Habari

Chimbuko la kushtua kuhusu Valentino Dei

February 14th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

WATU wengi wamekuwa wakiisubiri kwa hamu siku hii ya Valentino ili kuonyesha mapenzi kwa wapendwa wao kwa njia tofauti kote duniani.

Imekuwa desturi sasa kuwa inapowadia Februari 14 kila mwaka, haswa kwa vizazi vya sasa, unakuwa ndio muda muafaka wa watu kuonyeshana namna wanavyopendana.

Hata hivyo, watu wengi hawafahamu chimbuko la siku hii ambayo imegeuka kuwa kama sikukuu katika mataifa mengi, wengi wakiijua tu kuwa ni ‘siku ya wapendanao’. Kuna simulizi mbili zinazoeleza kuhusu asili ya siku ya Valentino.

Wateja wachagua zawadi za Valentino kw awapenzi wao jijini Nairobi Februari 14, 2019. Picha/ Peter Mburu

Kulingana na historia, siku ya Valentino haikuanza kwa kusherehekewa namna inavyoadhimishwa sasa, ila miaka ya awali, Waroma walikuwa na sherehe iliyoitwa Lupercalia.

Sherehe hii iliadhimishwa kati ya Febriari 13 na 15 kumshukuru ‘mungu’ wa uzazi ‘Lupercus’, ambapo mbuzi na mbwa walitolewa kafara na damu yake kunyunyiziwa wanawake waliokuwepo.

Hili lilifanywa kwa damu ya wanyama hao kupakwa kwenye ngozi, kisha wanawake ambao walikua uchi kuchapwachapwa, kwa imani kuwa vitendo hivyo vingefukuza pepo wa utasa. Wanawake walifurahia na kufika kufanyiwa hivyo.

Mwanamume asoma ujumbe kwenye ua la waridi jijini Nairobi Valentino Dei. Picha/ Peter Mburu

Anasa

Vilevile, ni sherehe iliyojawa na anasa, ambapo wanaume waliokota vijikaratasi vyenye majina ya wanawake, kisha wakaunganishwa kwenye sherehe hiyo kuiadhimisha pamoja, na mara kwa mara hata baada ya kuonyeshana mapenzi kwenye sherehe waliishia kupendana kikweli na hata kufunga ndoa.

Wakati huohuo, enzi hizo kulikuwa na mtawala wa Kiroma kwa jina Claudius II ambaye alithamini sana vita vya kijeshi na ambaye aliamini kuwa wanaume waliojihusisha na wanawake hawakupigana vyema.

Alianza kwa kuwafungia wanajeshi wake kutojihusisha na wake zao walipoelekea kushiriki vita, lakini baadaye akapiga marufuku kabisa ndoa katika himaya yake.

Duka la bidhaa za Valentino katika barabara ya Tom Mboya jijini Nairobi. Picha/ Peter Mburu

Hata hivyo, kulikuwa na padre wa Kiroma kwa jina St Valentine ambaye hakukubaliana naye na ambaye licha ya marufuku hiyo aliendelea kuunganisha vijana kuoana kisiri. Wakati Claudius II alipofahamu alivyokuwa akifanya Valentine, alimfunga jela.

Wawili hao wanaripotiwa kuwa walikuwa marafiki lakini Valentine akataka kumgeuza Claudius II kuokoka, jambo ambalo mtawala huyo hakufurahia. Ilimbidi kumlazimisha aidha awache wokovu, ama auawe. Valentine alichagua kuuawa badala ya kuacha wokovu.

Mapenzi 

Alipokuwa jela aidha, Valentine alipendana na bintiye mhukumu wake na kabla yake kuuawa, siku ya Februari 14, karne ya tatu, alimwandikia barua ya mapenzi binti huyo, ambayo ilitiwa sahihi “kutoka kwa Valentine wako.”

Aidha, wapenzi aliounganisha kisiri kinyume na sheria wanasemekana kuwa wangemtembelea katika seli alimokuwa akizuiliwa na kumpelekea maua na vijikaratasi vilivyoandikwa maneno ya kuonyesha mapenzi yao kwake, kama njia ya kumshukuru.

Wakenya walimiminika katika eneo la Kencom jijini Nairobi kutoa damu kuwafaa wenzao hospitalini kama ishara ya mapenzi. Picha/ Peter Mburu

Februari 14, Valentine aliuawa kulingana na sheria za himaya hiyo na maisha yakaendelea. Hata hivyo, miaka ya baadaye, kanisa la katoliki kupitia Pope Gelasius mnamo karne ya tano liliamua kuanza kusherehekea maisha ya St Valentine na vitendo vya uhai wake.

Pope Gelasius alifanya hivyo kwa kugeuza Februari 14, ambayo mwanzoni ilikuwa sikukuu ya wasio mcha Mungu ya ‘Lupercalia’, kusherehekea maisha ya St Valentine. Alimtaja Mtakatifu na kumworodhesha miongoni mwa watu waliouawa wakitetea haki.

Kadri muda ulivyosonga, watu walianza kutumia jina Valentine kuelezea hisia zao kwa wale waliowapenda na sherehe hii kupata umaarufu kote duniani, hata Afrika ambapo haikuwepo.

Leo hii, mamilioni ya watu kote duniani wanatumia maua, chokoleti na zawadi nyingine za kuonyesha namna mtu anavyomthamini mwingine kuonyeshana mapenzi na kuadhimisha sikukuu hii.