Vipusa wa Arsenal wararua Aston Villa na kutua kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza

Na MASHIRIKA

ARSENAL waliendeleza umahiri wao katika Ligi Kuu ya Uingereza kwa Wanawake (WSL) kwa kupokeza Aston Villa kichapo kinono cha 4-0 mnamo Jumamosi uwanjani Villa Park.

Mabao yote ya Arsenal yalipachikwa wavuni katika kipindi cha pili. Kim Little alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 51 kabla ya Mana Iwabuchi na Katie McCabe kutokea benchi na kucheka na nyavu za Villa kunako dakika ya 80 na 83 mtawalia.

Kichapo hicho kilitamatisha rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa Villa ligini katika kampeni za msimu huu huku Arsenal wakidhibiti sasa kilele cha jedwali la WSL kwa pointi 12.

Arsenal walitamalaki mchuano huo kwa kumiliki asilimia kubwa ya mpira na walistahili kujiweka uongozini kupitia Vivianne Miedema na Beth Mead kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa.

Little ambaye ni nahodha wa Arsenal alizamisha kabisa chombo cha Villa mwishoni mwa kipindi cha pili kwa kufungia waajiri wake bao la nne. Goli hilo lilikuwa lake la 150 ndani ye jezi za Arsenal.

Hearts wabamiza Motherwell na kuendeleza rekodi ya kutoshindwa katika Ligi Kuu ya Scotland

Na MASHIRIKA

HEARTS waliendeleza rekodi ya kutoshindwa katika Ligi Kuu ya Scotland msimu huu baada ya kupepeta Motherwell 2-0 mnamo Jumamosi usiku uwanjani Tynecastle.

Liam Boyce alifungua ukurasa wa mabao kupitia penalti katika dakika ya tano baada ya kuchezewa visivyo na Liam Kelly. Hearts walifungiwa bao la pili na Stephen Kingsley katika dakika ya 22 kupitia frikiki.

Penalti ya pili ya Boyce ilipanguliwa na kipa wa Motherwell walioshuhudia juhudi zao za kurejea mchezoni zikizimwa na kipa Craig Gordon. Kichapo hicho kilisaza Motherwell katika nafasi ya nne.

Mbali na kukomesha rekodi ya kutoshindwa kwa Motherwell katika mechi sita mfululizo, ushindi wa Hearts uliwawezesha kuwaruka Hibernian na mabingwa watetezi Rangers baada ya kupiga mechi yao ya nane bila ya kupoteza.

Bao la Boyce lilikuwa lake la 10 kufikia sasa kambini mwa Hearts msimu huu. Waajiri wake kwa sasa wanajiandaa kumenyana na mabingwa watetezi Rangers mnamo Oktoba 16 wakati ambapo Motherwell watamenyana na Celtic uwanjani Fir Park

Burnley na Norwich kusubiri zaidi kusajili ushindi wa kwanza ligini baada ya kuambulia sare tasa

Na MASHIRIKA

SUBIRA ya Burnley na Norwich City kusajili ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu itaendelea baada ya vikosi hivyo kuambulia sare tasa mnamo Jumamosi ugani Turf Moor.

Ilikuwa ya mechi ya kwanza kati ya 44 kuwahi kukutanisha Burnley na Norwich kukamilika kwa sare tasa.Dwight McNeil alipoteza fursa nzuri ya kufungia Burnley naye Matt Lowton akashuhudia kombora lake likigonga mwamba wa goli la Norwich ambao hadi kufikia sasa,

hawajafunga bao lolote kutokana na mechi nne zilizopita za ugenini.Mathias Normann nusura afunge mpira wa ikabu katika kipindi cha kwanza ila fataki yake ikapanguliwa na kipa Nick Pope.

Kipindi cha kwanza cha mchuano huo kilishuhudia jumla ya kadi tano za manjano zikitolewa na refa Kevin Friend aliyepuuza malalamishi mengi ya Burnley kutaka kupewa mkwaju wa penalti.

Sare hiyo iliwavunia Norwich alama yao ya kwanza ligini msimu huu baada ya kusakata jumla ya michuano saba ya ufunguzi na kupoteza sita.Kwa upande wao, Burnley sasa wanakamata nafasi ya 18 kwa alama tatu sawa na Newcastle United.

Kwa mara nyingine, Norwich wamejipata pagumu katika marejeo yao kwenye EPL. Japo walikuwa na mwanzo mgumu uliwashuhudia wakipigwa na Liverpool na Manchester City, Norwich walizamishwa na Watford na Everton katika michuano miwili iliyowashuhudia wakifungwa mabao matano nao wakitikisa nyavu za wapinzani mara moja pekee.

Japo walitatizika kufunga Burnley, Norwich walisalia imara katika safu ya ulinzi huku wakikamilisha mechi kwa mara ya kwanza bila ya kufungwa bao. Mechi hiyo ilikuwa ya 400 kwa kocha Sean Dyche kusimamia kambini mwa Burnley.

Kocha Steve Bruce katika hatari ya kutimuliwa na Newcastle baada ya kuchapwa na Wolves ligini

Na MASHIRIKA

KOCHA Steve Bruce wa Newcastle United amekiri kufadhaishwa na matokeo duni ya kikosi chake baada ya kichapo cha 2-1 kutoka kwa Wolves katika Ligi kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi kumtia katika presha ya kupigwa kalamu na waajiri wake.

Hwang Hee-chan alifunga mabao mawili na kusaidia Wolves ya kocha Bruno Lage kusajili ushindi wa kwanza katika uwanja wa nyumbani msimu huu. Bao la ushindi la Wolves lilifumwa wavuni dakika chache baada ya Jeff Hendrick kusawazishia Newcastle.

Matokeo hayo yalisaza Newcastle ambao hawajashinda mechi yoyote ligini kufikia sasa miongoni mwa vikosi vitatu vya mwisho jedwalini. Newcastle kwa sasa wanashikilia nafasi ya 19 kwa alama tatu sawa na Burnley ambao pia waliambulia sare tasa dhidi ya Norwich City ugani Turf Moor.

Bruce amekuwa akikosolewa mara kwa mara na mashabiki wa Newcastle kiasi cha mabango ya kumshinikiza kubanduka uwanjani St James’ Park kuinuliwa uwanjani baada ya kuchapwa na Wolves ugani Molineux mnamo Jumamosi.

Hata hivyo, mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 60 anaamini kwamba ana tajriba ya kutosha kubadilisha mkondo wa mambo kadri anavyokaribia kusimamia mchuano wake wa 1,000 katika ulingo wa ukufunzi.

“Hata uwe nani, awe kocha wa Newcastle au la, iwapo hutashinda mechi yoyote kutokana na saba, basi uwezekano wa kufutwa kazi huwa mkubwa. Hivyo, tuna ulazima wa kujinyanyua upesi na kuanza kushinda mechi,” akasema Bruce.

Dortmund wakomoa Augsburg na kupaa hadi nafasi ya pili kwenye Bundesliga

Na MASHIRIKA

BORUSSIA Dortmund walipaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) baada ya kupepeta Augsburg 2-1 mnamo Jumamosi uwanjani Signal Iduna Park.

Raphael Guerreiro alifungulia Dortmund ukurasa wa mabao kupitia mkwaju wa penalti katika dakika ya 10 kabla ya Julian Brandt kufunga goli la pili kunako dakika ya 51 baada ya Andi Zeqiri kusawazishia Augsburg katika dakika ya 35.

