Habari za Kitaifa

Abiria 13 wafariki katika ajali mbaya Salgaa

Na BENSON MATHEKA August 20th, 2024 1 min read

WATU 13 wamefariki Jumanne asubuhi, Agosti 20, 2024 baada ya magari kadhaa, likiwemo basi lililobeba abiria 60 kupata ajali katika barabara kuu ya Nakuru-Nairobi.

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilifichua kuwa takriban watu 36 walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyotokea karibu na eneo la Salgaa.

Kufuatia ajali hiyo, timu ya mashirika mengi inayojumuisha maafisa wa polisi ilitumwa kwenye eneo la tukio kusaidia kuokoa waliokuwa wamekwama kwenye ajali hiyo.

“Watu 36 waliojeruhiwa wamepelekwa katika Hospitali za Molo na Coptic kufuatia kisa cha trafiki barabarani kilichohusisha basi la abiria na magari mengi eneo la Migaa Molo, Kaunti ya Nakuru,” Shirika la Msalaba Mwekundu wa Kenya lilisema.

Basi hilo lilikuwa likielekea Mombasa kutoka Kakamega lilipopoteza mwelekeo na kugonga gari la saluni kabla ya kubingiria kwenye barabara kuu.

Waliojeruhiwa walikimbizwa katika hospitali za Coptic na Molo kwa matibabu, huku waliofariki wakipelekwa katika mochari za hospitali hizo hizo.

Wakati huo huo, polisi wameanzisha uchunguzi kubaini chanzo cha ajali hiyo.

Licha ya juhudi kubwa za uokoaji, kuna hofu kwamba watu zaidi wanaweza kuwa bado wamenaswa ndani ya mabaki ya basi.