Makala

Chimbuko la mtaa wa Manguo ambapo wakazi huishi na viboko

January 21st, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KWA lugha ya Kikikuyu, kiboko huwa anaitwa ‘nguo’.

Kwa mtaa wa Manguo, ulio viungani mwa mji wa Nyahururu, Kaunti ya Nyandarua, uwepo wa wanyama hao ni jambo la kipekee.

Kwa miongo mingi, wenyeji wamekuwa wakikaa pamoja na viboko, wanaoishi katika Mto Ewaso Nyiro.

Ndipo ukaitwa ‘Manguo’, kumaanisha ‘Mahali pa Viboko’.

Kulingana na wakazi, wamekuwa wakiishi pamoja na viboko hao kwa amani kwa muda mrefu, ijapokuwa kumekuwa na visa kadhaa ambapo wanyama hao wamewashambulia wakazi au kuvamia makazi yao.

Eneo hilo pia limepakana na Mto Ewaso Nyiro, unaotoka katika Mlima wa Aberdare na kuelekea katika Kidimbwi cha Lorian, kilicho karibu na mji wa Nanyuki, Laikipia.

Viboko hao huishi katika mto huo.

Viwanja vya nyasi ambayo viboko hula wakitoka katika Mto Ewaso Nyiro. PICHA | WANDERI KAMAU

Kulingana na Bw James Maina, ambaye ni mkazi wa eneo hilo, viboko hao huwa wanatokea katika nyakati za usiku.

Anasema kwamba ijapokuwa huwa wanaishi kwa amani na wanyama hao, huweza tu kumshambulia mtu nyakati za usiku.

“Katika visa vya mashambulio vya wanyama hao ambavyo huwa vinaripotiwa, mara nyingi hutokea nyakati za usiku. Ni vigumu sana kuwaona nyakati za mchana,” akasema Bw Maina.

Kulingana na mkazi mwingine, Brenda Nafula, serikali inafaa kuchukua hatua kuhakikisha kwamba imeweka mikakati ya kuwahifadhi wanyama hao, kwani idadi yao inaendelea kupungua nchini.

Pia wanasema kuwa mtaa huo unafaa kupewa utambuzi wa kipekee, kwani licha ya mashambulio machache ambayo yamekuwa yakisababishwa na wanyama hao, wakazi wamekuwa wakitangamana nao bila matatizo yoyote.

“Huu ni mtaa wa kipekee. Ni vigumu sana kupata mtaa ambao wakazi wanaishi pamoja na viboko, ikizingatiwa ni wanyama wakali sana, hasa wanapochokozwa,” akasema Bi Nafula.

Wakazi wengine wanasema unafaa kujumuishwa kama maeneo ya kipekee nchini, kwani unapakana na msitu wa Marmanet na Mto Ewaso Nyiro.

“Utalii ni miongoni mwa vitega uchumi muhimu nchini. Hivyo, upekee wa mtaa huu unafaa kuwa changamoto kwa serikali ya kitaifa na ile ya Kaunti ya Nyandarua kuchukua mikakati ya kuuboresha ili kuwa kivutio cha watalii,” asema Bw Edward Mwangi, ambaye ni mkazi.

Viwanja vya nyasi ambayo viboko hula wakitoka katika Mto Ewaso Nyiro. PICHA | WANDERI KAMAU