Zeqiri anachezea Augsburg kwa mkopo kutoka Brighton ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na goli lake lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa na Arne Maier aliyeshuhudia kombora lake likibusu mwamba wa lango la Dortmund.

Penalti ambayo Dortmund walipewa ilitokana na tukio la Donyell Malen kuchezewa visivyo ndani ya kijisanduku. Brandt alizamisha kabisa chombo cha wageni wao baada ya kushirikiana na Marius Wolf na Marco Reus ambaye kwa pamoja na Thorgan Hazard, pia walishuhudia fataki zao zikigonga mhimili wa goli la Augsburg.

Dortmund kwa sasa wanajivunia alama 15, moja pekee nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi, Bayern Munich.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Oktoba 2, 2021):

Dortmund 2-1 Augsburg

Hertha Berlin 1-2 Freiburg

Stuttgart 3-1 Hoffenheim

Wolfsburg 1-3 M’gladbach

Kocha alia timu yake ya Nairobi Water haijazoa ushindi mkubwa handiboli

Na AGNES MAKHANDIA

KOCHA wa timu ya handiboli ya kinadada ya Nairobi Water, Jack Ochieng amekiri kuwa bado hawajafika kiwango cha kusema wako bora kabisa licha ya kuwa kuzoa ushindi wa nane mfululizo Jumamosi.

Alisema hayo baada ya vipusa wake kuaibisha Rangers kwa magoli 38-17 kwenye Ligi Kuu ugani Nyayo jijini Nairobi.Water ilisomba Rangers 55-17 katika mechi ya mkondo wa kwanza na alisema kuwa ushindi wa pili haukumridhisha.

“Huwa hatuchezi hivi. Mabingwa watetezi hawafai kuonyesha mchezo kama huu. Haukuridhisha kabisa na nadhani tutalazimika kukaa chini na kutafuta mbinu zitakazotusaidia kuandikisha matokeo mazuri katika mashindano yajayo ya Afrika Mashariki na Kati nchini Tanzania na mechi zijazo ligini,” alichemka Ochieng.

“Mwezi Septemba, mchezo wetu na magoli tuliyofunga dhidi ya wanajeshi wa KDF hayakuwa mazuri. Nikitazama matokeo haya dhidi ya Rangers, najawa na hofu. Ukweli ni kuwa wachezaji wanajua wanaweza kufanya vyema kuliko matokeo haya,” aliongeza.

Water ililemea KDF pembamba 29-28 mwezi uliopita. Katika ushindi wa hivi punde, Brenda Ariviza alipachika mabao tisa naye Cecilia Katheu akachangia saba kwa upande wa Water.

Naomi Wamalwa na Tentrix Masika walifungia Rangers magoli matano kila mmoja. Water inaongoza ligi kwa alama 16 baada ya kujibwaga uwanjani mara nane. Inafuatiwa na KDF iliyo na alama 12 kutokana na michuano saba.

KDF inapumzika wikendi hii. Nanyuki inakamilisha mduara wa tatu-bora kwa alama 11 baada ya kusakata mechi tisa. Itapepetana na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) mnamo Jumapili.

Rangers ilishinda Amazon 40-28 katika mechi yake ya pili baadaye Jumamosi. Katika ligi ya wanaume, JKUAT ililemea Rangers 27-26, Gunners ikazidia Thika ujanja 37-31 nayo GSU ikapata ushindi wa bwerere Vickers ilipokosa kufika uwanjani.

Man-United wakabwa koo na Everton ligini

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walipoteza alama mbili muhimu katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu leo baada ya Everton kuwalazimishia sare ya 1-1 uwanjani Old Trafford.

Ni matokeo yaliyowaweka masogora wa kocha Ole Gunnar Solskjaer kigezoni kwa mara nyingine ikizingatiwa kwamba walishuka dimbani siku tatu baada ya kuponea chupuchupu katika gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) dhidi ya Villarreal ya Uhispania ugani Old Trafford.

Sare dhidi ya Everton iliendeleza msururu wa matokeo duni ya Man-United katika uwanja wao wa nyumbani muhula huu. Masogora hao walipigwa 1-0 na Aston Villa ligini siku saba zilizopita ugani Old Trafford baada ya West Ham United kuwapokeza kichapo kingine cha 1-0 kilichowadengua kwenye raundi ya tatu ya Carabao Cup.

Kufikia sasa, Man-United ambao ni mabingwa mara 20 wa EPL wameambulia sare mara mbili, kupoteza mechi moja na kushinda michuano minne kati ya saba iliyopita. Kikosi hicho kinajivunia alama 14 jedwalini sawa na Everton na Liverpool.

Wakicheza dhidi ya Everton, masogora wa Solskjaer waliwekwa kifua mbele na Anthony Martial aliyefunga bao kwa mara ya kwanza tangu Februari mwaka huu. Hata hivyo, juhudi za fowadi huyo raia wa Ufaransa zilifutwa na Andros Townsend aliyesawazishia Everton ya kocha Rafael Benitez.

Bao la Townsend lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Demarai Gray na Abdoulaye Doucoure aliyetatiza ngome ya Man-United waliolazimika kumuondoa Edinson Cavani katika dakika ya 57 na mahali pake kuchukuliwa na Cristiano Ronaldo aliyekuwa mfungaji wa bao la ushindi dhidi ya Villarreal kwenye UEFA.

Everton walidhani walikuwa wamepata bao la ushindi kunako dakika ya 86 ila teknolojia ya VAR ikabainisha kwamba Yerry Mina alicheka na nyavu za Man-United baada ya kuotea.

Jitihada za Man-United kurejea mchezoni zilizimwa na Everton waliosalia thabiti katika kipindi cha pili licha ya wenyeji kuleta uwanjani Jadon Sancho na Paul Pogba waliojaza nafasi za Martial na Fred mtawalia.

Baada ya kumenyana na Leicester City katika mchuano ujao ligini, Man-United watavaana na Atalanta ya Italia kwenye UEFA kabla ya ubabe wao kwenye EPL kutiwa kwenye mizani kwa mara nyingine dhidi ya Liverpool na Tottenham Hotspur kwa usanjari huo.

Vihiga Queens yapigwa fainali ya FKF Cup kuambulia patupu mashindano ya Kenya 2021

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) Vihiga Queens wameambulia pakavu msimu huu katika soka ya kitaifa baada kupigwa 2-1 na Ulinzi Starlets katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Kenya (FKF) la kinadada mjini Nakuru, Jumamosi.

Vipusa wa kocha Boniface Nyamunyamu, ambao walipoteza taji la Ligi Kuu kwa Thika Queens, wamezamishwa na wanajeshi wa Ulinzi kupitia mabao ya Lucy Mukhwana na Christine Wekesa.

Mukhwana alifungua ukurasa wa magoli dakika ya nane baada ya beki wa mwisho wa Vihiga kupokonywa mpira kabla ya Mukhwana kumwaga kipa Lilian Awuor kupitia shuti kali karibu na mlingoti.

Pande zote zilipoteza nafasi kadhaa nzuri, ingawa Ulinzi ya kocha Joseph Mwanzia ilionekana kuwa juu kimchezo kuliko Vihiga ambayo safu yake ya ulinzi haikuwa imara.

Topister Nafula alisawazishia Vihiga dakika ya 64 baada ya kutokea msongamano katika lango la Ulinzi.Shuti kali kutoka nje ya kisanduku kutoka kwa Wekesa dakika 10 baadaye liliamua mshindi wa mechi hiyo.

