomita 22 ya Zumaia Flysch nchini Uhispania mnamo Jumapili.

Njeru, ambaye alipokonya Mhispania Oihana Kortazar taji la Zumaia Flysch, pia ameibuka bingwa wa Kombe la Dunia (WMRA Classic World Cup). Amekuwa na msimu mzuri ambapo alinyakua mataji ya Trofeo Ciolo (Italia), Grossglockner (Austria) na Krkonossky (Czech).

Katika mbio za Zumaia Flysch, ambazo ni mikondo ya 14 na 15 ya Kombe la Dunia 2021, Njeru alifuatwa kwa karibu na mshindi wa mikondo ya La Montee du Nid d’Aigle (Ufaransa) na Sierra Zinal (Uswisi), Lucy Murigi kutoka Kenya aliyekamilisha mkondo wa Grossglockner katika nafasi ya tatu.

Murigi ni bingwa wa dunia mwaka 2018. Mwitaliano Alice Gaggi alikamilisha katika mduara wa tatu-bora Zumaia Flysch. Ndung’u, ambaye alitwaa taji la Krkonossky, kumaliza Trofeo Ciolo na nambari nne Trofeo Nasego na nambari mbili Grossglockner, aliibuka mshindi mpya wa Zumaia Flysch baada ya kuvua taji bingwa mtetezi Oiher Ariznabarreta kutoka Uhispania.

PICHA/GEOFFREY ANENE

Raia wa Hungary Sandor Szabo alifuata Ndung’u mgongoni naye Mhispania Amets Aramberi akaridhika na nafasi ya tatu. Kombe la Dunia la mbio za kupanda milima linajumuisha mikondo 16 katika maeneo 12 katika mataifa manane.