Habari

Afisa wa GSU anayedaiwa kuua atupwa rumande siku 21

October 31st, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi wa kitengo cha General Service Unit (GSU) aliyekiri mahakamani Alhamisi kwamba alikodiwa kumuua mwanamke, atasalia rumande kwa siku 21.

Hakimu mkazi Bi Carolyne Muthoni Nzibe aliamuru mshukiwa azuiliwe hadi Novemba 21 kuwasaidia polisi kuwafikia washukiwa wengine wanne waliotorokea Mombasa, Kisii, Busia na Murang’a.

Akiungama mbele ya Bi Nzibe, mshukiwa Anthony Kilonzo Sammy alisema, “Niliulizwa na rafiki yangu twende kumuua mwanamke na mumewe na singekataa.”

Kilonzo alimweleza hakimu kuwa usiku wa Oktoba 26, 2019, walikuwa ni kiguu na njia hadi eneo la Katani, Mlolongo, Kaunti ya Machakos mwendo wa saa tatu usiku.

Mshukiwa wa mauaji Anthony Kilonzo Sammy (centre), ambaye pia ni afisa wa polisi wa kitengo cha General Service Unit (GSU), bewa la Embakasi B, kitengo cha Garrison, aondoka mahakamani Oktoba 31, 2019, baada ya polisi kuruhusiwa wamzuilie katika kituo cha Kilimani kwa siku 21 wakamilishe uchunguzi wa kisa cha ufyatulianaji risasi Katani, Kaunti ya Machakos. Picha/ Paul Waweru

“Tulivizia nje ya lango la makazi yao na mwanamke huyo na mumewe walipowasili niliwamiminia risasi na kusababisha vifo vya wawili. Mumewe mhanga alipata majeraha na yuko hospitalini,” Kilonzo aliyeonekana mwenye wasiwasi ameungama mbele ya hakimu.

Mshukiwa huyo alitoboa siri alivyotenda na washukiwa wengine walio mafichoni baada ya kuulizwa na hakimu iwapo alikuwa na jambo la kusema.

“Je una jambo la kusema? Upande wa mashtaka unaomba uzuiliwe kwa siku 21 kuhojiwa kuhusiana na mauaji ya watu wawili katika eneo la Katani, Mlolongo, Kaunti ya Machakos usiku wa Oktoba 26, 2019,” Bi Nzibe amemuambia Kilonzo.

“Naam, nina jambo la kusema. Ukweli ni kwamba niliulizwa na rafiki yangu nimsaidie kuua mwanamke mmoja. Sikuwa na budi ila kwenda kutekeleza mauaji hayo,” akaungama Kilonzo.

“ Sammy, je, unataka kuungama mlivyotenda?” Bi Nzibe alimwuliza.

Mshukiwa huyo hakusikia swali vizuri kisha akaendelea kusimulia yaliyojiri siku hiyo.

“Basi ikiwa unataka kuungamana kitendo hicho basi nitawapa polisi muda wa siku 21 kukuhoji,” Bi Nzibe alimweleza mshukiwa huyo. Utarudishwa kortini Novemba 21 kwa maagizo zaidi.

Hakimu huyo amemweleza mshukiwa atafikishwa mbele ya Inspekta Mkuu wa Polisi akiandamana na mtu wa familia yake na wakili kuungama kisa hicho kwa mujibu wa sheria.

Kueleza polisi

Mshukiwa ameshauriwa na mahakama asiendelee kutoboa siri kortini lakini awaeleze polisi madai hayo.

Akiwasilisha ombi la kutaka Kilonzo azuiliwe katika korokoro ya polisi kwa siku 21, Koplo Ezekiel Ngode, kutoka kitengo maalumu cha kushughulikia visa vya uhalifu katika ofisi ya idara ya uchunguzi wa jinai (DCI), aliomba mahakamani iamuru mshukiwa azuiliwe kwa siku 21.

Koplo Ngode amesema Kilonzo alitiwa nguvuni mtaani Kayole akipokea matibabu ya kidonda alichopata baada ya kupigwa risasi usiku huo wa Oktoba 26, 2019, na kudanganya wauguzi alijeruhiwa akiwa kazini katika kambi ya GSU Embakasi.

“Uchunguzi umedhihirisha Kilonzo alitoroka kambini Oktoba 23, 2019,” mahakama imefahamishwa.

Mahakama imefahamishwa mumewe Anita Wanjiru alijeruhiwa wakati wa kisa hicho na amelazwa katika hospitali ya Shalom, Kaunti ya Machakos.