Vihiga ya kocha Boniface Nyamunyamu itashiriki Klabu Bingwa Afrika mwezi Novemba nchini Misri baada ya kutawala mashindano ya Cecafa jijini Nairobi mwezi uliopita.

Imetiwa katika Kundi B pamoja na Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), ASFAR (Morocco) na Rivers Angles (Nigeria).

 

Sesay hatimaye achagua Sierra Leone badala ya kuchezea Harambee Stars

Na GEOFFREY ANENE

BEKI wa pembeni kushoto David Sesay amekubali kujumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Sierra Leone kuzima matumaini ya kuchezea Kenya kimataifa.

Mzawa huyo wa Uingereza, ambaye anachezea klabu ya Barnet nchini Uingereza, aliwahi kuitwa mara ya kwanza katika timu ya Harambee Stars mwaka 2019 kutokana na kuwa mama yake kuwa Mkenya.

Hakuitikia mwito huo wa kocha Sebastien Migne akisema hakuwa amepata pasipoti ya Kenya. “Sikukataa mwito, lakini singeweza kujiunga na Harambee Stars kwa sababu nilikuwa tu nimepata klabu mpya wakati huo.

Sasa, niko asilimia 100 tayari kuchezea Kenya. Kenya ni timu ambayo ni chaguo langu bora,” alinukuliwa akisema wakati huo akichezea Crawley Town.Hata hivyo, Sesay,23, ambaye baba yake anatoka Sierra Leone, amejumuishwa katika timu ya taifa hilo kutoka magharibi mwa Afrika, ishara kuwa ameamua ndilo chaguo lake.

Kocha John Keister amemjumuisha katika kikosi cha wachezaji 19 wa Sierra Leone wanaocheza ughaibuni kwa mechi za kirafiki dhidi ya Sudan Kusini (Oktoba 6), Gambia (Oktoba 9) na Morocco (Oktoba 12) jijini Casablanca.

Beki wa zamani wa Spurs na Liverpool, Steven Caulker, kuchezea Sierra Leone kwa mara ya kwanza

Na MASHIRIKA

BEKI wa zamani wa Tottenham Hotspur na Liverpool, Steven Caulker ameitwa katika timu ya taifa ya Sierra Leona kwa mara ya kwanza.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 ni miongoni mwa wachezaji 19 wanaotandaza soka ya kulipwa ugenini ambao wameitwa kambini mwa Sierra Leone kwa ajili ya mechi za kirafiki dhidi ya Sudan Kusini, Gambia na Morocco mjini Casablanca, Morocco mnamo Oktoba 6,9 na 12 mtawalia.

Caulker ambaye kwa sasa anachezea Gaziantep kwa mkopo kutoka Fenerbache ambao ni watani wao wakuu katika Ligi Kuu ya Uturuki, aliwahi kuchezea Uingereza mara moja pekee katika mechi ya kirafiki waliyoipoteza kwa 4-2 dhidi ya Uswidi mnamo 2012.

Caulker alifunga bao katika mchuano huo. Alipata fursa ya kuwajibishwa katika mechi hiyo baada ya kuwajibishwa katika kila mchuano kwa dakika zote za mchezo wakati wa kampeni za Uingereza kwenye Olimpiki za 2012 jijini London.

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Caulker anaruhusiwa kuchezea Sierra Leone uliko usuli wa babu yake kwa kuwa mechi aliyochezea Uingereza ilikuwa ya kirafiki.

Caulker aliyewajibishwa mara 10 na Uingereza katika kikosi cha chipukizi wa U-21 atakuwa miongoni mwa wanasoka tegemeo wa Sierra Leone kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Januari 2022 nchini Cameroon.

Sogora huyo ambaye ni mraibu mkubwa wa kushiriki michezo ya kamari, aliwahi pia kuvalia jezi za Queens Park Rangers (QPR), Swansea City na Cardiff City.

Wachezaji wengine wapya ambao wamejumuishwa katika kikosi cha Sierra Leone ni David Sesay ambaye anachezea kikosi cha Barnet kinachoshiriki Ligi ya Daraja ya Tano nchini Uingereza na Issa Kallon anayevalia jezi za SC Cambuur nchini Uholanzi.

Wengine ni fowadi wa Genoa, Yayah Kallon na Jonathan Morsay anayepiga soka ya kulipwa nchini Ugiriki.

Williams Inaki wa Bilbao aweka rekodi ya kuchezeshwa katika mechi nyingi zaidi mfululizo kwenye La Liga

Na MASHIRIKA

FOWADI Inaki Williams wa Athletic Bilbao aliweka rekodi mpya ya kuwa mwanasoka ambaye sasa amewajibishwa katika michuano mingi zaidi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa mfululizo baada ya kuwa sehemu ya kikosi kilichowapepeta Alaves 1-0 mnamo Ijumaa usiku

Sogora huyo raia wa Uhispania mwenye umri wa miaka 27 alichezeshwa katika mchuano wake wa 203 mfululizo dhidi ya Alaves na hivyo akavunja rekodi iliyokuwa iliyowekwa na beki wa zamani wa Real Sociedad, Juan Larranaga kati ya 1986 na 1992.

Williams alianza safari ya kuweka rekodi yake mnamo Aprili 20, 2016 na kufikia sasa, amepachika wavuni mabao 39 na kuchangia 25 mengine.

Wakicheza dhidi ya Alaves, bao la Bilbao ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita jedwalini kwa alama 13 lilifumwa wavuni na Raul Garcia dakika chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza uwanjani San Mames kupulizwa.

Idadi kubwa zaidi ya mechi ambazo zimewahi kusakatwa na mchezaji mmoja kwa mfululizo katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ni 310 na rekodi hiyo inashikiliwa na kipa Brad Friedel.

Miongoni mwa wachezaji wa ndani ya uwanja (ambao si makipa), rekodi hiyo inashikiliwa na Frank Lampard aliyewahi kuwajibishwa na Chelsea ligini mara 164 mfululizo kati ya Oktoba 2001 na Disemba 2005.

Stoke City wakomesha rekodi ya kutoshindwa kwa West Brom kwenye Championship

Na MASHIRIKA

NICK Powell alifunga bao la pekee katika ushindi wa 1-0 uliowezesha Stoke City kupiga breki rekodi ya kutoshindwa kwa West Bromwich Albion katika Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship).

Chini ya kocha Michael O’Neill, Stoke City waliwazidi West Brom maarifa katika takriban kila idara huku Jacob Brown na Mario Vrancic walishuhudia makombora yao yakigonga mwamba wa goli la West Brom.

Wawili hao walimwajibisha vilivyo kipa Sam Johnstone aliyefanya pia kazi ya ziada kwa kudhibiti fataki za Sam Surridge aliyepoteza penalti.

Ilikuwa hadi dakika ya 79 ambapo Stoke City almaarufu The Potters walipata bao la ushindi ambalo kwa mujibu wa kocha Val Ismael wa West Brom, wenyeji wao walistahili kufunga ikizingatiwa ubora waliodhihirisha uwanjani.

Ushindi huo uliosajiliwa na Stoke mbele ya mashabiki 22,703 wa nyumbani, uliwapaisha hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Championship

Pep Guardiola akiri kwamba Jurgen Klopp amemfanya kuwa kocha bora zaidi

Na MASHIRIKA

PEP Guardiola wa Manchester City amesema uhasama mkubwa kati yake na Jurgen Klopp wa Liverpool katika ulingo wa ukufunzi umemfanya kuwa “kocha bora”.

