Makala

Arati afunguka vurugu zilivyozuka

January 14th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

GAVANA wa Kisii, Simba Arati amesimulia jinsi vurugu zilizuka katika hafla aliyokuwa akisambaza basari katika eneobunge la Mugirango Kusini.

Bw Arati alikuwa akitoa fedha za ufadhili wa masomo katika soko la Nyakembeni, kundi la watu analodai linahusishwa na mbunge Silvanus Osoro lilipovamia hafla yake.

Bw Osoro ndiye mbunge wa Mugirango Kusini, na wakati wa ghasia hizo baadhi ya waliohudhuria mkutano huo wa Gavana Arati walijeruhiwa kwa risasi.

Gavana huyo wa chama cha upinzani, ODM, amefunguka akisimulia jinsi vita vilizuka.

“Kina mama walikuwa wanacheza, mimi naye ninaongea na wao. Kidogo naona watoto wanakimbia…Kumbe ni watu wanatoka kwenye gari wakiwa na AK47 (aina ya bunduki),” Arati akadokeza.

Kulingana na Gavana huyo anayehudumu muhula wake wa kwanza Kaunti ya Kisii, alipotaka kujua aliyesababisha vurugu anadai aliambiwa ni Bw Osoro.

Alisimulia, “Nilipouliza ni nani, nikaambiwa ni Osoro. Risasi zilipigwa nyingi. Watu walivunjika miguu. Yule kijana alikuwa amenipa kiti nyuma yangu, akapigwa risasi na kwa sasa yuko hospitalini. Kina mama wazee, wengine walikuwa wajawazito wengine walivunjika wako hospitalini”.

Kulingana na Bw Arati, risasi iliyogonga kijana aliyekuwa nyuma yake ilikuwa inamlenga.

“Nina uhakika ile risasi ilipigwa kijana aliyekuwa nyuma yangu, ilikuwa inanilenga…Nchi hii ina sheria na lazima zifuatwe,” akadai.

Kufuatia kisa hicho cha Januari 8, 2024, Bw Osoro, hata hivyo, amejitenga na mashambulizi hayo.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa Rais William Ruto na Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, baadaye akizungumzia wanahabari alidai mashambulizi hayo yalipangwa na Gavana Simba Arati akiwa na nia ya kujizolea umaarufu Kisii “kwa njia ya huruma”.

Si mara ya kwanza wanasiasa hao wawili kutoka Kisii wamezozana hadharani.

Februari 2021, waliingiana mangumi katika hafla iliyohudhuriwa na Dkt Ruto na kiongozi wa ODM Bw Raila Odinga.

Wakati huo, Ruto alikuwa Naibu wa Rais chini ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye kwa sasa ni mstaafu.

ODM inamtaka Osoro achukuliwe hatua kisheria kufuatia vurugu za majuzi.