Habari

Asasi za kupambana na ufisadi zatengewa fedha nyingi

June 14th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

SERIKALI Alhamisi ilionyesha juhudi za kuendelea kupigana na ufisadi baada ya kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa asasi za kupambana na wizi wa mali ya umma kwenye makadirio ya bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020.

Katika makadirio hayo, afisi zaMkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) naIdara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) zimepokea mgao mkubwa ikilinganishwa na mwaka uliopita, wadadisi wakisema hatua hiyo inatokana na juhudi zake katika vita hivyo.

Kwenye bajeti hiyo ya Sh3.02 trilioni, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilitengewa Sh2 bilioni, ODPP Sh3 bilioni, Idara ya Mahakama Sh19.4 bilioni, DCI ikitengewa Sh4.8 bilioni huku Bunge la Kitaifa likitengewa Sh40.5 bilioni.

Uimarishaji mikakati

Waziri wa Fedha, Henry Rotich alisema hatua hiyo inalenga kuziwezesha asasi hizo kuimarisha mikakati yao katika vita hivyo.

“Nyongeza hii inalenga kuhakikisha kuwa lengo la serikali kuwakabili wafisadi linafaulu bila vikwazo vyovyote,” akasema Bw Rotich.

Mwaka uliopita, Bunge lilitengewa Sh36.8 bilioni, Idara ya Mahakama Sh15.2 bilioni, EACC Sh2.9 bilioni huku DPP ikitengewa Sh2.9 bilioni.

Mara kwa mara, asasi hizo zimekuwa zikilaumiana kuhusu kutofaulu kwa kesi zinazowakabili wafisadi ambazo zinawasilishwa mahakamani.