Ni pengo la alama moja pekee ndilo linawaweka Man-City ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) nyuma ya Liverpool ambao ni viongozi wa jedwali la kipute hicho kufikia sasa msimu huu.

Liverpool watakuwa wenyeji wa Man-City uwanjani Anfield mnamo Jumapili ya Oktoba 3, 2021. Mara ya pekee ambapo Man-City walikosa kunyanyua taji la EPL chini ya kipindi cha miaka minne iliyopita ni wakati Liverpool walipotawazwa mabingwa mnamo 2019-20.

“Tangu nitue hapa Uingereza – na si katika mwaka wangu wa kwanza – Liverpool wamekuwepo huku juu kwenye soka ya EPL,” akasema Guardiola. Guardiola ambaye ni raia wa Uhispania, alipokezwa mikoba ya Man-City mnamo Julai 2016 huku Klopp akianza kuwatia makali masogora wa Liverpool mnamo Oktoba 2015.

Kabla ya hapo, wakufunzi hao wawili waliwahi kukabiliana katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) wakati Guardiola alipokuwa akiwanoa Bayern Munich naye Klopp akiongoza kikosi cha Borussia Dortmund.

Guardiola amepoteza mechi nane dhidi ya Klopp katika mashindano yote, idadi hiyo ikiwa kubwa zaidi kuliko mkufunzi yeyote mwingine mpinzani wake.

 “Vikosi vinavyonolewa na Klopp vilinisaidia kuwa kocha bora,” akasema Guardiola atakayeongoza Man-City kuvaana na Liverpool ugenini siku chache baada ya kuwapiga Chelsea ligini kisha kutandikwa na Paris Saint-Germain (PSG) kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Klopp aliniweka katika kiwango tofauti na cha juu kabisa katika ulingo wa ukufunzi. Aliniweka katika ulazima wa kufikiri sana na kunichochea kujituma zaidi kudhihirisha ukubwa wa uwezo wangu.

Hayo yote yalichangia ubora wangu na akanidumisha katika kazi hii yenye panda-shuka tele,” akasema Guardiola. “Kwa miaka minne iliyopita, Liverpool na Man-City wamekuwa wakiwania nafasi mbili za kwanza kwenye jedwali la EPL.

Ni ishara ya ubora wa kila kocha na ukubwa wa ushindani kati ya timu hizo mbili. Lakini EPL si ya vikosi viwili. Kuna timu nyinginezo zilizo na uwezo wa kupigania ufalme wa kipute hicho,” akaeleza.

Mnamo Februari 2021, Liverpool walipigwa na Man-City 4-1 katika EPL ugani Anfield na Klopp amekiri kwamba masogora wake watakuwa na kiu ya kulipiza kisasi.

“Hii ni mechi spesheli sana kila msimu. Lazima uwe na masogora wako wote na kila mmoja awe katika fomu nzuri ndipo kocha apate nafasi ya kumbwaga mwenzake,” akasema Klopp.

“Pengine Man-City kwa sasa ndicho kikosi bora zaidi barani Ulaya kwa sasa. Walicheza dhidi ya Chelsea wikendi iliyopita na wakashinda wakati ambapo kila mmoja alikuwa akitazamia Chelsea washinde kutokana na uthabiti wao wa sasa.

Lakini mambo yalikwenda kinyume kwa sababu Man-City walicheza soka safi.” “Lazima tushinde mechi hiyo dhidi ya Man-City kwa kufunga mabao na pia kubana safu ya ulinzi ipasavyo,” akasema Klopp.

Matarajio makubwa ya mashabiki kutoka kwa Chelsea yanatutia presha – Tuchel

Na MASHIRIKA

KOCHA Thomas Tuchel wa Chelsea anatarajia beki Reece James kukosa mechi za timu ya taifa ya Uingereza kwa sababu ya jeraha.

Mnamo Septemba 30, 2021, James alijumuishwa katika kikosi kilichotajwa na kocha wa Uingereza, Gareth Southgate kwa minajili ya michuano ijayo ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 dhidi ya Andorra na Hungary.

Hata hivyo, Tuchel amesema maamuzi ya kujumuishwa kwa James, 21, kwenye kikosi hicho cha Uingereza ni “kosa la kutoeleweka kwa baadhi ya mambo.”“Nilishangaa sana kuona kwamba James ameitwa kambini mwa Uingereza.

Kwa sasa anauguza jeraha. Anashiriki mazoezi mepesi sana na sidhani atakuwa sehemu ya kikosi hicho cha Southgate.” Kulingana na uelewa wangu baada ya habari za hivi karibuni zaidi kutoka kwa madaktari wake, James hataungana na wenzake kambini mwa Uingereza.

Hivyo kuitwa kwake huenda kulichangiwa na kutoeleweka kwa baadhi ya mambo. Si chochote kingine,” akaongeza Tuchel. Aidha, mkufunzi huyo raia wa Ujerumani amesema kwamba ukubwa wa kiwango cha matarajio ya mashabiki kutoka kwa kikosi chake pia umeathiri uthabiti wa masogora wake kisaikolojia baada ya kikosi chake kupoteza mechi mbili mfululizo.

Chelsea walipigwa 1-0 na Juventus katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Septemba 29, 2021 baada ya kupokezwa kichapo sawa na hicho na mabingwa watetezi Manchester City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 25, 2021 ugani Stamford Bridge.

Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wa UEFA, watashuka dimbani mnamo Oktoba 2, 2021 kumenyana na Southampton katika EPL huku baadhi ya wachanganuzi wa soka wakiwapigia upatu wa kutwaa ufalme wa kivumbi hicho muhula huu.

“Sielewi kiini cha Chelsea kuwekwa mbele katika orodha ya wawaniaji halisi wa taji la EPL. Hilo linatutia presha bure. Kikosi kinaathirika zaidi kisaikolojia kinapopoteza mechi.

Ushindani ni mkali na hatuwezi kumbeza yeyote,” akasema kocha huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain (PSG) na Borussia Dortmund.

Rashford arejelea mazoezi baada ya kufanyiwa upasuaji kwenye mgongo mnamo Agosti 2021

Na MASHIRIKA

FOWADI Marcus Rashford amerejelea mazoezi kambini mwa Manchester United na alishiriki vipindi viwili vya mazoezi kwa mara ya kwanza mnamo Ijumaa tangu afanyiwe upasuaji kwenye mgongo.

Nyota huyo raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 23 hajawajibishwa katika mchuano wowote tangu alipoletwa uwanjani kama mchezaji wa akiba katika fainali ya Euro 2020 iliyokutanisha Uingereza na Italia mnamo Julai 11, 2021.

Rashford alikuwa na tatizo la mgongo kwa miezi kadhaa na alifanyiwa upasuaji mwanzoni mwa Agosti 2021. “Rashford alishiriki vipindi vya mazoezi kikamilifu kwa mara ya kwanza akikabiliana na wenzake kambini.

Ingawa alikabiliwa mara kwa mara na wanasoka wengine uwanjani, alionekana kuwa sawa na jambo hilo liliridhisha sana,” akasema kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Man-United.

Akizungumza na wanahabari mwishoni mwa kipindi hicho cha mazoezi kilichotumiwa na Man-United kujifua dhidi ya Everton katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 2, 2021, Solskjaer alikosoa waratibu wa kipute hicho.

