Habari

Awiti akosa kufika mbele ya Seneti kwa kuugua

May 15th, 2019 2 min read

Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu (CPAIC) pia iliitaka serikali hiyo kuwasilisha ripoti kuhusu mradi wa afya wa kiasi cha Sh3.8 bilioni uliokwama katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Homa Bay.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa kaunti hiyo Moses Kajwang’, Jumanne ilitoa amri hiyo baada ya Gavana Awiti kufeli kufika mbele yake kutoa ufafanuzi kuhusu masuala hayo.

Katikati ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti Kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (CPAIC) Moses Otieno Kajwang’. Picha/ Charles Wasonga

“Tulirajia Gavana Cyprian Otieno Awiti kufika mbele ya kamati hii kujibu maswali ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu katika miaka ya kifedha ya 2015/2016, 2016/2017, 2017/2018. Hata hivyo, tumepokea barua iliyotiwa saini na Katibu wa Kaunti Isaiah Ogwe kwamba amesafiri ng’ambo kwa matibabu,” akasema Bw Kajwang.

“Hata hivyo, kwa kuwa suala hilo linahusu serikali nzima, tunaitaka kuwasilisha kwa kamati hii majibu yaliyoandikwa kwa maswali yote yaliyoibuliwa kwenye ripoti hiyo ndani ya siku saba kuanzia leo (jana Jumanne) ili tupate muda tosha wa kuyakagua kabla ya kukutana na gavana mwenyewe,” akaongeza.

Majibu kamilifu

Bw Kajwang alisema CPAIC itatoa tarehe nyingine ambapo Gavana Awiti atahitajika kufika mbele kutoa majibu kamilifu kwa maswali husika ikiwemo kukwama kwa mradi wa afya uliokadiriwa kugharimu Sh3.8 bilioni.

Katika barua yake Bw Ogwe anaiomba kamati hiyo kumruhusu Gavana Awiti kufika mbele yake Juni 2019 “kwa sababu amesafiri nje kwa ukaguzi wa kimatibabu.”

Hata hivyo, Bw Kajwang’ pamoja na wanachama wa CPAIC, Kimani Wamatangi (Kiambu), Charles Kabiru (Kirinyaga) na Ladema Ole Kina (Narok) walishikilia kuwa Bw Awiti sharti afike mbele yao ndani ya siku 30.

“Ikiwa muda huo utatamatika kabla ya Bw Awiti kufika mbele yetu Seneti, itahitaji Bunge la Homa Bay kubaini kuwa Bw Awiti anafaa kuendelea kuwa afisini kwa mujibu wa Katiba na sheria husika,” akasema Bw Kajwang’.

“Hata hivyo, tunamtakia afueni haraka ili aweza kurejelea majukumu ya afisi yake,” akama Ole Kina.

Duru zinasema kuwa Gavana Awiti amekuwa akiugua tangu mwanzoni mwa mwaka 2019 kiasi kwamba hajakuwa akionekana hadharani.

Naibu wake Hamilton Orata ndiye amekuwa akiendesha shughuli za kaunti hiyo huku taharuki ikitanda katika kaunti hiyo kuhusu utendakazi mbaya katika idara mbalimbali za kaunti hiyo.