Habari za Kitaifa

Afueni kidogo bei ya petroli, dizeli, mafuta taa ikishuka


WAKENYA wamepata afueni kidogo baada ya Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Kawi na Mafuta (Epra) kupunguza bei ya petroli, dizeli na mafuta taa kwa Sh1, Sh1.50 na Sh1.30 kwa lita moja, mtawalia.

Epra ilitoa tangazo hilo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumapili jioni, Julai 14, 2024.

 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mafuta na Kawi nchini Daniel Kiptoo. Picha|Maktaba

“Wakati wa kipindi hiki, bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta taa zitapungua kwa Sh1, Sh1.50 na Sh1.30, kwa lita, mtawalia,” Epra ikasema kwenye taarifa iliyotiwa saini na Mkurugenzi wake Mkuu, Daniel Kiptoo.

Hii ina maana kuwa wateja jijini Nairobi watanunua petroli kwa Sh188.84 kwa lita, kutoka bei ya mwezi jana ya Sh189.84.

Nayo dizeli itauzwa kwa Sh171.60 kwa lita kutoka Sh173.10 huku mafuta taa yakiuzwa kwa Sh161.75 kwa lita kutoka bei ya Sh163.05 ya tangu Juni 15, 2024.

“Bei hizi mpya zitatumika kuanzia Julai 15, 2024 hadi Agosti 15, 2024,” Epra ikaeleza.

Mamlaka hiyo ilisema kuwa bei hizo mpya, za petroli, dizeli na mafuta taa, zinajumuisha Ushuru wa Thamani (VAT) wa kima cha asilimia 16 kulingana na Sheria ya Fedha ya 2023, Sheria za Ushuru zilizofanyiwa marekebisho za 2020 zilizoanishwa na kiwango cha mfumko wa bei kwa mujibu wa Notisi ya Kisheria Nambari 194 ya 2020.

Bei ya mafuta katika soko la kimataifa imeshuka

Epra ilieleza kuwa bei za bidhaa hizo zilishuka kutokana na kushuka kwa bei zake katika masoko ya kimataifa.

Kwa mfano bei ya petroli iliyoingizwa nchini ilishuka kwa kima cha asilimia 4.65 kutoka dola 750.95 za Amerika (Sh97,623.5) kwa lita 100, mnamo Mei hadi dola 716.03 (Sh93,083.9) mnamo Juni.

Nayo dizeli ilishuka kwa kima cha asilimia 1.19 kutoka dola 690.99 (Sh89,828.7) kwa lita 1000 hadi dola 682.73 (Sh88,754.9)

Hata hivyo, bei ya mafuta taa iliongezeka kwa kima cha asilimia 2.01 kutokla dola 674.14 (Sh87,638.2) kwa lita 1000, mwezi Mei, hadi dola 692.80 (Sh90,064) mwezi Juni, 2024.

“Licha ya kupanda kwa bei ya mafuta taa katika masoko ya kigeni katika kipindi hicho, Epra bado ilipunguza bei ya mafuta ya rejareja kwa Sh1.30 kwa lita kutokana na sababu nyinginezo kama vile kuendelea kuimarika kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya dola ya Amerika,” Epra imeeleza.