Man-United waliopiga Villarreal 2-1 katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumatano usiku ugani Old Trafford watacheza tena saa 72 baadaye huku wapinzani wao wakuu Manchester City na Liverpool ambao wote walicheza Jumanne, wakisakata mechi zao za EPL mnamo Jumapili.

“Hatukupewa maelezo yoyote kuhusiana na hilo. Bila shaka ni kwa ajili ya mechi hizo kuonyeshwa moja kwa moja runingani. Tulikuwa na tatizo sawa na hilo mnamo 2020-21 ambapo tulirejea kutoka Uturuki na kushuka tena uwanjani mara moja,” akatanguliza.

“Sisi na Chelsea tulisakata mechi za UEFA mnamo Jumatano na ingekuwa rahisi sisi kucheza Jumapili nao Man-City na Liverpool walionogesha mechi zao za UEFA mnamo Jumanne wakipangiwa kutandaza michuano ya EPL mnamo Jumamosi,” akaeleza kocha huyo raia wa Norway.

Bayer Leverkusen yapepeta Celtic bila haya katika Europa League

Na MASHIRIKA

MWANZO mzuri wa Celtic katika mchuano wa Europa League dhidi ya Bayer Leverkusen ya Ujerumani ulifumuliwa na masihara ya mabeki wao walioruhusu wageni kuwaponda 4-0 katika mechi iliyowakutanisha usiku wa Alhamisi jijini Glasgow.

Makosa ya David Turnbull yalimpa fowadi Piero Hincapie fursa ya kuwafungulia Leverkusen ukurasa wa mabao katika dakika ya 25 kabla ya Florian Wirtz kufunga la pili baada ya kumwacha hoi kipa Joe Hart kunako dakika ya 35.

Ingawa Celtic walipania kurejea mchezoni katika kipindi cha pili, makali yao yalizimwa kirahisi na Lucas Hilario aliyefunga penalti katika dakika ya 58 kabla ya Amine Adli aliyetoka benchi katika kipindi cha pili kuzamisha kabisa chombo cha Celtic mwishoni mwa mchuano huo.

Kichapo kinawasaza Celtic mkiani mwa Kundi G bila alama yoyote na kwa sasa wanajiandaa kumenyana na Ferencvaros ambao pia hawajashinda mchuano wowote kufikia sasa.

Leverkusen na Real Betis wanajivunia rekodi ya kushinda mechi zao mbili za ufunguzi wa Kundi G. Celtic walitumia mchuano huo dhidi ya Leverkusen kama jukwaa mwafaka la kuwakaribisha kikosini wanasoka Kyogo Furuhashi na nahodha Callum McGregor ambao wamekuwa nje kwa kipindi kirefu kuuguza majeraha.

Leverkusen walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo wakipigiwa upatu wa kuibuka ushindi ikizingatiwa kwamba wamepoteza mechi moja pekee kufikia sasa muhula huu – kichapo cha 4-3 dhidi ya Borussia Dortmund katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Leverkusen hawajawahi kusajili sare katika mchuano wowote kati ya 21 iliyopita katika soka ya bara Ulaya. Kikosi hicho kimeshinda mara 13 na kupoteza mechi nane kati ya hizo.

Mechi dhidi ya Leverkusen ilikuwa ya kwanza kwa Celtic kutofunga bao katika mashindano ya bara Ulaya tangu Disemba 2019 walipopigwa 2-0 na CFR Cluj katika Europa League.

Sturridge apata hifadhi katika kikosi cha Perth Glory nchini Australia

Na MASHIRIKA

FOWADI wa zamani wa Liverpool na timu ya taifa ya Uingereza, Daniel Sturridge, ametia sani mkataba wa mwaka mmoja na kikosi cha Perth Glory cha Ligi Kuu ya Australia (A-League).

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 hakuwa na klabu tangu aagane na klabu ya Trabzonspor ya Uturuki mnamo Machi 2020.“Ni fursa njema kujaribu changamoto mpya kwingineko,” akasema Sturridge.

“Sturrdige ni miongoni mwa wanasoka stadi zaidi kuwahi kusajiliwa na kikosi cha Perth Glory na katika historia ya A-League,” akasema mmiliki wa kikosi hicho, Tony Sage.

Sturridge alihudumu kambini mwa Liverpool kwa misimu sita ambapo alifunga mabao 67 kutokana na mechi 160 kabla ya kutumwa kwa mkopo katika kikosi cha West Bromwich Albion kwa minajili ya nusu ya kampeni za msimu wa 2017-18.

Aliyoyomea Uturuki bila ada yoyote kuvalia jezi za Trabzonspor mnamo 2019 akiwa mchezaji huru.Mkataba wake wa miaka mitatu na Trabzonspor ulitamatishwa ghafla mnamo Machi 2020 baada ya sogora huyo wa zamani wa Manchester City na Chelsea kupigwa marufuku ya miezi minne kwa kukiuka kanuni zinazodhibiti mchezo wa kamari miongoni mwa wanasoka.

Kocha Ronald Koeman wa Barcelona asema amechoka kujitetea kutokana na matokeo duni

Na MASHIRIKA

KOCHA Ronald Koeman ambaye anakabiliwa na presha tele ya kupigwa kalamu na Barcelona amesema “amechoka” na matukio ya kujitetea mara kwa mara.

Kwa mujibu wa ripoti, mkufunzi huyo raia wa Uholanzi yuko pua na mdomo kutimuliwa na Barcelona baada ya miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kupoteza michuano miwili ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Anapojiandaa kuongoza kikosi chake kumenyana na mabingwa watetezi wa La Liga, Atletico Madrid, mnamo Oktoba 2, 2021, Koeman amesema kwamba mustakabali wake uwanjani Camp Nou haujulikani ila ana uhakika kwamba “umening’inizwa padogo” baada ya vichapo kutoka kwa Bayern Munich na Benfica kwenye hatua ya makundi ya UEFA.

“Hakuna yeyote ambaye amezungumza nami. Rais wa klabu, Joan Laporta, alikuwa hapa lakini sijafaulu kumuona kwa sababu tulikuwa tukijiandaa kwa mechi ijayo dhidi ya Atletico,” akatanguliza Koeman.

“Ningali hapa lakini nina macho na masikio ya kuchuja mengi yanayoendelea na kusikia. Hata hivyo, nimechoka kujitetea mara kwa mara kikosi kinapofanya vibaya. Haina haja kabisa. Leo si wakati mzuri ila naamini ipo siku ambapo nitazungumza kwa kina kuhusu mambo yanayosibu Barcelona kwa sasa,” akasema Koeman.

Ingawa hivyo, kocha huyo wa zamani wa Everton na timu ya taifa ya Uholanzi alikataa kujibu maswali ya jinsi anavyohusiana na Laporta na badala yake akasisitiza: “Ningali hapa.”

Uhusiano kati ya Laporta na Koeman ulianza kuingia baridi tangu Machi 2021 kinara huyo aliporejea kudhibiti usukani wa urais kambini mwa Barcelona.

Barcelona wamekuwa wakikabiliana na panda-shuka tele tangu waagane na supastaa raia wa Argentina, Lionel Messi aliyeyoyomea Ufaransa kuvalia jezi za Paris Saint-Germain (PSG) mwanzoni mwa msimu huu wa 2021-22.

Baada ya kupigwa 3-0 na Bayern katika mchuano wa kwanza wa UEFA msimu huu ugani Camp Nou, Barcelona walipokezwa kichapo sawa na hicho na Benfica mnamo Septemba 29 nchini Ureno.

Kufikia sasa, wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la La Liga huku pengo la alama tano likitamalaki kati yao na viongozi Real Madrid. Barcelona wamesajili sare tatu kutokana na mechi sita zilizopita za La Liga.

Kulingana na magazeti mengi nchini Uhispania, ni suala la muda tu kabla ya Koeman kupigwa kalamu na Barcelona waliojivunia huduma zake akiwa mchezaji mnamo 1992 waliponyanyua taji la European Cup.

Wachezaji wa Brighton na Southampton katika kikosi cha Mali kitakachopigania tiketi ya Kombe la Dunia dhidi ya Kenya

Na GEOFFREY ANENE

Mali imetaja Ijumaa kikosi cha wachezaji 29 kitakachovaana na Harambee Stars wakiwemo kiungo Yves Bissouma na mshambuliaji Moussa Djenepo wanaocheza kwenye Ligi Kuu nchini Uingereza.

Bissouma anachezea Brighton & Hove Albion naye Djenepo ni mali ya Southampton.Kipa Djigui Diarra anayetiwa makali ya kunyaka mpira na kocha Mkenya Razak Siwa katika klabu ya Young Africans (Yanga) nchini Tanzania, kipa Adama Malouda Traore ambaye klabu yake ya Sheriff Tiraspol iliduwaza miamba Real Madrid kwenye Klabu Bingwa Ulaya na Amadou Haidara (RB Leipzig) ni majina mengine makubwa katika timu ya Mali.

Eagles, ambavyo timu ya Mali inafahamika kwa jina la utani, itaalika Kenya nchini Morocco mnamo Oktoba 7 kabla ya kuzuru Nairobi mnamo Oktoba 10 kwa mechi ya marudiano.

Kenya ni ya pili katika Kundi E kwa alama mbili, mbili nyuma ya viongozi Mali, lakini sako kwa bako na Uganda. Rwanda inapatikana mkiani kwa alama moja.

VIKOSI:

Mali

Makipa – Djigui Diarra (Young Africans), Bosso Mounkoro (TP Mazembe), Mohamed Niare (Stade Malien), Ismael Diawara (Malmo); Mabeki – Hamari Traore (Rennes), Falaye Sacko (Guimaraes), Aboubacar Kouyate (Metz), Massadio Haidara (Lens), Mamadou Fofana (Amiens), Charles Traore (Nantes), Senou Coulibaly (Dijon), Moussa Sissako (Standard Liege); Viungo – Diadie Samassekou (Hoffenheim), Chieck Doucoure (Lens), Amadou Haidara (Leipzig), Lassana Coulibaly (Salernitana), Mohamed Camara (Salzburg), Aliou Dieng (Al Ahly), Adama Traore (Hatayspor), Kouame Nguessan (Troyes), Yves Bissouma (Brighton); Washambuliaji – Moussa Djenepo (Southampton), Moussa Doumbia (Reims), Kalifa Coulibaly (Nantes), Adama Malouda (Sheriff Tiraspol), Kevin Zohi (Vizela), Ibrahima Kone (Sarspborg), El Bilal Toure (Reims), Mahamadou Doucoure (Nimes).

Harambee Stars:

Makipa

Ian Otieno (Zesco, Zambia), Faruk Shikhalo (KMC, Tanzania), James Saruni (Ulinzi Stars), Brian Bwire (Tusker);

 Mabeki

Joseph Stanley Okumu (KAA Gent, Ubelgiji), Joash Onyango (Simba, Tanzania), David Odhiambo (Napsa, Zambia), Samuel Olwande (Kariobangi Sharks), Johnstone Omurwa (Wazito), Eugene Asike (Tusker), Frank Odhiambo (Gor Mahia), Daniel Sakari (Tusker), David Owino (KCB), Abud Omar (AEL Larisa, Ugiriki), Eric Ouma (AIK, Uswidi), Bolton Omwenga (Kagera Sugar, Tanzania);

 

Viungo

Richard Odada (Red Star Belgrade, Serbia), Lawrence Juma (Sofapaka), Patila Omoto (Kariobangi Sharks), Ismael Gonzalez (Real Murcia, Uhispania), Kenneth Muguna (Azam, Tanzania), Duke Abuya (Nkana, Zambia), Keagan Ndemi (Bandari), Boniface Muchiri (Tusker), Reagan Otieno (KCB), Erick Zakayo (Tusker), Ovella Ochieng (Marumo Gallants, Afrika Kusini), Philip Mayaka (Colorado Rapids, Amerika), Musa Masika (Wazito), Abdallah Hassan (Bandari);

 Washambuliaji

Michael Olunga (Al Duhail, Qatar), Henry Meja (Tusker, Kenya), Sydney Lokale (Kariobangi Sharks), Erick Kapaito (Kariobangi Sharks).

Pele aondoka hospitalini na kurejea nyumbani baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye utumbo

Na MASHIRIKA

JAGINA wa soka nchini Brazil, Pele, ameruhusiwa kuondoka hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji wa utumbo kuondoa uvimbe.

Nguli huyo wa kabumbu mwenye umri wa miaka 80 alifanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Albert Einstein jijini Sao Paulo mnamo Septemba 4, 2021.

Pele ambaye ni mchezaji wa pekee anayejivunia rekodi ya kushinda Kombe la Dunia mara tatu, alitolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi siku 10 baadaye japo akalazwa tena hospitani muda mfupi uliofuatia katika kile ambacho matatibu walisema ni hatua ya dharura ya kuzuia matatizo mengi.

“Nafurahia sana kurejea nyumbani. Nashukuru kikosi kizima cha matabibu katika Hospitali ya Albert Einstein. Wataalamu hao walifanya nikae hospitalini bila kuhangaika,” akasema Pele akiwa mwingi wa shukrani kwa mashabiki waliomtumia jumbe za heri pamoja na kumtakia afueni ya haraka.

Pele amekuwa akitibiwa hospitalini humo tangu Agosti 31 baada ya uvimbe kubainika kwenye utumbo wake.Afya ya Pele imezungumziwa mno nchini Brazil tangu afanyiwe upasuaji mwingine mnamo 2015 baada ya kulazwa hopsitalini kwa mara ya pili chini ya kipindi cha miezi sita.

Afya yake ilidorora tena mnamo 2019 na akalazwa hospitalini kwa wiki mbili. Pele ndiye mfungaji bora wa muda wote nchini Brazil na ni miongoni mwa wanasoka wanne pekee kuwahi kufunga bao katika fainali nne tofauti za Kombe la Dunia.

Kwa mujibu wa Guinness Book of World Records, Pele aliwahi kufunga mabao 1,279 kutokana na mechi 1,363 katika enzi zake kitaaluma. Kati ya mabao hayo ni 77 aliyofungia Brazil katika mechi 91 za kimataifa.

Mechi ya Europa League kati ya Marseille na Galatasaray yavurugwa na mashabiki

Na MASHIRIKA

FUJO za mashabiki uwanjani Stade Velodrome zilisababisha mchuano wa Europa League kati ya Olympique Marseille ya Ufaransa na Galatasaray ya Uturuki kusimamishwa kwa takriban dakika nane mnamo usiku wa Alhamisi usiku.

Vifaa butu vilirushwa uwanjani na mashabiki mwishoni mwa kipindi cha kwanza licha ya wafuasi wa pande zote mbili kutengwa ugani. Mechi hiyo ilisimamishwa baadaye ili kuwaruhusu maafisa wa polisi kurejesha utulivu uwanjani.

Kocha Fatih Terim wa Galatasaray na mahodha wa vikosi vya Galatasaray na Marseille – Fernando Muslera na Dimitri Payet mtawalia waliwakaribia mashabiki kwa nia ya kutuliza hali bila mafanikio.

Mechi hiyo ilirejelewa kwa dakika nane za mwisho wa kipindi cha kwanza baada ya vurugu iliyozuka kati ya beki wa Arsenal, William Saliba anayechezea Galatasaray kwa mkopo na fowadi Mbaye Diagne wa Marseille kutulizwa.

Si mara ya kwanza kwa Marseille kuhusika katika tukio kama hilo la mechi kusimamishwa kwa sababu ya vurugu kutoka kwa mashabiki wao. Payet aliwahi kutupiwa chupa ya maji uwanjani kabla ya naye kuiokota na kurejesha kwa mashabiki – tukio lililozua fujo wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) dhidi ya Nice.

Ushindi wa 3-2 uliosajiliwa tena na Marseille dhidi ya Montpellier katika Ligue 1 mnamo Agosti 2021 pia ulidumishwa licha ya mashabiki kurusha chupa, karatasi shashi na vifaa butu uwanjani kulalamikia baadhi ya maamuzi ya refa.

Okumu na timu yake ya Gent walitetemesha Europa League Conference

Na GEOFFREY ANENE

KAA Gent anayochezea Joseph Okumu iliendelea kutesa wapinzani kwenye mashindano ya daraja ya tatu ya Bara Ulaya (Europa League Conference) baada ya kulemea Anorthosis Famagusta ugani Ghelamco Arena mnamo Septemba 30.

Wenyeji Gent maarufu kama Buffalos, walipata bao la ufunguzi kutoka kwa Pavlos Korrea aliyejifunga alipogusa shuti kali la kutoka mbali kutoka kwa Tarik Tissoudali dakika ya 29.

Kisha, Sven Kums aliongeza bao la pili dakika ya 81 baada ya kukamilisha pasi murwa kutoka kwa Tissoudali aliyeibuka mchezaji bora wa mchuano huo. Wachezaji watano walionyeshwa kadi ya njano katika mchuano huu akiwemo Okumu kwa upande wa Gent.

Baada ya ushindi huo dhidi ya timu hiyo kutoka Cyprus unaofuata ule wa 1-0 dhidi ya Flora Tallinn (Estonia), Okumu anatarajiwa kucheza dhidi ya Antwerp kwenye Ligi Kuu ya Ubelgiji hapo Oktoba 3 kabla ya kuungana na timu ya taifa ya Kenya kwa mechi dhidi ya Mali za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Harry Kane afunga mabao matatu na kusaidia Spurs kutamba katika Europa Conference League

Na MASHIRIKA

FOWADI Harry Kane alitokea benchi na kufunga mabao matatu chini ya dakika 20 za kipindi cha pili na kusaidia waajiri wake Tottenham Hotspur kuchabanga NS Mura ya Slovenia 5-1 katika kivumbi cha Europa Conference League mnamo Alhamisi usiku.

Baada ya kusajili matokeo mseto katika mechi za mwanzo za kampeni mbalimbali za msimu huu, ikiwemo sare dhidi ya Rennes katika mchuano wa Kundi G kwenye Europa Conference League, Spurs walitamalaki kipute dhidi ya NS Mura na kumiliki asilimia kubwa ya mpira.

Kikosi hicho cha kocha Nuno Espirito kilifunga karamu ya mabao kupitia penalti ya Dele Alli katika dakika ya nne kabla ya Giovani lo Celso kufanya mambo kuwa 2-0 baada ya kukamilisha krosi ya Harry Winks katika dakika ya nane.

Ingawa Ziga Kous alipania kuwarejesha NS Mura mchezoni, chombo cha wageni hao kilizamishwa na Kane aliyefunga mabao matatu ya haraka katika dakika za 68, 77 na 88 mtawalia.

Kocha Nuno alikifanyia kikosi chake cha Spurs kilichopepetwa 3-1 na Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Septemba 26, 2021 mabadiliko tisa huku Alli na Sergio Reguilon pekee wakidumisha nafasi zao katika kikosi cha kwanza.

Penalti ambayo Spurs walipewa katika mechi hiyo ilitokana na Alli kuchezewa visivyo na kipa Matko Obradovic. Baada ya kuona kikosi chake kikilemewa na NS Mura, Nuno alilazimika kuleta uwanjani wanasoka Kane, Son Heung-Min na Lucas Moura katika dakika ya 60.

Spurs kwa sasa wanajiandaa kumenyana na Aston Villa mnamo Oktoba 3, 2021.Matokeo dhidi ya NS Mura yanasaza Spurs kileleni mwa Kundi G kwa alama sawa na Rennes walio na mabao machache licha ya kutoka nyuma na kupepeta Vitesse ya Uholanzi 2-1.

West Ham wapiga Rapid Vienna na kuweka hai matumaini ya kusonga mbele kwenye Europa League

Na MASHIRIKA

KOCHA David Moyes wa West Ham United amesema maazimio yake ni “kujaribu kusalia katika mashindano ya Europa League baada ya Krismasi” ya mwaka huu wa 2021 baada ya kikosi chake kupepeta Rapid Vienna ya Austria 2-0 mnamo Alhamisi usiku ugani London Stadium.

Declan Rice aliwafungulia West Ham ukurasa wa mabao katika dakika ya 29 kabla ya Said Benrahma kufunga goli la pili sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

West Ham walizamisha chombo cha Rapid Vienna katika Europa League wiki mbili baada ya kuwapepeta Dinamo Zagreb ya Croatia 2-0 katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi H mnamo Septemba 16, 2021.

Masogora wa Moyes sasa wanajiandaa kumenyana na Genk ya Ubelgiji katika mechi mbili zijazo za Kundi H.Kati ya wanasoka wengine wa West Ham waliopoteza nafasi za wazi za kufungia waajiri wao mabao ni Craig Dawson, Jarrod Bowen na Pablo Fornals.

“Napania kuhakikisha kwamba kikosi kinasalia katika Europa League baada ya Krismasi kwa kumaliza kampeni za makundi katika nafasi ya kwanza au ya pili.

Hatutalegeza kamba kabisa licha ya ushindani mkali tunaoshuhudia pia katika Ligi Kuu ya Uingereza,” akasema Moyes ambaye ni kocha wa zamani wa Manchester United na Everton.

Mechi ijayo ya West Ham ni kipute cha EPL kitakachowakutanisha na limbukeni Brentford katika uwanja wa London Stadium mnamo Oktoba 3, 2021.

Matumaini ya Leicester City kusonga mbele katika Europa League sasa yaning’inia padogo

Na MASHIRIKA

MASAIBU ya Leicester City katika Europa League yaliendelezwa na Legia Warsaw ya Poland iliyowapokeza kichapo cha 1-0 katika mchuano wa Kundi C uliowakutanisha mnamo Alhamisi usiku.

Chini ya kocha Brendan Rodgers, Leicester walishuka dimbani wakitarajiwa kujinyanyua baada ya kulazimishiwa sare ya 2-2 na Napoli katika mechi ya ufunguzi wa kampeni zao za Europa League msimu huu.

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Legia katika mchuano dhidi ya Leicester lilifumwa wavuni na Mahir Emreli wa Azerbaijan aliyemzidi ujanja beki Daniel Amartey nje ya kijisanduku na kuvurumisha kombora zito katika dakika ya 31.

Ingawa Leicester walisalia butu katika safu ya mbele, walipata nafasi kadhaa za kufunga mabao kupitia Ayoze Perez aliyeshirikiana vilivyo na Patson Daka.

Kiungo mkabaji Jannik Vestergaard alipoteza pia fursa maridhawa za kurejesha Leicester mchezoni ila fataki zake zikadhibitiwa vilivyo na kipa Cezary Miszta.

Mchuano mwingine wa Kundi C ulioshuhudia Spartak Moscow ya Urusi ikipepeta Napoli 3-2 ulitamalakiwa na drama tupu baada ya refa kuchomoa kadi 12 za manjano na mbili nyekundu.

Quincy Promes alifanya mambo kuwa 3-1 katika dakika ya 90 kabla ya Victor Osimhen kufungia Napoli bao la pili dakika nne baadaye. Hata hivyo, Napoli ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) ilikuwa tayari imelemewa katika takriban kila idara.

Leicester ambao ni washikilizi wa Kombe la FA, bado hawajapata dira kwenye mashindano mbalimbali ya msimu huu huku wakishinda mechi mbili pekee kati ya sita za ufunguzi za kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Hofu zaidi kwa kocha Rodgers ni udhaifu wa safu yake ya mbele iliyovurumisha makombora 18 langoni mwa wapinzani ila mafowadi wakashindwa kutikisa nyavu.

Kelechi Iheanacho alikosa mechi hiyo huku mfungaji bora Jamie Vardy akisalia benchi ili kumpisha sajili mpya Daka aliyenunuliwa kwa Sh3.4 bilioni mwanzoni mwa msimu huu kuongoza safu ya ushambuliaji.

Daka ambaye ni raia wa Zambia, alitua Leicester akipigiwa upatu wa kutamba ikizingatiwa kwamba aliwaongoza RB Salzburg ya Austria kunyanyua taji la Ligi Kuu kwa mara ya nne mfululizo baada ya kufungia miamba hao mabao 27 kutokana na mechi 28 za msimu wa 2020-21.

EPL kutuza vikosi vyenye idadi kubwa ya wanasoka waliochanjwa dhidi ya corona

Na MASHIRIKA

VINARA wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wanawazia uwezekano wa kuanza kutuza vikosi ambavyo vimehamasisha idadi kubwa ya wachezaji na wafanyakazi wao kupokea chanjo za corona.

Kumekuwa na hofu kuhusu kiwango cha kupokelewa kwa chanjo hizo miongoni mwa vikosi vya EPL huku chini ya nusu za wachezaji wa klabu zote za kipute hicho wakichanjwa.

“Tunawazia kuhusu jinsi ya kutuza vikosi ambavyo vimehimiza idadi kubwa ya wanasoka wao kuchanjwa. Tuzo pia zitatolewa katika kiwango cha mchezaji binafsi,” ikasema sehemu ya taarifa ya EPL.

Taarifa hiyo inatolewa baada ya kipa Karl Darlow wa Newcastle United kulazwa hospitalini kwa muda mrefu kwa sababu ya virusi vya corona ambavyo kiungo matata wa Chelsea na timu ya taifa ya Ufaransa, N’Golo Kante alipata wiki hii.

“Ni klabu saba pekee ambazo zina asilimia 50 ya wachezaji ambao wamechanjwa. Hivyo, bado tuna safari ndefu katika kufanikisha mpango wa kutoa chanjo,” ikasema sehemu nyingine ya taarifa ya EPL.

Kwa mujibu wa vinara wa EPL, kanuni za kudhibiti maambukizi ya corona zitaendelea kudumishwa uwanjani na katika maeneo yote ya mazoezi japo baadhi zitalegezwa mwishoni mwa mwaka huu wa 2021 iwapo idadi kubwa ya wadau watachanjwa.

West Ham kukosa wanasoka wawili tegemeo dhidi ya Rapid Vienna katika Europa League

Na MASHIRIKA

RYAN Fredericks atakosa kuwa sehemu ya kikosi kitakachowajibishwa na kocha David Moyes wa West Ham United dhidi ya Rapid Vienna ya Austria katika Europa League mnamo Septemba 30, 2021.

Nyota mwingine wa West Ham atakayekosa uhondo wa gozi hilo ni beki wa kulia, Vladimir Coufal.Fredericks alipata jeraha wiki iliyopita wakati wa mechi ya Carabao Cup iliyoshuhudia West Ham wakiwadengua Manchester United katika raundi ya tatu ya kivumbi hicho.

Coufal naye alijeruhiwa wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyokutanisha West Ham na Leeds United ugani Elland Road mnamo Septemba 25, 2021.

Mchuano dhidi ya Rapid Vienna ni wa kwanza kwa West Ham kutandaza katika uwanja wao wa nyumbani wa London Stadium katika soka ya bara Ulaya, kando na mechi za kufuzu kwa kipute hicho, tangu 2006.

Mchezaji wa mwisho kufungia West Ham bao katika gozi la bara Ulaya isipokuwa michuano ya kufuzu kwa kivumbi hicho ni Frank Lampard katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Osijek ya Croatia katika Uefa Cup mnamo 1999.

Rapid Vienna watashuka dimbani kumenyana na West Ham wakilenga kujinyanyua baada ya kupoteza mechi nne kati ya tano zilizopita katika mashindano yote. Kwa upande wao, West Ham watapania kuendeleza ubabe wao kwenye Europa League baada ya kuchabanga Dinamo Zagreb ya Ukraine kwa mabao 2-0 katika mchuano uliopita ugenini.

Mechi ya Europa League kati ya West Ham na Rapid Vienna inachezewa ugani London Stadium siku chache baada ya waajiri wa Moyes kuzindua minara mitatu kwa heshima ya wanasoka nguli wa West Ham –  Geoff Hurst, Bobby Moore na Martin Peters.

Watatu hao walikuwa sehemu ya kikosi kilichonyanyulia West Ham taji la European Cup Winners Cup mnamo 1965 na timu ya taifa ya Uingereza iliyotwaa Kombe la Dunia mnamo 1966.

Pigo kwa Arsenal jeraha likimweka nje kiungo Granit Xhaka kwa miezi mitatu

Na MASHIRIKA

KIUNGO Granit Xhaka wa Arsenal sasa atasalia mkekani kwa kipindi cha miezi mitatu kuuguza jeraha la goti alilolipata katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Tottenham Hotspur uwanjani Emirates.

Kwa mujibu wa Arsenal, nahodha huyo wa timu ya taifa ya Uswisi mwenye umri wa miaka 29 alipata jeraha baya kwenye goti lake la kushoto baada ya kuchezewa visivyo na fowadi Lucas Moura wa Spurs.

Hiyo ikawa sababu ya kuondolewa kwake uwanjani katika dakika ya 82 kwenye ushindi wa 3-1 waliousajili kwenye gozi hilo la London Kaskazini.“Hali yake imetathminiwa na madaktari na imebainika kwamba hatahitaji kufanyiwa upasuaji wowote.

Lakini atasalia nje kwa miezi mitatu kabla apone,” ikasema sehemu ya taarifa ya Arsenal.Xhaka amewajibishwa na Arsenal katika mechi nne kati ya sita ambazo zimetandazwa na Arsenal kwenye kampeni za EPL msimu huu.

Mbili kati ya mechi alizokosa ni sehemu ya marufuku ya mechi tatu aliyopigwa baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Manchester City mnamo Agosti 28, 2021.